Mandhari ya Hifadhi ya Ruaha. |
Shirika la Hifadhi Tanzania (TANAPA) limepewa miezi sita, liwe limefuta kampuni 11 zilizopewa maeneo ya kujenga ndani ya hifadhi ya Ruaha tangu Juni mwaka 2009 na kushindwa kufanya ujenzi.
Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira imeagiza hayo wakati ikiwasilisha maoni yake kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2013/2014, bungeni Dodoma juzi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli alisema sababu kubwa inayochangia Tanzania kuwa na idadi ndogo ya watalii ni uchache wa vyumba vya kulala watalii katika maeneo mengi nchini.
“Hata hivyo, kamati imegundua kuwa uchache huu wa hoteli katika hifadhi unachangiwa na baadhi ya wafanyabiashara waliopewa maeneo ya kujenga, kutoyaendeleza kwa muda mrefu,” alisema Lembeli ambaye ni Mbunge wa Kahama (CCM).
Alisema katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pekee, kampuni 11 ambazo zilipewa maeneo ya kujenga kuanzia Juni 2009 ikiwa ni miaka minne iliyopita, hadi leo hayajaanza ujenzi katika maeneo hayo.
Alitaja kampuni hizo kuwa ni ASB Tanzania Ltd, Ruhuji Ltd, Antelope Safaris Ltd, Pango Safaris Ltd, Kwihala Camp, Tourism Promotion Services Tanzania Ltd na Indian Ocean Hotels.
“Kamati inaona hatua hii ni hujuma dhidi ya maendeleo ya utalii nchini na inaitaka mamlaka husika kufuta vibali hivyo kama kampuni hizi hazijaanza ujenzi katika kipindi cha miezi sita ijayo,” alisema.
Aidha, alisema kwakuwa mwaka 2002 Serikali ilijiwekea lengo la kufikisha watalii milioni moja ifikapo mwaka 2010 na kwa kuwa katika mwaka wa fedha 2013/2014 kuna uwezekano mkubwa wa kufikisha zaidi ya watalii hao, ni vyema Serikali ijiwekee lengo jipya la idadi ya watalii watakaoingia nchini.
No comments:
Post a Comment