BAJETI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI MWAKA 2013/2014...


HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHESHIMIWA DKT. EMMANUEL JOHN  NCHIMBI   (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
KWA MWAKA 2013/2014

I. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, baada ya kuzingatia taarifa iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.

2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kutumia  fursa hii kutoa masikitiko yangu kwa familia na wananchi kwa ujumla kutokana na vifo, ulemavu, upotevu na uharibifu wa mali na miundombinu vilivyosababishwa na ajali za barabarani, majini, kuporomoka kwa majengo na vifusi, vurugu na fujo katika mwaka mzima wa 2012. Aidha, nawapa pole ndugu na jamaa wa marehemu waliopoteza maisha yao katika matukio hayo. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

3. Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Anna Margareth Abdallah, Mbunge Viti Maalum kwa kuyachambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Naishukuru pia Kamati hiyo kwa maelekezo na ushauri wao wenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

4. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake aliyoitoa mapema katika mkutano huu wa Bunge ambayo imetoa mwelekeo wa kazi za Serikali kwa ujumla katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.

5. Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, kuhifadhi na kuwarekebisha wafungwa, kutekeleza Programu ya Huduma  kwa Jamii, kudhibiti uingiaji na utokaji nchini wa raia na wageni, kutoa huduma za zimamoto na uokoaji, kuwahudumia wakimbizi waliopo nchini, na kutoa vitambulisho vya Taifa. Majukumu haya yanatekelezwa kupitia Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Huduma kwa Jamii, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Wakimbizi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.


II.  HALI YA USALAMA NCHINI
Hali ya Uhalifu
6. Mheshimiwa Spika, kama inavyofahamika kwamba wajibu wa kwanza wa Serikali ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Umuhimu wa amani na utulivu kama msingi mkuu ambao umejengwa nchini na waasisi wa Taifa letu na mchango wake katika ustawi wa nchi yetu kiuchumi, kijamii na kisiasa umeendelea kuzingatiwa. Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza kikamilifu jukumu lake la kulinda na kudumisha amani na utulivu nchini kwa kubaini, kuzuia na kutanzua vitendo vya uhalifu, migogoro, vurugu, fujo na ukiukwaji wa Sheria za Usalama Barabarani.

7. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2012 makosa ya jinai makubwa na madogo 566,702 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi ikilinganishwa na makosa  564,716 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hiki mwaka 2011. Idadi ya makosa imeongezeka kwa asilimia 0.3. Tazama Jedwali Na. 1. Ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa makosa madogo kutokana na ushirikishwaji wa wananchi katika vita dhidi ya uhalifu na kuongezeka kwa wigo wa doria na misako ya Polisi Mijini na Vijijini.

8. Mheshimiwa Spika, makosa makubwa ya jinai yamegawanyika katika makundi matatu ambayo ni makosa dhidi ya binadamu, makosa ya kuwania mali na makosa dhidi ya maadili ya jamii. Idadi ya makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi imepungua kutoka 76,052 mwaka 2011 hadi 72,765 mwaka 2012 ikiwa ni sawa na upungufu wa asilimia 4.3. Mafanikio ya kupungua  idadi ya makosa makubwa ya jinai yanatokana na utekelezaji wa mikakati ya Jeshi la Polisi ya kuimarisha doria, misako  na operesheni maalum, ushirikishwaji wa wananchi katika mapambano dhidi ya uhalifu, ushirikiano wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola ndani ya nchi na ushirikiano wa Jeshi la Polisi na majeshi mengine ya Polisi kikanda na kimataifa.

Usalama Barabarani
9. Mheshimiwa Spika, pamoja na mikakati ya Jeshi la Polisi ya kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani, ajali hizi zimeendelea kusababisha vifo, majeraha na  ulemavu wa kudumu kwa wananchi pamoja na upotevu na uharibifu wa mali za wananchi, Taasisi na Serikali kwa ujumla. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2012  makosa makubwa ya usalama barabarani 23,604  yaliripotiwa katika vituo vya Polisi ambapo watu 4,062 walipoteza maisha na wengine 20,037 kujeruhiwa ikilinganishwa na makosa makubwa  24,078 yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi  Desemba, 2011 ambapo watu 4,013  walifariki na wengine 20,917 kujeruhiwa. Idadi ya makosa  ilipungua kwa asilimia  1.9. Tazama Jedwali Na. 1.

10. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wengine kama SUMATRA, TBS, TANROADS na Shule za Udereva zilizosajiliwa limeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti  ajali za barabarani zikiwemo kutoa elimu ya kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani kwa watumiaji wa barabara, kushirikisha wadau wa usalama barabarani katika kuhuisha mikakati ya kupunguza ajali za barabarani, kuendeleza doria za masafa mafupi na marefu katika kusimamia Sheria za Usalama Barabarani, kufanya ukaguzi wa magari, kutumia kamera za kutambua madereva wanaoendesha kwa mwendo kasi bila kuzingatia alama za usalama barabarani, kuendelea kusimamia zoezi la utoaji wa leseni mpya, kuwahamasisha wasafiri kutoa mapema taarifa za madereva wanaokiuka Sheria za Usalama Barabarani na kuwahamasisha wamiliki wa Mabasi kubandika kwenye Mabasi yao namba za simu za viongozi wa Polisi Usalama Barabarani. Kwa ujumla Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza maoni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yaliyoainishwa katika “Performance Audit Report on the Management of Traffic Inspections and Speed Limits in Tanzania” ya mwaka 2012. Taarifa hii inalitaka Jeshi la Polisi lijikite zaidi katika kuzuia na kudhibiti vyanzo vya ajali za barabarani vya mwendokasi, ulevi, uzembe wa madereva na kuzidisha abiria na mizigo.

Vitendo vya Uvunjifu wa Amani, Vurugu na Fujo
11. Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 15/02/2013, Mawaziri tisa kutoka Wizara za Katiba na Sheria, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Kilimo, Chakula na Ushirika, Nishati na Madini, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mambo ya Ndani ya Nchi pia Ofisi ya Rais, Utawala Bora na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa walihudhuria warsha iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi iliyofanyika hapa Dodoma kuhusu mipango ya Serikali katika kudumisha usalama nchini. Warsha hiyo ilitanguliwa na mkutano mkuu wa mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi uliofanyika kuanzia tarehe 12 – 14/02/2013 uliokuwa na kauli mbiu isemayo “Tujenge Uwezo wa Jamii na Polisi Kukabiliana na Vurugu kwa Kuimarisha Utii wa Sheria Bila Shuruti”. 

12. Mheshimiwa Spika, kufanyika kwa warsha hiyo ya Mawaziri kulitokana na kuendelea kuwepo kwa vitendo vya vurugu, fujo na uvunjifu wa amani vinavyotokana na migogoro ya kijamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Vurugu za kisiasa zilizotokea Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Singida na Iringa, migogoro ya ardhi iliyotokea Babati, Madale - Dar es Salaam, Sumbawanga, Ngorongoro, Rufiji na Kilosa, migogoro ya kidini iliyotokea Zanzibar, Mbeya, Temeke, Geita na mgogoro kuhusu uwekezaji katika sekta ya gesi Mkoani Mtwara, ni kati ya matukio mengi yanayoendelea kutokea nchini. Katika matukio hayo ya  vurugu, fujo na uvunjifu wa amani  watu kadhaa wamepoteza maisha wakiwemo askari polisi, wananchi  mbalimbali wamejeruhiwa na umefanyika uharibifu wa miundombinu, mazingira na mali za Serikali na watu binafsi.

13. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumejitokeza vurugu za udini ambapo zipo kesi 16 zilizohusisha jumla ya watuhumiwa 195. Kesi 13 tayari zimefikishwa Mahakamani na kesi tatu upelelezi bado unaendelea. Athari za vurugu za udini ni pamoja na uvunjifu wa amani. Serikali imejipanga vyema kuona kuwa hali hiyo haiendelei na haijirudii tena kwa ustawi wa Taifa letu.

14. Mheshimiwa Spika, matukio haya inawezekana yameacha makovu ya chuki za ki-itikadi na hisia za kulipiza kisasi miongoni mwa waathirika. Jeshi la Polisi limejizatiti kukabiliana na vitendo hivi  vya fujo, vurugu na uvunjifu wa amani kwani vikiachwa viendelee uchumi wa nchi utadorora kutokana na ushiriki hafifu wa wananchi kwenye shughuli za maendeleo unaosababishwa na hofu inayojengeka katika jamii ya Watanzania na wawekezaji wa ndani na nje kutokana na nchi kuelekea kupoteza sifa yake ya kuwa ni Kisiwa cha Amani.

15. Mheshimiwa Spika, naungana na Watanzania wenzangu kulaani vitendo vyote vya fujo na vurugu vilivyosababisha uvunjifu wa amani. Nawakemea vikali wale wote walioshiriki, kuwezesha, kufadhili, kuhamasisha, kuchochea na kushawishi jamii kushiriki katika vitendo vilivyosababisha vurugu hizo na hata umwagaji wa damu. Natoa pole kwa wahanga wote wa vurugu hizo. Hatua za kisheria kwa watuhumiwa zinaendelea kuchukuliwa.
16. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kuliomba Bunge lako Tukufu liendelee kuunga mkono kwa vitendo utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Jeshi la Polisi. Programu hii pamoja na mambo mengine, imelenga kuligeuza Jeshi la Polisi kuwa la kisasa, lenye watendaji wenye weledi na linaloshirikiana na jamii katika kubaini, kuzuia, kudhibiti na kukabili vitendo vya uhalifu, fujo na vurugu.

17. Mheshimiwa Spika, ninapenda kuwashukuru Mawaziri wenzangu waliohudhuria warsha iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi hapa Mjini Dodoma mwezi Februari 2013 kwa kutoa Tamko la Dodoma lililokubali kusimamia na kutekeleza mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu ya kuimarisha ulinzi na usalama nchini kwa:-
i) Kuliweka  suala la usalama kuwa ni moja ya vipaumbele vya Taifa
ii) Kutenga fedha za kutosha kuliwezesha Jeshi la Polisi kumudu kikamilifu wajibu wake wa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao
iii) Kutambua kwamba kila Wizara ni mdau katika suala la usalama na inayo wajibu wa kuepusha migogoro inayozalisha vurugu
iv) Kufanya tathmini ya maeneo ambayo ni vyanzo vya migogoro na kutafuta njia ya kuzuia/kutanzua migogoro hiyo. Kuimarisha/kuhuisha mifumo ya usimamizi wa sheria na uwajibikaji wa kila Idara ya Serikali
v) Kujenga ubia wa kiutendaji baina ya Wizara wanazoziongoza na vyombo vya ulinzi na usalama katika kubaini vyanzo vya migogoro na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia na kutanzua migogoro hiyo
vi) Kuliwezesha Jeshi la Polisi kwa rasilimali vifaa na miundombinu pindi Mikoa mipya inapoanzishwa
vii) Kurekebisha haraka na kwa vipaumbele upungufu wa kisera, kisheria na kikanuni unaoweza kuchangia mianya ya kusababisha migogoro ya kijamii

III. TAARIFA YA UTEKELEZAJI  WA MALENGO YA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010 KATIKA KIPINDI CHA 2012/2013
18. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina malengo 10 ya kutekeleza yanayotokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010. Taarifa ya utekelezaji wa malengo hayo kwa mwaka 2012/2013, ni kama ifuatavyo:-

19. Mheshimiwa Spika, lengo la kwanza ni kuendeleza mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya. Katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013 Jeshi la Polisi liliwahamasisha na  kushirikiana na wananchi katika Ulinzi Shirikishi ili kudhibiti uhalifu ukiwemo uingizaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya katika maeneo yao. Ushirikiano wa wananchi na vyombo vingine vya dola uliliwezesha Jeshi la Polisi kuwakamata watuhumiwa 546 wakiwa na jumla ya kilo 33.299 za dawa za kulevya za viwandani ambapo Cocaine ni  kilo 14.209, Heroine kilo 13.073 na Mandrax kilo 6.017. Aidha, watuhumiwa 6,730 walikamatwa  na kilo 37,704.201 za  dawa za kulevya za mashambani ambapo bhangi ni kilo 26,938.445 na mirungi kilo 10,765.756. Jumla ya ekari 211 za mashamba ya bhangi ziliteketezwa katika Kanda Maalum ya Kipolisi ya Tarime/Rorya na Mkoani Tanga.

20. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wananchi kupata taarifa za waingizaji, wasafirishaji na watumiaji wa dawa za kulevya.  Pia litaendelea kubaini mtandao wa wahalifu wa ndani na nje ya nchi unaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini kwa kushirikiana na Shirika la Polisi la Kimataifa (INTERPOL) kupata taarifa za kiintelijensia kuhusu wasafirishaji wa dawa za kulevya. Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Vyombo vya Ulinzi na Usalama cha kupambana na biashara ya dawa za kulevya kitaendelea kuimarishwa kwa kukiongezea rasilimali watu na vitendea kazi.

21. Mheshimiwa Spika, lengo la pili ni kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Magereza. Tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu bado ni kubwa licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kukabiliana nalo. Kulingana na takwimu, msongamano Magerezani kwa kiwango kikubwa unasababishwa na uwepo wa mahabusu wengi. Tarehe 1 Februari, 2013 idadi ya wafungwa na mahabusu waliokuwepo Magerezani ilifikia 34,355. Kati ya hao wafungwa walikuwa 16,330 na mahabusu 18,025 kama ilivyofafanuliwa katika Jedwali Na.2.

22. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013 jumla ya wafungwa 387 walikuwa wanatumikia kifungo cha nje kwa kutumia kanuni za kifungo cha nje za mwaka 1968. Tazama Jedwali Na. 3. Vile vile wafungwa 903 waliachiliwa na Mahakama ili kutumikia kifungo cha nje chini ya Sheria ya Huduma kwa Jamii kwa kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013. Aidha, wafungwa 3,814 walifaidika na msamaha wa Rais uliotolewa tarehe 9 Desemba, 2012 wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Hatua zingine zinazochukuliwa ili kupunguza msongamano ni pamoja na kuundwa kwa Jukwaa la Haki Jinai  chini ya uenyekiti wa Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo wajumbe wengine ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Mahakama. Jukumu la msingi la jukwaa hilo ni kuimarisha utoaji wa haki nchini.

23. Mheshimiwa Spika, lengo la tatu ni kuimarisha na kuboresha mfumo wa upelelezi wa makosa ya jinai ili kurahisisha uendelezaji wa kesi mahakamani. Kwa kutumia vyuo vya Taaluma ya Polisi vya Moshi na Kidatu, kati ya Julai 2012 hadi Februari 2013, Jeshi la Polisi limetoa mafunzo ya Intelijensia na mbinu za kisasa za upelelezi kwa wapelelezi 328. Wapelelezi 22 walipata mafunzo katika nchi za Marekani, Misri, Nigeria na Botswana. Jeshi la Polisi pia limepata vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kisayansi katika maabara iliyopo Makao Makuu ya Polisi. Vifaa hivyo vitaimarisha ung’amuzi wa wahalifu, ukaguzi na ukusanyaji wa vielelezo na ushahidi kwenye matukio makubwa ya uhalifu. Aidha, mchakato wa kuikabidhi Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kazi za kuendesha mashtaka Mahakamani umeendelea. Hadi sasa mchakato huo umekamilika katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya katika Mikoa 22 ya Kipolisi Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar. 

24. Mheshimiwa Spika, lengo la nne ni kuanzisha mpango wa kuwapatia askari nyumba bora za kuishi. Kutokana na mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari nchi nzima, Jeshi la Polisi limeanza utekelezaji wa mpango wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kupunguza ukubwa wa tatizo hili. Kwa kuanzia Jeshi la Polisi limeingia ubia wa kujengewa nyumba 350 katika Mkoa wa Polisi Kinondoni kuanzia mwaka wa fedha wa 2013/2014. Utaratibu uliofuatwa katika Mkoa wa Kinondoni utatumika kupunguza tatizo la makazi ya askari katika Mikoa yote nchini. Mkakati wa muda mrefu ni kujenga nyumba za gharama nafuu kwa kutumia Shirika la Uzalishaji Mali (Corporation Sole) la Jeshi la Polisi ambalo uanzishwaji wake utakamilika  hivi karibuni. Kwa sasa tumekamilisha ujenzi wa maghorofa 90 yaliyotoa nafasi ya makazi bora kwa askari 360 pamoja na familia zao. Jeshi la Polisi litaendelea kutumia fedha za bajeti ya maendeleo kujenga nyumba za askari kadri uwezo utakavyoruhusu.

25. Mheshimiwa Spika, lengo la tano ni kujenga vituo vya Polisi katika kila Tarafa nchini. Mikakati ya kupunguza tatizo la makazi itatumika pia kupeleka huduma ya polisi karibu na wananchi kwa kujenga vituo vya polisi katika kila Tarafa. Kutokana na mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi, Jeshi la Polisi litatumia Shirika la Uzalishaji Mali litakaloanzishwa na mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kujenga vituo vya Tarafa kwa awamu. Hivi sasa Jeshi la Polisi litaendeleza utekelezaji wa Polisi Jamii  kwa  kuwatumia Wakaguzi 526 wa Tarafa na askari Kata kutoa huduma za polisi kwa kutumia vituo vilivyopo karibu na Tarafa zisizo na vituo vya polisi hasa maeneo ya vijijini.

26. Mheshimiwa Spika, lengo la sita ni kuwapatia wananchi mafunzo ya Ulinzi Shirikishi ili wawe tayari kujilinda katika maeneo yao. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeanzisha kampeni mahsusi ya kuhamasisha Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali kuzingatia ukweli kwamba zinao wajibu wa kujenga miundombinu ya amani katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Tarafa na Kata kwa kutumia sheria na taratibu zilizopo. Jeshi la Polisi limeendelea kuwatumia Wakaguzi wa Tarafa/Jimbo na Askari Kata/Shehia kuwaelimisha wananchi  kwamba kila mmoja anawajibika kwa ulinzi wake binafsi, familia yake, jirani yake na jamii kwa ujumla tofauti na fikra potofu za baadhi ya watu kwamba usalama wa raia na mali zao ni jukumu la Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali pekee.

27. Mheshimiwa Spika, lengo la saba ni kuimarisha mafunzo ya askari wa vyombo vya ulinzi na usalama. Katika kipindi cha Julai  hadi Desemba  2012 askari 12,276 kutoka Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji wamepatiwa mafunzo katika fani mbalimbali ambapo Polisi ni 9,407, Magereza 2,413, Zimamoto na Uokoaji 72 na Uhamiaji 384. Mwaka 2013/2014, mafunzo yatatolewa kwa jumla ya askari 32,957 ambapo Polisi ni 30,000, Magereza 2,307 na  Uhamiaji 650.

28. Mheshimiwa Spika, lengo la nane ni kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora za kilimo katika maeneo ya Magereza. Katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Magereza  kwa kushirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Manyara, Lindi, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro na Morogoro na vile vile  kwa kushirikiana na  Kampuni ya Highland Seed Growers Ltd na TANSEED katika Mikoa ya Rukwa, Ruvuma na Kigoma kwa ujumla limelima hekta 990.2 za mashamba ya mbegu bora za kilimo na  matarajio ni kuvuna tani 2,000 za mbegu bora. Katika  mwaka 2013/2014, Jeshi la Magereza linatarajia kuhudumia hekta 3,175 za mazao mbalimbali kwa mategemeo ya kupata mavuno ya tani 4,500 iwapo hali ya hewa itakuwa nzuri.

29. Mheshimiwa Spika, lengo la tisa ni kutoa vitambulisho vya Taifa. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ina jukumu la kusimamia mfumo wa utambuzi na usajili wa watu pamoja na utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa Watanzania, wageni wakaazi na wakimbizi wanaostahili. Huu ni mfumo mpya ambao utakuwa na manufaa kwa Taifa katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiusalama.

30. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua mfumo wa utambuzi na usajili wa watu hapo tarehe 7 Februari 2013 Jijini Dar es Salaam. Tukio la uzinduzi liliambatana na Mheshimiwa Rais kukabidhiwa kitambulisho cha kwanza cha Taifa katika historia ya Tanzania. Hili ni jambo jema linalohitaji Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nchini kupongezwa. Aidha, vitambulisho vilitolewa pia kwa vikundi mbalimbali vinavyowakilisha jamii na viongozi Wakuu wa Kitaifa wakiwemo Marais wastaafu, Mawaziri Wakuu wastaafu, Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
31. Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni kuendelea kutoa vitambulisho vya Taifa kwa wafanyakazi  wa Wizara, Idara na Wakala wa Serikali wa Mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama wapatao 290,000, wakaazi 220,000 wa Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro, wakaazi 2,159,182 wa Mkoa wa Dar es Salaam na wakaazi 165,825 wa Zanzibar. Napenda kuwataarifu Watanzania wote kupitia Bunge lako Tukufu kwamba zoezi la utoaji wa vitambulisho vya Taifa ni endelevu ambalo litafanyika katika Mikoa na Wilaya zote za Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa vile zoezi hili haliendeshwi kwa kuzingatia misingi ya itikadi za kisiasa, kidini au kikabila, natoa rai kwamba sote tuweke mbele suala la uzalendo na kutoa ushirikiano wa dhati kwa NIDA katika kufanikisha utoaji wa vitambulisho hivi kwa maslahi ya Taifa letu.

32. Mheshimiwa Spika, lengo la kumi ni kuimarisha Vikosi vya Zimamoto na Uokoaji vyenye wataalam na zana za kisasa ili kukabiliana na majanga ya moto.  Katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2012 askari wa Zimamoto na Uokoaji 72 wamepatiwa mafunzo. Kati yao 12 wamepatiwa mafunzo nje ya nchi ya uokozi kwenye maji (7) na majengo marefu (5) na askari 60 wamepatiwa mafunzo ndani ya nchi. Jeshi pia limepata msaada kutoka Ujerumani wa kompyuta 100 na vifaa vya kinga ya moto. Ili kusogeza huduma za zimamoto na uokoaji karibu na wananchi, ujenzi wa kituo cha Zimamoto na Uokoaji eneo la Mwenge – Dar es Salaam unaendelea.

IV. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/2013 NA MALENGO YA MWAKA 2013/2014
33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilipangiwa kukusanya mapato ya shilingi 96,449,327,801. Hadi tarehe 28 Februari, 2013, Wizara ilikuwa imekusanya shilingi 76,990,955,792 sawa na asilimia 79.8 ya lengo la mwaka. Katika mwaka 2013/2014, Wizara ina lengo la kukusanya mapato ya shilingi 145,024,760,000. Nguvu zaidi zitaelekezwa katika kuziba mianya ya uvujaji wa mapato hususan katika kuimarisha na kuboresha matumizi ya benki kwa ajili ya kufanya malipo ya huduma zitolewazo na taasisi za Wizara.
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara iliidhinishiwa kutumia shilingi 555,540,268,000 kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Februari, 2013 jumla ya shilingi 337,534,661,068 zilikuwa zimetumika sawa na asilimia 60.8 ya bajeti ya mwaka mzima kama ifuatavyo:- Shilingi 178,838,875,099 zimetumika kulipia mishahara, Matumizi Mengineyo shilingi 148,977,021,516 na fedha za maendeleo ni shilingi 9,718,764,453. Katika mwaka 2013/2014, Wizara imetengewa shilingi 741,131,711,000 kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

JESHI LA POLISI
35. Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema hapo awali kwamba amani, utulivu na usalama wa nchi yetu ni mihimili mikuu ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wananchi wetu. Kuongezeka kwa tishio la uhalifu, fujo, migogoro na kuzorota kwa usalama wa raia huathiri mfumo mzima wa ustawi wa nchi  katika maeneo hayo matatu na kwa ujumla hudhoofisha nguvu za wananchi katika kujiletea maendeleo. Jeshi la Polisi Tanzania ndilo lenye jukumu  la kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinakuwepo wakati wote kwa kuweka mazingira salama kwa wananchi kuendesha shughuli za kujiletea maendeleo yao na  wakati huo huo kuvutia wawekezaji wa ndani na nje  kuwekeza  mitaji yao katika sekta za kiuchumi kwa faida ya maendeleo ya nchi yetu. Pamoja na ukweli huo, mafanikio ya hatua za Polisi yanategemea mashirikiano ya jamii na mtu mmoja mmoja.

Kuzuia na Kudhibiti Vitendo vya Uhalifu na Ajali za Barabarani
36. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi liliendelea kutekeleza jukumu lake la kisheria la kuhakikisha usalama, amani na utulivu vinakuwepo hapa nchini. Pamoja na changamoto zilizojitokeza, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuwalinda wananchi na mali zao, kusimamia utii wa sheria za nchi, kuzuia makosa ya jinai na usalama barabarani, kupeleleza makosa ya jinai, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wa makosa ya jinai na makosa ya usalama barabarani. Mafanikio haya yanathibitishwa na kupungua kwa makosa makubwa ya jinai yakiwemo mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha kwa kiwango cha asilimia 4.3 na kupungua kwa ajali za barabarani kwa asilimia 1.9. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha doria, misako na operesheni maalum ili kupunguza matishio ya uhalifu, makosa makubwa ya jinai na ajali za barabarani kwa kiwango cha asilimia 10.

Programu ya Maboresho ya Jeshi la Polisi
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi liliendelea kutumia fedha za bajeti zilizoidhinishwa na Bunge lako Tukufu kuimarisha mifumo ya kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu na makosa ya usalama barabarani na kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kazi za Polisi. Pia Jeshi la Polisi liliendelea kuimarisha mifumo ya menejimenti ya rasilimali watu na ustawi wa askari kijamii na kiuchumi, kuandaa mikakati mipya ya kupunguza tatizo la uhaba na uchakavu wa kambi na vituo vya Polisi, kupunguza tatizo la uhaba wa vitendea kazi hususan magari na pikipiki na kuhamasisha wananchi na wadau wa usalama wa raia kuhusu Ulinzi Shirikishi na Utii wa Sheria Bila Shuruti.

38. Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa kama sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Maboresho, Jeshi la Polisi limeanza utekelezaji wa mfumo wa kupima kiwango cha ufanisi wa Maafisa, Wakaguzi na askari kwa kutumia mkataba wa utendaji (Performance Contract) uliosainiwa kati ya mtendaji mmoja mmoja na kiongozi wake wa kazi. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litapima ufanisi wa utendaji kwa ngazi ya Mkoa/Kikosi, Wilaya, Tarafa/Jimbo na Kata/Shehia na litaendelea kutekeleza malengo na shabaha zilizomo katika maeneo saba ya maboresho  kama yalivyoidhinishwa na Baraza la Mawaziri mnamo tarehe 31 Machi 2011.
Mkakati wa Kupunguza Uhalifu
39. Mheshimiwa Spika, mkakati wa kupunguza uhalifu unaotumiwa pia na majeshi mengine ya Polisi duniani umelisaidia Jeshi la Polisi nchini kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu na wahalifu kwa kiwango kikubwa katika mwaka 2012/2013. Mkakati huo unaelekeza mbinu na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kabla uhalifu haujatendeka, baada ya uhalifu kutendeka, mshtakiwa anapofikishwa mahakamani na ufuatiliaji wa wahalifu wa kawaida na wahalifu wazoefu baada ya kumalizika kwa kesi zao mahakamani. Matumizi ya mbinu hizi yanahusisha ushirikiano wa karibu kati ya Jeshi la Polisi na vyombo vinavyounda Jukwaa la Haki Jinai pamoja na raia wema.

40. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mbinu zinazotumika kuzuia uhalifu kabla haujatendeka ni pamoja na kutambua maeneo hatarishi ambayo uhalifu hutendeka mara kwa mara na kuongeza doria ya askari Polisi na vikundi vya ulinzi shirikishi katika maeneo hayo na kufuatilia nyendo za wahalifu wazoefu mara wanapomaliza kutumikia adhabu gerezani. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaendelea kutumia mkakati wa kupunguza uhalifu ili kila Mkoa wa Kipolisi ufikie shabaha ya kupunguza uhalifu kwa asilimia 10.

Mauaji ya Wazee na Vikongwe Kwa Imani za Kishirikina
41. Mheshimiwa Spika, kumekuwa na wimbi la mauaji ya wazee na vikongwe hasa katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora, Mbeya, Rukwa, Iringa na Singida. Katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2012, takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha kwamba jumla ya wazee na vikongwe 1,271 waliuawa katika Mikoa hiyo kutokana na imani za kishirikina. Kati ya idadi hiyo, wanaume walikuwa 532 sawa na asilimia 41.9 na wanawake 739 sawa na asilimia 58.1. Serikali inalaani kwa nguvu zake zote mauaji haya ya wazee na imani za kishirikina katika karne hii ya 21.

42. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limeweka mikakati ifuatayo:-
i) Kuendelea kuwahamasisha wananchi kutekeleza kwa vitendo falsafa ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi kama mkakati mkuu wa kuzuia uhalifu katika maeneo wanayoishi
ii) Kuendelea kushirikiana na raia wema, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi zinazoratibu shughuli za waganga wa jadi kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani waganga wanaothibitika kupiga ramli za uchochezi na kusababisha mauaji ya wazee na vikongwe
iii) Kuendelea kushirikiana na raia wema na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani wahalifu wanaokodishwa kufanya mauaji ya wazee na vikongwe
iv) Kuendelea kutumia taarifa za kiintelijensia kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani wanaotuhumiwa kutoa fedha kwa waganga wa jadi kwa lengo la kuambiwa waliowaua ndugu zao au kupewa mbinu na masharti ya kupata utajiri wa haraka
v) Kuendelea kukiimarisha Kitengo cha Intelijensia cha Jeshi la Polisi kwa rasilimali watu na vitendea kazi kuanzia  ngazi ya Makao Makuu hadi ngazi ya Kata/Shehia ili kujenga uwezo wa kupata mapema taarifa za uhalifu Mijini na Vijijini
vi) Kuendelea kutumia Vikosi Kazi vya Kitaifa, Mikoa na Wilaya kuendesha operesheni maalum za kuzuia na kudhibiti ongezeko la mauaji ya wazee na vikongwe katika Mikoa iliyokithiri kwa mauaji hayo.
Natoa wito kwa Watanzania wote kushirikiana na Serikali kukomesha mauaji, hofu na unyanyasaji kwa wazee.

Huduma za Polisi Katika Tarafa/Jimbo, Kata/Shehia na Maeneo Maalum ya Uwekezaji
43. Mheshimiwa Spika, idadi ya watu na mahitaji ya huduma ya usalama wa raia na mali zao yanazidi kuongezeka kila mwaka hususan kwenye ngazi ya Tarafa/Jimbo, Kata/Shehia na maeneo mapya ya makazi na uwekezaji. Katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi lilinunua pikipiki 564 kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa Wakaguzi wa Tarafa kwa Tanzania Bara na Majimbo kwa Zanzibar. Aidha, vitengo vipya vilivyoanzishwa Makao Makuu ya Polisi kwa ajili ya kuratibu usalama katika migodi, ulinzi wa mazingira na usalama wa watalii vilianza kazi rasmi kwa kupatiwa watendaji hadi ngazi ya Kituo cha Polisi. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaongeza idadi ya askari katika Kata/Shehia ambazo ni tishio kwa uhalifu na kununua pikipiki kwa ajili ya kuimarisha doria na misako katika Kata /Shehia  hizo.

Kuongeza Matumizi ya TEHAMA Katika Kazi za Polisi
44. Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya mbinu za kutenda uhalifu na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia duniani ni changamoto kwa Jeshi la Polisi hivyo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni ya lazima ili kuongeza uwezo wa Jeshi la Polisi kubaini na kutanzua uhalifu nchini. Katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi limeajiri wataalam 355 wa fani ya TEHAMA ambao wanaendelea na mafunzo ya awali ya uaskari katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi. Mfumo wa kisasa wa kuchukua alama za vidole za watuhumiwa (Automated Fingerprints Information System - AFIS) umeendelea kusimikwa katika vituo vya Polisi. Aidha, Mkandarasi atakayesimika mfumo wa ufuatiliaji wa washtakiwa (Offender Management Information System - OMIS) ameanza kazi za awali katika Mkoa wa Dar es Salaam na Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litawapanga askari wapya wenye fani ya TEHAMA kufanya kazi katika Mikoa yote nchini na litaendelea kutekeleza awamu zinazofuata za miradi ya AFIS na OMIS kwa mujibu wa mikataba na uwezo wa kibajeti.

Jukwaa la Haki Jinai
45. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, ushirikiano wa kiutendaji kati ya Jeshi la Polisi na taasisi nyingine zinazounda Jukwaa la Haki Jinai ambazo ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Jeshi la Magereza na Mahakama uliendelea kuimarika. Viongozi wa Taasisi hizo walishiriki katika mkutano mkuu wa Maafisa Waandamizi wa Polisi uliofanyika Mjini Dodoma mwezi Februari 2013 na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha utoaji wa haki hapa nchini. Jeshi la Polisi lilijikita katika eneo la kuongeza ufanisi katika upelelezi wa makosa ya jinai na hivyo kufanikiwa kuongeza kiwango cha washtakiwa kupatikana na hatia kutoka asilimia 5 mwaka 2011 hadi asilimia 11.6 mwaka 2012. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaanza rasmi kutumia mitihani ya kupima ujuzi ili kujenga na kuongeza weledi wa askari wake katika fani za Intelijensia na upelelezi.
Udhibiti wa Uzagaaji wa Silaha Ndogondogo
46. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi liliendelea kuweka alama maalum katika silaha ndogondogo zinazomilikiwa na taasisi za Serikali, makampuni na watu binafsi kwa lengo la kudhibiti uzagaaji wa silaha na matumizi ya silaha hizo katika uhalifu. Katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013, jumla ya silaha 15,003 zimewekewa alama hiyo hivyo kufanya jumla ya silaha 52,607 zilizowekewa alama hiyo tangu zoezi hili lilipoanza mwaka 2009. Hadi sasa zoezi la kuweka alama kwenye silaha limefanyika katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, Tabora, Manyara, Singida, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara. Taasisi ambazo silaha zao zimewekewa alama maalum ni pamoja na Tanzania National Parks Authority (TANAPA), BARRICK GOLD, Bank of Tanzania (BoT), GRUMET GAMES RESERVES na Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA). Katika mwaka 2013/2014, zoezi hilo litaendelea kutekelezwa na sheria mpya ya kusimamia na kudhibiti umiliki na utumiaji wa silaha za kiraia inatarajiwa  kuanza kutumika.

Ushirikiano wa Polisi Kikanda na Kimataifa
47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi lilishiriki katika mafunzo, ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia, operesheni za kikanda na lilikuwa mwenyeji wa vikao vya kamati na mkutano mkuu wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) ambavyo vilifanyika Zanzibar na Dar es Salaam mwezi Septemba 2012 na Machi, 2013. Kwa mpangilio huo, Jeshi la Polisi liliendelea kushirikiana na Mashirika ya Polisi ya kikanda na kimataifa katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu hapa nchini.  Mashirika hayo ni pamoja na Shirikisho la Polisi la Kimataifa – Interpol, Shirikisho la Polisi la nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika – EAPCCO na Shirikisho la Polisi la nchi za Kusini mwa Afrika SARPCCO. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na majeshi mengine ya polisi kikanda na kimataifa ili kuimarisha udhibiti wa makosa yanayovuka mipaka ukiwemo ugaidi, uharamia, biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya kusafirisha binadamu, uhamiaji haramu, wizi wa magari, wizi wa kutumia mitandao ya TEHAMA, bidhaa bandia, biashara haramu ya silaha na  uchafuzi wa mazingira.

Kuimarisha Mifumo ya Menejimenti ya Rasilimaliwatu
48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, jumla ya askari 3,024 waliajiriwa na 5,637 wa vyeo mbalimbali walihudhuria mafunzo na kupandishwa vyeo. Mafunzo ya upandishwaji vyeo yalifanyika kama ifuatavyo:- Uofisa (200), Ukaguzi mdogo (597), RSM (47), Sajini Taji (404), Sajini (882) na Koplo (3,502). Aidha, Inspekta Jenerali wa Polisi alihamisha Maafisa, Wakaguzi na askari wapatao 540 kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji katika komandi za Jeshi la Polisi nchini na kuziba nafasi zilizoachwa wazi kutokana na Maafisa na askari kwenda nje ya nchi kushiriki katika Ulinzi wa Amani. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaajiri askari wapya 3,000 na kuwapandisha vyeo jumla ya askari 7,110 wakiwemo NCO wenye elimu ya shahada ya kwanza na shahada ya uzamili. Pia Jeshi la Polisi litaendelea kuwaruhusu Maafisa, Wakaguzi na askari kufanya mitihani maalum inayowawezesha kushiriki katika Operesheni za Ulinzi wa Amani ndani na nje ya nchi.

49. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, jumla ya Maafisa watano wamesimamishwa kazi, 12 mashtaka ya kijeshi yanaendelea dhidi yao na wengine 28 wameandikiwa barua za kujieleza kwa nini wasishtakiwe kijeshi kutokana na makosa mbalimbali ya kinidhamu.

Ushughulikiaji wa Malalamiko
50. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya watendaji wachache wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo kuomba na kupokea rushwa. Katika mwaka 2012 malalamiko yaliyopokelewa yalikuwa 314 ikilinganishwa na malalamiko 340 yaliyopokelewa mwaka 2011. Malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi yalikuwa 193 na 121 yalikuwa ni madai ya askari kuhusu stahiki zao mbalimbali. Malalamiko 213 kati ya 314 yamejibiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kutokana na ushughulikiaji wa malalamiko mbalimbali ya ukiukwaji wa maadili askari 99 walishtakiwa kijeshi na kufukuzwa kazi na mwingine mmoja amesimamishwa kazi kutokana na kukiuka maadili ya ajira ndani ya Jeshi la Polisi hali iliyosababisha askari wanafunzi 95 kutopokelewa kuanza mafunzo katika Chuo cha Polisi Moshi.

51. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho askari 13 walitunukiwa sifa na zawadi ya jumla ya shilingi 7,540,000 kwa kukataa kupokea rushwa. Askari hao ni wa Mikoa ya Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Rukwa, Shinyanga, Temeke na Kaskazini Pemba. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia nidhamu na maadili ya Maafisa, Wakaguzi na askari wake ikiwa ni pamoja na kutoa ufumbuzi wa haraka wa malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi. Jeshi litaendelea pia kutekeleza Programu ya Kupambana na Rushwa nchini inayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (DFID).

Kuimarisha Miundombinu na Vitendea Kazi vya Polisi
52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi liliendeleza ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi Dar es Salaam, kuanza hatua za awali za kusimika mfumo wa OMIS na kukamilisha awamu ya kwanza ya  utekelezaji wa mradi wa kuimarisha usalama wa mizigo na huduma zinazosafirishwa kupitia barabara kuu za Tanzania hususan barabara kuu ya Dar es Salaam hadi Rusumo. Miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 10.1 haikuendelezwa kutokana na ufinyu wa bajeti ya maendeleo. Aidha, taratibu za kisheria za kuanzisha Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi (Police Force Corporation Sole) zimekamilika. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaendeleza ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi, Kituo cha Polisi Vikokotoni, kukamilisha ujenzi wa nyumba za askari katika Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara na Iringa na kuendeleza miradi ya AFIS na OMIS. Kuhusu vitendea kazi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inakamilisha taratibu za kupata magari ya aina mbalimbali kwa ajili ya kazi za Jeshi la Polisi kupitia ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Serikali ya Watu wa China na India.


JESHI LA MAGEREZA
Usafirishaji wa Mahabusu Kwenda Mahakamani na Kurudi Magerezani
53. Mheshimiwa Spika, jukumu la kuwasindikiza mahabusu kwenda Mahakamani na kurudi Gerezani linaendelea kutekelezwa katika Mikoa ya Dar es Salaam na  Pwani. Hivi karibuni jukumu hili limeanza kutekelezwa katika Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Dodoma katika Wilaya tatu za Dodoma Mjini, Dodoma Vijijini na Mpwapwa. Utaratibu huu umeonyesha mafanikio katika suala zima la kupunguza msongamano wa mahabusu Magerezani kwa sababu mahabusu hufikishwa Mahakamani kwa tarehe walizopangiwa na Mahakama ambapo wengine huachiliwa kwa dhamana au kesi zao kufutwa na nyingine kumalizika kwa mujibu wa sheria. Lengo la mwaka 2013/2014, ni kutekeleza jukumu hili katika Wilaya za Mkoa wa Dodoma zitakazokuwa zimesalia na kuanza katika Mkoa wa Mwanza.

Programu za Urekebishaji wa Wafungwa
54. Mheshimiwa Spika, mradi wa uendeshaji wa shughuli za wafungwa kwa kutumia mtandao wa kompyuta kwa awamu ya pili unaendelea baada ya awamu ya kwanza kukamilika. Utekelezaji wa awamu ya pili umeanza kwa kusimika miundombinu katika Magereza ya Butimba – Mwanza, Uyui - Tabora na ofisi za Magereza katika Mikoa hiyo. Kazi kama hiyo inatarajiwa kufanyika katika ofisi ya Magereza Mkoa wa Dodoma, Gereza Kuu la Isanga na Msalato. Kwa ujumla mfumo huu umesaidia kujenga uwezo wa Jeshi la Magereza katika upatikanaji wa taarifa za wahalifu zilizo sahihi na kwa wakati, kujua maendeleo na mwenendo mzima wa wahalifu katika maeneo mbalimbali yaliyounganishwa katika mfumo huu. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Magereza litaendelea na awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango huu kwa Mikoa mingine mitatu ambayo itaanzia na vituo vya Magereza Makuu ya Ruanda - Mbeya, Maweni – Tanga na Arusha kisha kumalizia ofisi za Magereza katika Mikoa ya Mbeya, Tanga na Arusha.

Ajira na Mafunzo
55. Mheshimiwa Spika, kibali cha kuajiri askari wapya 1,000 kimepatikana na mchakato wa ajira umeanza. Jumla ya watumishi 2,413 wamepatiwa mafunzo. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Magereza linatarajia kuajiri askari wapya 1,020 na watumishi raia 15 wa fani mbalimbali na kuwapatia mafunzo watumishi 520  nje ya Vyuo vya Jeshi la Magereza na askari 1,787 ndani ya vyuo vya Jeshi.

Uimarishaji wa Magereza Yenye Ulinzi Mkali
56. Mheshimiwa Spika, ukarabati na uboreshaji wa majengo na miundombinu ya Magereza yenye ulinzi mkali umefanyika na unaendelea katika Gereza la Butimba sehemu za wanawake, kiwanda na mahabusu. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, ukarabati wa majengo na miundombinu utaendelea chini ya Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria nchini ( LSRP) katika Sehemu ya Wanawake ya Magereza ya Ruanda – Mbeya, Karanga – Kilimanjaro, Musoma – Mara, Isanga – Dodoma na Lilungu – Mtwara.

Upanuzi, Ukamilishaji, Ukarabati na Ujenzi wa Mabweni ya Wafungwa
57. Mheshimiwa Spika, kazi ya ujenzi wa mabweni ya wafungwa katika Gereza la Wilaya ya Chato unaendelea. Ukarabati wa ukuta wa ngome, upanuzi wa sehemu ya wanawake na kuezeka upya mabweni ya wafungwa iliendelea katika Magereza ya  Kilwa na Bukoba. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, lengo ni kuanza kazi ya ukarabati wa mabweni ya wafungwa katika Gereza la Mahabusu Sumbawanga na kuendeleza ujenzi wa mabweni mapya katika Gereza Mkuza – Pwani.

Ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Magereza wa Mikoa
58. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Magereza limeendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa Ofisi ya Magereza Mkoa wa Singida na ujenzi wa Ofisi ya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi litakamilisha ujenzi wa Ofisi ya Magereza Mkoa wa Singida, kuendeleza ujenzi wa Ofisi ya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam na kuanza ujenzi wa Ofisi ya Magereza Mkoa wa Tanga.



Matumizi ya Nishati Mbadala Magerezani
59. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na matumizi makubwa ya kuni Magerezani na hivyo kuwepo na tishio la uharibifu wa mazingira, Jeshi la Magereza limeendelea kuchukua hatua za kuanza kutumia gesi asilia (natural gas), gesi itokanayo na tungamotaka (biogas)  na makaa ya mawe kama nishati mbadala kwa kupikia chakula cha wafungwa Magerezani. Mfumo wa gesi itokanayo na tungamotaka katika Gereza Ukonga umekamilika na umeanza kutumika. Matumizi ya makaa ya mawe yanaendelea katika Magereza ya Mkoa wa Mbeya. Kwa sasa Jeshi la Magereza lipo katika mchakato wa kutumia majiko yanayotumia kuni kidogo ambayo yameanza kutumika katika Gereza Karanga – Moshi na Ilagala – Kigoma. Matarajio ni kueneza matumizi ya nishati hii katika Magereza mengine yenye matumizi makubwa ya kuni kadri uwezo wa fedha utakavyoruhusu.

Ujenzi na Ukamilishaji wa Nyumba za Askari
60. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limekamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa la kuishi askari Mkoani Iringa na limeanza kutumika. Aidha, Jeshi linaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba zilizojengwa kwa njia ya ubunifu katika Magereza ya Ngara, Kasulu, King’ang’a, Mwanga, Masasi, Ngudu, Kenegele, Nzega na Kambi ya Bugorola. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Jeshi la Magereza litaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba katika Magereza ya Butimba, Karanga na Mugumu. Aidha, nyumba zilizojengwa kwa ubunifu wa askari ambazo zipo katika hatua mbalimbali pia zitaendelea kupewa kipaumbele katika ukamilishaji wake.

Uimarishaji wa Mifumo ya Majisafi na Majitaka
61. Mheshimiwa Spika, Magereza yaliyo mengi yanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji na uchakavu wa miundombinu ya majisafi na majitaka ambayo pia inaelemewa na tatizo kubwa la msongamano wa wafungwa na mahabusu. Katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, ujenzi wa miundombinu ya majisafi umeendelea katika Gereza Isupilo - Iringa na ujenzi wa mfumo wa majitaka unaendelea katika Gereza Mkwaya – Mbinga. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, lengo ni kukarabati mfumo wa majitaka na kuboresha mfumo wa majisafi katika Gereza Kuu Isanga.

Kilimo cha Umwagiliaji
62. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza liliendelea na mchakato wa ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji katika Gereza la Idete – Morogoro. Hatua mbalimbali za kufanya tathmini ya athari za mazingira na usanifu wa michoro kwa ajili ya mradi huo zimekamilika. Aidha, taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi zinaendelea.  Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Jeshi la Magereza litaanza mchakato wa mradi wa umwagiliaji katika Gereza Kitengule – Kagera uwezo wa fedha ukiruhusu.


Ununuzi wa Magari na Zana za Kilimo
63. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza bajeti ya mwaka 2012/2013, Jeshi la Magereza halikuweza kununua matrekta kutokana na ukosefu wa fedha. Malengo kwa mwaka 2013/2014, ni kuendelea kuyafanyia matengenezo matrekta yaliyopo pamoja na zana zake. Aidha, katika kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji Magerezani, Jeshi la Magereza linatarajia kununua magari madogo matatu kwa ajili ya shughuli za utawala.

Shirika la Magereza
64. Mheshimiwa Spika, Shirika la Magereza limeendelea na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na viwanda vidogo vidogo kwa kutengeneza samani za ofisi na bidhaa za ngozi kwa ajili ya taasisi na Idara za Serikali na watu binafsi. Kwa upande wa kilimo, eneo la ekari 6,400 limelimwa kwa matarajio ya kuvuna tani 8,640 za mazao mbalimbali. Vile vile Shirika kupitia Kikosi Ujenzi cha Magereza limeendelea kufanya kazi za ujenzi wa majengo ya taasisi za Serikali na watu binafsi. Kazi hizo ni pamoja na ujenzi wa uzio wa Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ukarabati wa majengo ya Idara ya Uhamiaji Mkoani Tanga, ujenzi wa Rest House ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na ujenzi wa mfumo wa majitaka Baraza la Mitihani la Taifa. Matarajio ya mwaka 2013/2014, ni kuongeza shughuli za uzalishaji kupitia miradi ya kilimo, mifugo na kutumia ipasavyo soko la samani za ofisi, bidhaa za ngozi na shughuli za ujenzi ambalo linaendelea kupanuka.

HUDUMA KWA JAMII
65. Mheshimiwa Spika, Programu ya Huduma kwa Jamii ilianza rasmi mwaka 2005 kama adhabu mbadala ya kifungo gerezani. Hivi sasa programu hii inatekelezwa katika Mikoa 16 ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Iringa, Kagera, Mara, Shinyanga, Ruvuma, Pwani, Geita na Morogoro. Katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013 jumla ya wafungwa 903 wamefaidika na programu hii. Wafungwa hao hutumikia vifungo vyao nje ya magereza kwa kufanya kazi bila ya malipo katika taasisi za umma. Changamoto kubwa ya programu hii ni Mikoa mingine kushindwa kunufaika nayo kutokana na ufinyu wa bajeti, uhaba wa Maofisa wa Probesheni na baadhi ya Mahakimu kujikita katika kutoa adhabu ya kifungo gerezani badala ya kutumia adhabu mbadala.


IDARA YA UHAMIAJI
66. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji ina jukumu la kudhibiti uingiaji, utokaji na ukaaji wa wageni, na pia kuwawezesha raia wa Tanzania kupata hati za kusafiria. Aidha, Idara hii ndio inayoratibu mchakato wa maombi ya uraia wa Tanzania kwa wageni.

Hali  ya Ulinzi na Usalama Mipakani
67. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013 Idara iliendelea kutoa huduma katika mipaka kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini. Katika kipindi hicho, jumla ya wageni 801,676 waliingia na wengine 729,078 walitoka. Kiujumla hali ya mipaka ni shwari na idadi ya Wasomali na Waethiopia  wanaosafirishwa kwenda Kusini mwa Afrika kwa makundi imepungua kufikia 627 mwaka 2012  ikilinganishwa na  1,424 katika kipindi kama hiki  mwaka 2011. Aidha, huduma zilizotolewa na Idara ya Uhamiaji ni kama inavyoonyesha katika Jedwali Na. 4.

Tatizo la Wahamiaji Haramu
68. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji imeendelea kupambana na tatizo la wahamiaji haramu nchini. Tatizo hili linatokana na sababu za kihistoria kama kuwepo kwa masalia ya wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika, wakimbizi hususan wale wa muda mrefu waliotoroka toka makambi ya wakimbizi pamoja na kundi la wahamiaji haramu hususan kutoka nchi za Pembe ya Afrika kama Somalia, Ethiopia na Eritrea, ambalo lilianza kujitokeza mwaka 2007.

69. Mheshimiwa Spika, kundi hili la raia toka Pembe ya Afrika linakuwa kubwa kutokana na mtandao wa usafirishaji unaoendesha biashara haramu ya binadamu. Mtandao huo huanzia nchi wanazotoka hadi kule wanakoelekea Kusini mwa Afrika kupitia hapa nchini na kuendesha biashara hii kwa kupata kipato. Kundi hili linawajumuisha wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu (victims of human trafficking) na raia wa kigeni wanaohiari wenyewe kusafirishwa na mawakala haramu kuelekea nchi nyingine bila kufuata taratibu zilizowekwa (smuggled persons). Makundi yote haya kwa ujumla yanatengeneza kundi moja la wahamiaji haramu ambalo kwa sasa ni tatizo la kitaifa.

70. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013 Idara ya Uhamiaji iliendelea kufanya doria na misako yenye lengo la kudhibiti wahamiaji haramu nchini ambapo jumla wahamiaji haramu 2,319 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikilinganishwa na wahamiaji haramu 5,603 waliokamatwa katika kipindi kama hiki mwaka jana.

71. Mheshimiwa Spika, kuhusu wahamiaji waliotokana na masalia ya wapigania uhuru pamoja na wakimbizi waliotoroka makambini, Serikali imeamua kwa kuushirikisha uongozi wa Mikoa husika kufanya operesheni ya kuwabaini na kuwaondosha wahamiaji haramu hao. Mikoa ambayo itahusika na zoezi hilo ni  Kagera, Kigoma, Rukwa na Mara kwa upande wa Kaskazini na Magharibi mwa nchi yetu. Operesheni hii pia itafanyika katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa upande wa Kusini.

72. Mheshimiwa Spika, katika kupambana na tatizo linalokua la usafirishaji wa binadamu, Serikali imebainisha biashara hii kuwa ni moja ya uhalifu mkubwa wa kimataifa (Serious Crime). Serikali imeanzisha Kikosi Kazi kinachopambana na wasafirishaji wa biashara hii haramu. Hadi sasa Serikali imekamata na kutaifisha vyombo vya usafiri vinavyotumiwa na wasafishaji hao. Kwa kuwa tatizo hili linazigusa nchi mbalimbali katika ukanda wanakotoka, wanakopitia na kule wakoishia wahamiaji haramu, Serikali imefanya juhudi ya kuwa na vikao vya pamoja na nchi hizo ili kutengeneza mikakati itakayowezesha kupata suluhisho la pamoja katika kukabiliana na tatizo la wahamiaji haramu.

73. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji pia imeendelea kukabiliana na tatizo hili kwa kufanya yafuatayo:- Kuendelea kushirikiana na nchi jirani kwa kufanya mikutano ya ujirani mwema ya mara kwa mara pamoja na kuingia makubaliano ya kufanya misako na kupeana taarifa ya biashara haramu ya binadamu na wahusika kuchukuliwa hatua, kuendelea na zoezi la kuwaorodhesha wahamiaji walowezi ili kuwatambua na kuwa na kumbukumbu sahihi. Kushirikisha wadau wengine wa masuala ya Uhamiaji katika zoezi la kuwaondosha nchini wahamiaji haramu waliokamatwa, kuendeleza mfumo wa Maafisa Uhamiaji Kata kwa lengo la kushirikiana kwa karibu zaidi na jamii katika kutekeleza sheria ya Serikali za Mitaa ya kumtaka kila mwenyeji kutoa taarifa ya mgeni yeyote anayeingia au kuishi mahali popote ugenini, na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya kuwahifadhi na kuwapa kazi wahamiaji haramu bila kuwa na vibali halali.

Vibali Mbalimbali Vilivyotolewa kwa Wageni
74. Mheshimiwa Spika, Idara imetoa vibali kwa wageni wawekezaji, wageni waliopata ajira katika makampuni na wageni wengine walioingia nchini kwa malengo mbalimbali. Jumla ya wageni 12,878 walipewa hati za ukaazi kwa mchanganuo ufuatao:- daraja “A” 1,191, daraja “B” 7,037, daraja “C” 2,571, hati za ufuasi 297  na hati za msamaha 1,782.  Hati za msamaha ni vibali vya kuishi vinavyotolewa kwa wageni bila malipo yoyote. Wageni hao ni wale wanaofanyaka kazi katika Taasisi za Kimataifa zilizoko nchini (International Organizations), Wawakilishi wa nchi pamoja na wafanyakazi katika Ofisi za Balozi mbalimbali hapa nchini pamoja na wategemezi wao, wanafunzi toka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi nyingine, pamoja na wageni toka nchi Washirika wa Maendeleo wanaofanya kazi katika Mashirika ya Umma, Asasi za Kiserikali au katika sekta mbalimbali Serikalini.

Hati za Kusafiria  
75. Mheshimiwa Spika, Idara imetoa jumla ya hati za kusafiria 31,347 kwa Watanzania waliotaka kusafiri nje ya nchi kwa madhumuni mbalimbali. Kati ya hati hizo 30,202 ni za kawaida, 818 za Afrika Mashariki, 212 za kibalozi na 115 za kiutumishi. Aidha, kukua kwa hali ya utandawazi kumesababisha kubadilika kwa teknolojia ya udhibiti wa pasipoti na hati nyingine za safari. Kutokana na mabadiliko hayo, Idara ya Uhamiaji imeanza mchakato wa kupata mitambo mipya ya kuchapisha hati za safari itakayokuwa na uwezo wa kutoa hati zenye “ Biometric Features” ili kuepuka tatizo la pasipoti za Tanzania kughushiwa kirahisi.

Wageni Waliopatiwa Uraia wa Tanzania
76. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013 wageni 64 walipatiwa uraia. Wageni waliopata uraia ni wa kutoka India (27), Kenya (7), Uingereza (2), Pakistani (5), Somalia (1), Japan (1), Lebanon (6), Malawi (1), Burundi (6), Rwanda (1), Uganda (4), DRC (1), China (1) na Umoja wa Falme za Kiarabu (1). Hivi sasa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaendelea kuandaa Sera ya Uhamiaji na Uraia ili kushughulikia masuala ya uhamiaji na uraia nchini kwa ufanisi zaidi.

Watanzania Waliopatiwa Uraia wa Mataifa Mengine
77. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Watanzania 37 walipata uraia wa mataifa mengine kama ifuatavyo:-  Uingereza (1), Ujerumani (9), Norway (14), Uganda (2), Uholanzi (1), Denmark (3), Namibia (5) na Zambia (2) hivyo kupoteza haki ya kuwa raia wa Tanzania kwa  mujibu wa Sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995.

Wasomali Waliovuliwa Uraia
78. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiwapa raia wa kigeni uraia wa Tanzania wageni wakaazi walioomba na kukubaliwa baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria ya uraia. Hata hivyo kutokana na baadhi yao kutokuwa waaminifu, kama Waziri mwenye dhamana kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu Na. 15(1) cha Sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995, nilifuta uraia wa Tanzania kwa watu 102 raia wa Somalia (wakimbizi) waliokuwa wamepewa uraia wa Tanzania kwa tajnisi baada ya kuthibitika kwamba waliwasilisha taarifa na vielelezo visivyokuwa sahihi wakati wanaomba uraia. Hivyo kuanzia tarehe 6 Julai, 2012 wahusika wote walipoteza uraia wa Tanzania na wanatakiwa kuishi nchini kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Na. 7 ya mwaka 1995 na Sheria ya Wakimbizi Na. 8 ya mwaka 1998.

Ajira na Mafunzo
79. Mheshimiwa Spika, watumishi wapya 52 wameajiriwa na wengine 385 walioko kazini wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu. Kati yao tisa wamepata mafunzo ya muda mfupi nje ya nchi, mmoja mafunzo ya muda mrefu nje ya nchi, 324 wamepata mafunzo ya muda mfupi ndani ya nchi na 51 walipatiwa mafunzo ya muda mrefu ndani ya nchi. Katika mwaka 2013/2014, Idara inatarajia kutoa mafunzo kwa watumishi 650 waliopo kazini.

Vyombo vya Usafiri
80. Mheshimiwa Spika, Idara imenunua jumla ya magari 34 ambapo magari 10 ni aina ya Toyota Landcruiser Hardtop na 24 Toyota Hilux Pickup. Aidha, imenunua mabasi madogo matatu (3) na pikipiki 100. Katika mwaka 2013/2014, Idara ya Uhamiaji inatarajia  kununua magari 12, pikipiki 56, boti za doria tano na lori moja. Vyombo hivi vya usafiri vitasaidia kuimarisha shughuli za misako na doria dhidi ya wahamiaji haramu katika sehemu mbalimbali nchini zikiwemo zile za mipakani.

Majengo ya Ofisi
81. Mheshimiwa Spika, Idara imekamilisha ujenzi wa ofisi za Uhamiaji katika Mikoa ya Shinyanga na Morogoro. Aidha, ujenzi wa ofisi za Uhamiaji katika Mikoa ya Ruvuma na Manyara unaendelea na mchakato wa kuwapata Wakandarasi wa ujenzi wa ofisi za Uhamiaji katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Singida umeanza. Katika mwaka 2013/2014, Idara inatarajia kuanza ujenzi wa ofisi mpya katika Mikoa ya Mtwara na Geita, ofisi ya Wilaya ya Ifakara Mkoani Morogoro na kituo cha Kirongwe Mkoani Mara. Idara pia itaendelea na ukarabati wa ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mbeya.

Makazi ya Askari
82. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, Idara imenunua maghorofa mawili Mkoani Tabora kwa ajili ya makazi ya askari yenye uwezo wa kuishi familia 12 pamoja na nyumba tano za Maafisa Uhamiaji zenye uwezo wa kuishi familia tano. Aidha, ujenzi wa nyumba tano za viongozi wa Idara ya Uhamiaji Makao Makuu unaendelea Mtoni Kijichi – Dar es Salam. Katika mwaka 2013/2014, Idara itaanza ujenzi wa nyumba za askari Kisongo Jijini Arusha na  Chakechake – Pemba.

83. Mheshimiwa Spika, Idara imekamilisha ukarabati wa nyumba  za askari Igoma - Mwanza na pia ukarabati unaendelea katika vituo vya Horohoro – Tanga, Borogonja – Mara, Tunduma – Mbeya, Tanga Mjini, Dodoma Mjini na mabweni ya Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda Moshi. Katika mwaka 2013/2014, Idara inatarajia kufanya ukarabati wa nyumba za askari zilizoko Mtoni Kijichi – Dar es Salaam.



Mapambano Dhidi ya VVU/UKIMWI
84. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji imeendelea kutoa elimu pamoja na kuwahudumia watumishi wanaoishi na VVU/UKIMWI kwa lengo la kupunguza maambukizo mapya ya UKIMWI mahala pa kazi na kwa familia za askari. Aidha, Idara imesambaza vipeperushi katika vituo vya kuingilia nchini vinavyolenga kutoa elimu juu ya maambukizo ya VVU na UKIMWI pamoja na athari zake.

JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI
85. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kuokoa maisha na mali kwenye majanga ya moto na majanga mengineyo yanayolikumba Taifa letu. Pamoja na majukumu haya ya msingi, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013, jumla ya maeneo 5,149 yalifanyiwa ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kama ilivyofafanuliwa katika Jedwali Na. 5. Pia jumla ya magari makubwa na madogo 6,455,447 yalikaguliwa. Huduma hii inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Zimamoto na Uokoaji  Na. 14 ya mwaka 2007.  
 
86. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limefanikiwa kuwapatia mafunzo askari 72, ndani ya nchi askari 60 na nje ya nchi 12. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji litaendelea na zoezi la ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto, kuendelea kutoa elimu juu ya kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo mbalimbali, na litaendelea kuimarisha huduma zake kwa kujenga vituo vya Zimamoto na Uokoaji kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.

IDARA YA WAKIMBIZI
87. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na jitihada mbalimbali zenye lengo la kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la kuwepo maelfu ya wakimbizi hapa nchini, ambao baadhi yao walikuwa wanasita kurejea kwenye nchi zao za asili pamoja na kuwa hali ya usalama katika nchi hizo ilikuwa imeimarika vya kutosha. Katika kukabiliana na tatizo hilo niliwavua hadhi ya ukimbizi, kwa mujibu wa sheria, wakimbizi wa Burundi wapatao 38,000 na kuwataka kurejea kwenye nchi yao ya asili na wale ambao wangekataa kutekeleza agizo hilo wangechukuliwa hatua. Uamuzi huo uliwezesha raia wa Burundi wapatao 35,000 waliokuwa wanaishi kwenye kambi ya Mtabila Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma kurejea nchini Burundi kwa kusaidiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNHCR na International Organization for Migration (IOM) na kuwezesha kambi hiyo kufungwa rasmi tarehe 31/12/2012. Hivi sasa UNHCR wanafanya ukarabati wa miundombinu ya kambi hiyo ili eneo la kambi likabidhiwe rasmi kwa uongozi wa Mkoa wa Kigoma.

88. Mheshimiwa Spika, baada ya kufunga kambi ya Mtabila, kwa sasa Tanzania inayo kambi moja tu ya Nyarugusu Wilayani Kasulu ambayo inahifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Pamoja na kwamba hali ya usalama katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini nchini DRC ambako wakimbizi hao wanatoka bado sio ya kuridhisha, tunaamini kuwa yapo baadhi ya maeneo katika majimbo hayo ambayo hali ya usalama inaridhisha ambapo wakimbizi wa DRC wanaweza kuanza kurejea huko. Kwa kuzingatia hali hiyo, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Tanzania inakusudia kuitisha Kikao cha Pande Tatu kitakachojumuisha Serikali ya Tanzania, Serikali ya DRC na UNHCR ili kukubaliana namna ya kuwapa fursa wakimbizi wanaotoka maeneo ya Kivu Kaskazini na Kusini kurejea nchini kwao bila ya kikwazo chochote. Aidha, katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2012 wakimbizi 96 wa DRC walirejea kwao. Lengo pia ni kuwezesha wakimbizi wote wa kambi ya Nyarugusu kurejea kwao na kambi hiyo kufungwa.

89. Mheshimiwa Spika, vile vile Serikali imeendelea na mchakato wa kutoa uraia kwa wakimbizi wa Somalia wa makazi ya Chogo yaliyopo Wilayani Handeni ambao wametimiza sifa na masharti yaliyowekwa. Lengo ni kufunga makazi hayo. Pamoja na jitihada hizo zilizofanya idadi ya wakimbizi kupungua, Tanzania imeendelea kuwahifadhi wakimbizi ambapo takwimu zinaonyesha kuwa hadi tarehe 31 Desemba, 2012  ilikuwa inahifadhi jumla ya wakimbizi 100,489  wakiwemo Warundi 35,343, Wakongo 63,330, Wasomali 1,574 na  242 wakimbizi wa mataifa mbalimbali kama ilivyofafanuliwa katika  Jedwali Na. 6.   

90. Mheshimiwa Spika, lipo kundi maalum la wakimbizi wa Burundi wapatao 162,000 walioingia nchini mwaka 1972 ambao wanaishi kwenye makazi ya Katumba na Mishamo Mkoani Katavi na Ulyankulu Mkoani Tabora ambapo Serikali ipo kwenye mchakato maalum wa kupata ufumbuzi wa kudumu wa hadhi yao.

MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA
91. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeajiri watumishi 89, imenunua vitendea kazi muhimu vya ofisi vikiwemo vifaa vya elektroniki na kuendelea na ukarabati wa ofisi katika Mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar. Aidha, NIDA imempata Mkandarasi wa kujenga ofisi za utambuzi na usajili za Wilaya zote nchini. Katika mwaka 2013/2014, NIDA itaendelea na zoezi la utambuzi na usajili wa watu, kuajiri watumishi 542, kununua magari 20, kuendelea kuweka mfumo wa mawasiliano kati ya ofisi za Wilaya na Makao Makuu ya NIDA, kuendelea na uboreshaji wa upanuzi wa Makao Makuu ya NIDA na kukamilisha mchakato wa kutunga sheria ya usajili na utambuzi wa watu.

V. TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA AHADI ZA SERIKALI BUNGENI 2012/2013
92. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Serikali Bungeni katika mwaka 2012/2013, umezingatiwa katika hotuba hii katika eneo la III -Taarifa ya utekelezaji wa malengo ya Ilani ya Uchaguzi na la IV - Mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2012/2013. Ahadi hizo zipo katika  maeneo ya vitendea kazi, ajira na mafunzo, misako na doria, ujenzi na ukarabati wa ofisi, vituo, nyumba na magereza, zoezi la utambuzi na usajili wa  watu, kuwarejesha wakimbizi kwao na kuweka alama maalum katika silaha zinazomilikiwa na taasisi za Serikali, makampuni na watu binafsi. Kwa ujumla wake, taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali zilizotolewa Bungeni katika mwaka 2012/2013, ni kama inavyoonyesha katika Kiambatisho Na. 1 cha hotuba hii.



VI. SHUKRANI
93. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Anna Margareth Abdallah Mbunge Viti Maalum kwa kuyapitia na kuyachambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Maelekezo na ushauri wa Kamati hiyo utaisaidia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika  kutekeleza majukumu yake.

94. Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee nazitoa kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Pereira Ame Silima, Mbunge wa Chumbuni, Katibu Mkuu Ndugu Mbarak Abdulwakil, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Mwamini Malemi, Inspekta Jenerali wa Polisi Ndugu Saidi Mwema, Kamishna Jenerali wa Magereza Ndugu John Minja, Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Ndugu Pius Nyambacha, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Ndugu Magnus Ulungi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Ndugu Dickson Maimu, Mkurugenzi wa Wakimbizi Ndugu Judith Mtawali, Mkurugenzi wa Huduma  kwa Jamii Ndugu Fidelis Mboya, Wakuu wote wa Idara na Vitengo, Makamanda, askari pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambao wamefanikisha maandalizi ya hotuba hii na pia kwa kusaidia kufanikisha majukumu ya Wizara.

95. Mheshimiwa Spika, nachukua pia fursa hii kuwashukuru nchi wahisani ikiwemo China, Marekani, Ujerumani, Misri, Botswana, Nigeria na taasisi za INTERPOL, IOM, EU, UNHCR, DFID, UNICEF, WFP, Hanns Seidel Foundation na Pharm Access pamoja na wadau wengine wote kwa misaada yao ambayo imeongeza uwezo wa kiutendaji katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

96. Mheshimiwa Spika, mwisho ingawa sio mwisho kwa umuhimu, ninawashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal kwa maelekezo yao mbalimbali na  Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu kwa kuhimiza utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

VII. MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2013/2014
97. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naliomba Bunge lako Tukufu lipitishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2013/2014 ya shilingi 741,131,711,000 kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Kati ya makadirio hayo, shilingi 578,284,694,000 ni za matumizi ya kawaida ambapo shilingi 271,572,291,000 ni Matumizi Mengineyo na mishahara shilingi 306,712,403,000. Makadirio ya shilingi 162,847,017,000 ni kwa ajili ya mipango ya maendeleo. Mchanganuo ni kama ifuatavyo:-

Fungu 14: Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Matumizi Mengineyo shilingi   18,610,590,000
Mishahara shilingi                   1,812,194,000
Maendeleo shilingi                                 0.00
Jumla shilingi                  20,422,784,000

Fungu 28: Jeshi la Polisi
Matumizi Mengineyo shilingi   149,600,221,000
Mishahara shilingi                 205,663,241,000
Maendeleo shilingi                    8,980,451,000
Jumla shilingi                            364,243,913,000

Fungu 29: Jeshi la Magereza
Matumizi Mengineyo shilingi    53,510,022,000
Mishahara shilingi                  72,758,378,000
Maendeleo shilingi                   2,666,566,000
Jumla shilingi                 128,934,966,000

Fungu 51: Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Matumizi Mengineyo shilingi     2,107,467,000
Mishahara shilingi                   2,711,513,000
Maendeleo shilingi                                 0.00
Jumla shilingi                    4,818,980,000

Fungu 93: Idara ya Uhamiaji
Matumizi Mengineyo shilingi   47,743,991,000
Mishahara shilingi                  23,767,077,000
Maendeleo shilingi                151,200,000,000
Jumla shilingi                 222,711,068,000

98. Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.

99. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

3 comments:

Anonymous said...

This is my first timе go to ѕеe at here аnԁ і
аm actually haρρy to read еvеrthing
at sіngle place.

Μу blog poѕt Sixpack

Anonymous said...

I’m not thаt muсh of a іnternet readеr to be hοnest but your
sіtes геally nіce, kееp it up!
I'll go ahead and bookmark your website to come back in the future. All the best

Visit my web blog - home acne products

Anonymous said...

I am no longer positive the place you are getting your info, but good topic.
I needs to spend some time learning more or working out more.
Thank you for magnificent information I used to be in search of this info for my mission.