HALI SHWARI MTWARA, WALIOKAMATWA SASA WAFIKIA 121...

Polisi wakidhibiti hali ya usalama Mtwara.
Mji wa Mtwara ambao kwa siku mbili kuanzia Jumatano wiki hii uligubikwa na vurugu kubwa kiasi cha kuibua hofu ya usalama wa wakazi wake, imerejea katika hali ya kawaida, ingawa shughuli za kiuchumi zimeonekana kuendelea kusimama.

Vurugu hizo ziliibuka Jumatano asubuhi mara baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kusoma bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2013/14, huku sababu kubwa ikielezwa ni kutoridhishwa na uamuzi wa Serikali wa kusisitiza kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Hata hivyo, hatua ya baadhi ya watu hao ilionekana kuwa ni zaidi ya agenda ya gesi, kwani mara kadhaa viongozi wakuu wa nchi, akiwemo Rais Jakaya Kikwete walizungumzia umuhimu wa bomba hilo kwa uchumi wa nchi na pia ambavyo Mtwara itanufaika, huku akisisitiza mkoa huo haujapuuzwa na wala hautapuuzwa.
Uchunguzi wa gazeti hilo jana mjini Mtwara ulionesha kuwa, hali ya amani imerejea, kwani tofauti na ilivyokuwa siku mbili zilizopita, jana polisi wachache tu walionekana wakifanya doria na hakukuwa na purukushani yoyote.
Pamoja na kurejea kwa amani, shughuli za kiuchumi ziliendelea kusimama. Mathalani, hali ya usafiri wa daladala ambayo inatumiwa na wananchi wengi kwenda kazini na kwenye shughuli zingine za kiuchumi hazikuwepo, hivyo kufanya wananchi waendelee kubaki majumbani au kutembea kwa miguu.
Kuanzia saa sita mchana pikipiki chache zinazobeba abiria 'bodaboda’ zilianza kufanya kazi hivyo kupunguza kero ya usafiri, lakini hadi jioni ni bodaboda chache ndizo zilizokuwa zinaonekana barabarani.
Maduka, baa na huduma zingine za kiuchumi hazikufunguliwa hata wale wafanyakazi ambao wanapata chakula chao katika migahawa na hoteli mbalimballi hawakuweza kupata huduma hiyo.
Barabara nyingi ambazo awali zilikuwa na magogo, jana zilionekana nyeupe baada ya polisi, wanajeshi na raia wema kuanza kusafisha barabara hiyo kuanzia juzi jioni na jana jioni kwa kuondoa magogo hayo.
Aidha, usafiri wa mabasi ya mikoani ikiwa pamoja na kutoka Dar es Salaam uliokuwa umesimama kwa siku mbili huku mabasi yakiishia mjini Lindi, jana yalianza kufika Mtwara na basi la kwanza kufika hapa lilikuwa ni basi la Manning Nice ambalo lilifika mjini hapa saa 9.30 alasiri.
Lakini hata hivyo wasafiri wengi ambao walikuwa wamekwama Lindi waliparamia gari hilo na wakaonesha kufurahia baada ya kufika katika mji wa Mtwara.
“Siamini kama nimefika Mtwara, niligeuka mkimbizi pale Lindi na nilishaanza kuishiwa na fedha,” alisema Kassim Nachepe.
Lakini wasafiri wengi ambao walifika jana walihangaika kupata mahali pa kukaa kutokana na nyumba nyingi za wageni kuwa zimejaa kutokana na kutokuwepo kwa basi liloondoka mjini hapa.
Wananchi ambao walizungumza na gazeti hili jana walikiri kuwa hali ya jana ilikuwa ni ahueni tofauti na siku mbili zilizopita na wakashukuru Polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kurejesha hali ya usalama katika mji huo.
Wakati hali ya utulivu ikiendelea mjini Mtwara, imeelezwa kuwa idadi ya watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika katika vurugu za maandamano ya kupinga kusafirishwa kwa gesi  zilizosababisha kifo cha mtu mmoja na uharibifu wa mali na miundombinu, sasa imefikia 121.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu kutoka Mtwara, Kamanda wa Polisi Mkoani Mtwara, Linus Sinzumwa alisema watahakikisha washitakiwa hao wanafikishwa  mahakamani mapema baada ya upelelezi kukamilika.
Alisema tofauti na siku mbili zilizopita kwa sasa, jeshi hilo limedhibiti vurugu hizo,  hali ya mkoa huo imetulia na wananchi wanaendelea na shughuli za maendeleo kama kawaida.
Mei 22, mwaka huu zilitokea vurugu kubwa katika Manispaa ya Mtwara na viunga vyake, kiini kikiwa ni madai ya baadhi ya wananchi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa rasilimali ya gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Katika vurugu hizo ofisi ya Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtwara Mjini, Hasnain Mohamed Murji iliyopo Mikindani iliharibiwa na kuibiwa vitu mbalimbali, ofisi ya Mahakama ya Mwanzo ya Mitengo ilichomwa na kuteketea na nyaraka za ofisi.
Madhara mengine ni kuchomwa moto kwa ofisi ya CCM ya Kata ya Chikongola, kuchomwa moto kwa nyumba binafsi ya Ofisa Mtendaji Kata ya Magomeni, kuchomwa moto kwa nyumba ya Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) wa Mtwara, Kassim Mikongoro, kuibiwa na kuvunjwa kwa nyumba za askari wanne na kuibiwa vitu mbalimbali katika Ofisi ya Kata ya Chikongola.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Mei 15, mwaka huu, kikundi cha watu ambao hawakufahamika walisambaza vipeperushi vyenye lengo la kuhimiza wakazi wa Mtwara kuwa Ijumaa ya Mei 17, saa 3 asubuhi wasikilize hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ikisomwa bungeni ili kujua mustakabali wa gesi kutosafirishwa kutoka Mtwara.
“Vipeperushi hivyo vilihimiza huduma zote za kijamii zisimamishwe siku hiyo. Pamoja na vipeperushi hivyo, Mei 17, mwaka huu, huduma zote za kijamii kama vile usafiri wa magari (daladala), pikipiki (bodaboda) na baadhi ya bajaj zilifanya kazi wakati huduma za maduka na migahawa zilifungwa.
“Hata hivyo, hotuba hiyo haikusomwa bungeni siku hiyo. Kikundi hicho kiliendelea kuhamasisha kwa kutumia mitandao ya simu na karatasi za vipeperushi na kuwahimiza wananchi wasikilize hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo pindi itakaposomwa,” alisema Waziri Nchimbi.
Kutokana na kitendo hicho, Serikali imelaani vikali vurugu zilizotokea na imeapa kuwasaka waasisi wa vurugu hizo ndani na nje ya Mtwara na ndani na nje ya nchi ili waliohusika kupanga, kushawishi, kuandaa na kutekeleza vurugu hizo wafikishwe kwenye mkono wa sheria.

No comments: