Shekhe Ponda Issa Ponda. |
Kesi ya uchochezi na wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59, inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Issa Ponda na wafuasi wake 49, jana ilitajwa kwa mara ya mwisho kabla ya kutolewa hukumu wiki ijayo.
Akiahirisha kesi hiyo jana Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Victoria Nongwa alisema kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na Mei 9 mwaka huu atasoma hukumu ya washitakiwa hao.
Awali hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Aprili 18 mwaka huu lakini Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana aliahirisha kwa kuwa Hakimu Nongwa, anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo.
Shekhe Ponda na wenzake wanakabiliwa na mashitaka ya uchochezi, kuingia kwa jinai na kujimilikisha isivyo halali kiwanja cha Chang’ombe Markazi, kinachomilikiwa na Kampuni ya Agritanza na wizi wa mali zenye thamani hiyo.
Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi 16 ambao walidai kuwa kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na Bakwata ambao waliamua kubadilishana eneo la ekari 40 za Kampuni ya Agritanza lililoko Kisarawe mkoani Pwani kwa lengo la kujenga Chuo Kikuu cha Waislamu.
Machi 4 mwaka huu, washitakiwa walipatikana na kesi ya kujibu na kuanza kujitetea ambapo walikuwa na mashahidi zaidi ya 50, wakiwemo washitakiwa wenyewe, ambao walikiri kukutwa eneo la tukio na kudai kuwa walikwenda kwa ajili ya ibada ya Itikafu ambayo hufanyika saa 9 usiku.
Wanadaiwa Oktoba 12 na 16 mwaka jana, katika eneo la Chang’ombe Markazi walipanga njama na katika hali iliyokuwa ikisababisha uvunjifu wa amani, waliingia na kujimilikisha kwa nguvu ardhi ya kampuni hiyo na kuiba mali zenye thamani ya Sh milioni 59.7.
Katika shitaka la uchochezi linalowakabili Shekhe Ponda na Mukadam ambao wanaendelea kusota rumande, inadaiwa katika eneo hilo la Chang’ombe Markazi kwa maelezo kuwa wao ni viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, waliwashawishi wafuasi wake ambao ni washitakiwa hao kutenda makosa hayo.
No comments:
Post a Comment