HOTUBA
YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHESHIMIWA DKT. EMMANUEL JOHN NCHIMBI
(MB.), AKIWASILISHA BUNGENI
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
KWA
MWAKA 2013/2014
I.
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, baada ya kuzingatia taarifa iliyowasilishwa mbele
ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na
Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka
wa fedha wa 2013/2014.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kutumia fursa hii kutoa masikitiko yangu kwa familia
na wananchi kwa ujumla kutokana na vifo, ulemavu, upotevu na uharibifu wa mali
na miundombinu vilivyosababishwa na ajali za barabarani, majini, kuporomoka kwa
majengo na vifusi, vurugu na fujo katika mwaka mzima wa 2012. Aidha, nawapa
pole ndugu na jamaa wa marehemu waliopoteza maisha yao katika matukio hayo. Namwomba
Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Anna Margareth Abdallah,
Mbunge Viti Maalum kwa kuyachambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi. Naishukuru pia Kamati hiyo kwa maelekezo na ushauri wao
wenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
4. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii pia kumpongeza
Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake aliyoitoa mapema katika mkutano huu wa Bunge
ambayo imetoa mwelekeo wa kazi za Serikali kwa ujumla katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.
5. Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, kuhifadhi na
kuwarekebisha wafungwa, kutekeleza Programu ya Huduma kwa Jamii, kudhibiti uingiaji na utokaji
nchini wa raia na wageni, kutoa huduma za zimamoto na uokoaji, kuwahudumia
wakimbizi waliopo nchini, na kutoa vitambulisho vya Taifa. Majukumu haya yanatekelezwa kupitia
Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Huduma kwa Jamii, Idara ya Uhamiaji,
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Wakimbizi na Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa.
II. HALI YA USALAMA NCHINI
Hali ya Uhalifu
6.
Mheshimiwa Spika, kama
inavyofahamika kwamba wajibu wa kwanza wa Serikali ni kulinda usalama wa raia
na mali zao. Umuhimu wa amani na utulivu kama msingi mkuu ambao umejengwa
nchini na waasisi wa Taifa letu na mchango wake katika ustawi wa nchi yetu
kiuchumi, kijamii na kisiasa umeendelea kuzingatiwa. Kwa upande wake, Jeshi la
Polisi limeendelea kutekeleza kikamilifu jukumu lake la kulinda na kudumisha
amani na utulivu nchini kwa kubaini, kuzuia na kutanzua vitendo vya uhalifu, migogoro,
vurugu, fujo na ukiukwaji wa Sheria za Usalama Barabarani.
7. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2012 makosa ya jinai
makubwa na madogo 566,702 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi ikilinganishwa
na makosa 564,716 yaliyoripotiwa katika
kipindi kama hiki mwaka 2011. Idadi ya makosa imeongezeka kwa asilimia 0.3. Tazama Jedwali Na. 1. Ongezeko hilo
limechangiwa na kuongezeka kwa makosa madogo kutokana na ushirikishwaji wa wananchi
katika vita dhidi ya uhalifu na kuongezeka kwa wigo wa doria na misako ya
Polisi Mijini na Vijijini.
8. Mheshimiwa
Spika, makosa makubwa ya jinai yamegawanyika katika makundi matatu ambayo
ni makosa dhidi ya binadamu, makosa ya kuwania mali na makosa dhidi ya maadili
ya jamii. Idadi ya makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo vya
polisi imepungua kutoka 76,052 mwaka 2011 hadi 72,765 mwaka 2012 ikiwa ni sawa
na upungufu wa asilimia 4.3. Mafanikio ya kupungua idadi ya makosa makubwa ya jinai yanatokana
na utekelezaji wa mikakati ya Jeshi la Polisi ya kuimarisha doria, misako na operesheni maalum, ushirikishwaji wa
wananchi katika mapambano dhidi ya uhalifu, ushirikiano wa Jeshi la Polisi na
vyombo vingine vya dola ndani ya nchi na ushirikiano wa Jeshi la Polisi na majeshi
mengine ya Polisi kikanda na kimataifa.
Usalama
Barabarani
9. Mheshimiwa Spika, pamoja na mikakati ya Jeshi la Polisi ya kuzuia
na kudhibiti ajali za barabarani, ajali hizi zimeendelea kusababisha vifo,
majeraha na ulemavu wa kudumu kwa
wananchi pamoja na upotevu na uharibifu wa mali za wananchi, Taasisi na
Serikali kwa ujumla. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2012 makosa makubwa ya usalama barabarani 23,604 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi ambapo
watu 4,062 walipoteza maisha na wengine 20,037 kujeruhiwa ikilinganishwa na
makosa makubwa 24,078 yaliyoripotiwa katika
kipindi cha Januari hadi Desemba, 2011
ambapo watu 4,013 walifariki na wengine
20,917 kujeruhiwa. Idadi ya makosa
ilipungua kwa asilimia 1.9. Tazama Jedwali Na. 1.
10. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wengine
kama SUMATRA, TBS, TANROADS na Shule za Udereva zilizosajiliwa limeendelea
kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani zikiwemo kutoa elimu ya
kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani kwa watumiaji wa barabara, kushirikisha
wadau wa usalama barabarani katika kuhuisha mikakati ya kupunguza ajali za
barabarani, kuendeleza doria za masafa mafupi na marefu katika kusimamia Sheria
za Usalama Barabarani, kufanya ukaguzi wa magari, kutumia kamera za kutambua
madereva wanaoendesha kwa mwendo kasi bila kuzingatia alama za usalama barabarani,
kuendelea kusimamia zoezi la utoaji wa leseni mpya, kuwahamasisha wasafiri
kutoa mapema taarifa za madereva wanaokiuka Sheria za Usalama Barabarani na kuwahamasisha
wamiliki wa Mabasi kubandika kwenye Mabasi yao namba za simu za viongozi wa
Polisi Usalama Barabarani. Kwa ujumla Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza
maoni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yaliyoainishwa katika “Performance Audit Report on the Management
of Traffic Inspections and Speed Limits in Tanzania” ya mwaka 2012. Taarifa hii inalitaka Jeshi la Polisi
lijikite zaidi katika kuzuia na kudhibiti vyanzo vya ajali za barabarani vya
mwendokasi, ulevi, uzembe wa madereva na kuzidisha abiria na mizigo.
Vitendo
vya Uvunjifu wa Amani, Vurugu na Fujo
11. Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 15/02/2013, Mawaziri tisa kutoka
Wizara za Katiba na Sheria, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto, Kilimo, Chakula na Ushirika, Nishati na Madini, Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Mambo ya Ndani ya Nchi pia Ofisi ya Rais, Utawala Bora na
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa walihudhuria warsha
iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi iliyofanyika hapa Dodoma kuhusu mipango ya
Serikali katika kudumisha usalama nchini. Warsha hiyo ilitanguliwa na mkutano
mkuu wa mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi uliofanyika kuanzia
tarehe 12 – 14/02/2013 uliokuwa na kauli mbiu isemayo “Tujenge Uwezo wa Jamii na Polisi Kukabiliana na Vurugu kwa Kuimarisha
Utii wa Sheria Bila Shuruti”.
12. Mheshimiwa Spika, kufanyika kwa warsha hiyo ya Mawaziri kulitokana
na kuendelea kuwepo kwa vitendo vya vurugu, fujo na uvunjifu wa amani
vinavyotokana na migogoro ya kijamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Vurugu
za kisiasa zilizotokea Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Singida na
Iringa, migogoro ya ardhi iliyotokea Babati, Madale - Dar es Salaam,
Sumbawanga, Ngorongoro, Rufiji na Kilosa, migogoro ya kidini iliyotokea
Zanzibar, Mbeya, Temeke, Geita na mgogoro kuhusu uwekezaji katika sekta ya gesi
Mkoani Mtwara, ni kati ya matukio mengi yanayoendelea kutokea nchini. Katika
matukio hayo ya vurugu, fujo na uvunjifu
wa amani watu kadhaa wamepoteza maisha
wakiwemo askari polisi, wananchi mbalimbali wamejeruhiwa na umefanyika
uharibifu wa miundombinu, mazingira na mali za Serikali na watu binafsi.
13. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumejitokeza vurugu za udini ambapo
zipo kesi 16 zilizohusisha jumla ya watuhumiwa 195. Kesi 13 tayari zimefikishwa
Mahakamani na kesi tatu upelelezi bado unaendelea. Athari za vurugu za udini ni
pamoja na uvunjifu wa amani. Serikali imejipanga vyema kuona kuwa hali hiyo
haiendelei na haijirudii tena kwa ustawi wa Taifa letu.
14. Mheshimiwa Spika, matukio haya inawezekana yameacha makovu ya chuki
za ki-itikadi na hisia za kulipiza kisasi miongoni mwa waathirika. Jeshi la
Polisi limejizatiti kukabiliana na vitendo hivi
vya fujo, vurugu na uvunjifu wa amani kwani vikiachwa viendelee uchumi
wa nchi utadorora kutokana na ushiriki hafifu wa wananchi kwenye shughuli za
maendeleo unaosababishwa na hofu inayojengeka katika jamii ya Watanzania na
wawekezaji wa ndani na nje kutokana na nchi kuelekea kupoteza sifa yake ya kuwa
ni Kisiwa cha Amani.
15. Mheshimiwa Spika, naungana na Watanzania wenzangu kulaani vitendo
vyote vya fujo na vurugu vilivyosababisha uvunjifu wa amani. Nawakemea vikali wale
wote walioshiriki, kuwezesha, kufadhili, kuhamasisha, kuchochea na kushawishi
jamii kushiriki katika vitendo vilivyosababisha vurugu hizo na hata umwagaji wa
damu. Natoa pole kwa wahanga wote wa vurugu hizo. Hatua za kisheria kwa
watuhumiwa zinaendelea kuchukuliwa.
16. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kuliomba Bunge lako Tukufu
liendelee kuunga mkono kwa vitendo utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya
Jeshi la Polisi. Programu hii pamoja na mambo mengine, imelenga kuligeuza Jeshi
la Polisi kuwa la kisasa, lenye watendaji wenye weledi na linaloshirikiana na
jamii katika kubaini, kuzuia, kudhibiti na kukabili vitendo vya uhalifu, fujo
na vurugu.
17. Mheshimiwa Spika, ninapenda kuwashukuru Mawaziri wenzangu
waliohudhuria warsha iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi hapa Mjini Dodoma mwezi
Februari 2013 kwa kutoa Tamko la Dodoma
lililokubali kusimamia na kutekeleza mipango ya muda mfupi, muda wa kati na
muda mrefu ya kuimarisha ulinzi na usalama nchini kwa:-
i)
Kuliweka suala la usalama kuwa ni moja
ya vipaumbele vya Taifa
ii)
Kutenga fedha za kutosha kuliwezesha Jeshi la Polisi kumudu kikamilifu wajibu
wake wa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao
iii)
Kutambua kwamba kila Wizara ni mdau katika suala la usalama na inayo wajibu wa
kuepusha migogoro inayozalisha vurugu
iv)
Kufanya tathmini ya maeneo ambayo ni vyanzo vya migogoro na kutafuta njia ya
kuzuia/kutanzua migogoro hiyo. Kuimarisha/kuhuisha mifumo ya usimamizi wa
sheria na uwajibikaji wa kila Idara ya Serikali
v)
Kujenga ubia wa kiutendaji baina ya Wizara wanazoziongoza na vyombo vya ulinzi
na usalama katika kubaini vyanzo vya migogoro na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia
na kutanzua migogoro hiyo
vi)
Kuliwezesha Jeshi la Polisi kwa rasilimali vifaa na miundombinu pindi Mikoa
mipya inapoanzishwa
vii)
Kurekebisha haraka na kwa vipaumbele upungufu wa kisera, kisheria na kikanuni
unaoweza kuchangia mianya ya kusababisha migogoro ya kijamii
III.
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MALENGO YA
ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010 KATIKA KIPINDI CHA 2012/2013
18. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina malengo 10
ya kutekeleza yanayotokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010. Taarifa
ya utekelezaji wa malengo hayo kwa mwaka 2012/2013, ni kama ifuatavyo:-
19. Mheshimiwa Spika, lengo la kwanza ni kuendeleza mapambano dhidi ya
biashara ya dawa za kulevya. Katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013 Jeshi
la Polisi liliwahamasisha na kushirikiana na wananchi katika Ulinzi
Shirikishi ili kudhibiti uhalifu ukiwemo uingizaji, usambazaji na matumizi ya
dawa za kulevya katika maeneo yao. Ushirikiano wa wananchi na vyombo vingine
vya dola uliliwezesha Jeshi la Polisi kuwakamata watuhumiwa 546 wakiwa na jumla
ya kilo 33.299 za dawa za kulevya za viwandani ambapo Cocaine ni kilo 14.209, Heroine kilo 13.073 na Mandrax
kilo 6.017. Aidha, watuhumiwa 6,730 walikamatwa na kilo 37,704.201 za dawa za kulevya za mashambani ambapo bhangi ni
kilo 26,938.445 na mirungi kilo 10,765.756. Jumla ya ekari 211 za mashamba ya
bhangi ziliteketezwa katika Kanda Maalum ya Kipolisi ya Tarime/Rorya na Mkoani
Tanga.
20. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi litaendelea
kushirikiana na wananchi kupata taarifa za waingizaji, wasafirishaji na
watumiaji wa dawa za kulevya. Pia
litaendelea kubaini mtandao wa wahalifu wa ndani na nje ya nchi unaojihusisha
na uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini kwa kushirikiana na
Shirika la Polisi la Kimataifa (INTERPOL) kupata taarifa za kiintelijensia
kuhusu wasafirishaji wa dawa za kulevya. Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Vyombo vya
Ulinzi na Usalama cha kupambana na biashara ya dawa za kulevya kitaendelea kuimarishwa
kwa kukiongezea rasilimali watu na vitendea kazi.
21. Mheshimiwa Spika, lengo la pili ni kupunguza msongamano wa wafungwa
na mahabusu katika Magereza. Tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu bado
ni kubwa licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kukabiliana nalo. Kulingana
na takwimu, msongamano Magerezani kwa kiwango kikubwa unasababishwa na uwepo wa
mahabusu wengi. Tarehe 1 Februari, 2013 idadi ya wafungwa na mahabusu waliokuwepo
Magerezani ilifikia 34,355. Kati ya hao wafungwa walikuwa 16,330 na mahabusu
18,025 kama ilivyofafanuliwa katika Jedwali
Na.2.
22. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari,
2013 jumla ya wafungwa 387 walikuwa wanatumikia kifungo cha nje kwa kutumia
kanuni za kifungo cha nje za mwaka 1968. Tazama
Jedwali Na. 3. Vile vile wafungwa 903 waliachiliwa na Mahakama ili kutumikia
kifungo cha nje chini ya Sheria ya Huduma kwa Jamii kwa kipindi cha Julai, 2012
hadi Februari, 2013. Aidha, wafungwa 3,814 walifaidika na msamaha wa Rais uliotolewa
tarehe 9 Desemba, 2012 wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 51 ya Uhuru wa
Tanzania Bara. Hatua zingine zinazochukuliwa ili kupunguza msongamano ni pamoja
na kuundwa kwa Jukwaa la Haki Jinai chini ya uenyekiti wa Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo
wajumbe wengine ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Mahakama. Jukumu la
msingi la jukwaa hilo ni kuimarisha utoaji wa haki nchini.
23. Mheshimiwa Spika, lengo la tatu ni kuimarisha
na kuboresha mfumo wa upelelezi wa makosa ya jinai ili kurahisisha uendelezaji
wa kesi mahakamani. Kwa
kutumia vyuo vya Taaluma ya Polisi vya Moshi na Kidatu, kati ya Julai 2012 hadi
Februari 2013, Jeshi la Polisi limetoa mafunzo ya Intelijensia na mbinu za
kisasa za upelelezi kwa wapelelezi 328. Wapelelezi 22 walipata mafunzo katika
nchi za Marekani, Misri, Nigeria na Botswana. Jeshi la Polisi pia limepata
vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kisayansi katika maabara
iliyopo Makao Makuu ya Polisi. Vifaa hivyo vitaimarisha ung’amuzi wa wahalifu,
ukaguzi na ukusanyaji wa vielelezo na ushahidi kwenye matukio makubwa ya
uhalifu. Aidha, mchakato wa kuikabidhi Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kazi za
kuendesha mashtaka Mahakamani umeendelea. Hadi sasa mchakato huo umekamilika
katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya katika Mikoa 22 ya Kipolisi
Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar.
24. Mheshimiwa Spika, lengo la nne ni kuanzisha mpango wa kuwapatia
askari nyumba bora za kuishi. Kutokana na mahitaji makubwa ya rasilimali fedha
kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari nchi nzima, Jeshi la Polisi
limeanza utekelezaji wa mpango wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi
(PPP) ili kupunguza ukubwa wa tatizo hili. Kwa kuanzia Jeshi la Polisi
limeingia ubia wa kujengewa nyumba 350 katika Mkoa wa Polisi Kinondoni kuanzia
mwaka wa fedha wa 2013/2014. Utaratibu uliofuatwa katika Mkoa wa Kinondoni
utatumika kupunguza tatizo la makazi ya askari katika Mikoa yote nchini.
Mkakati wa muda mrefu ni kujenga nyumba za gharama nafuu kwa kutumia Shirika la
Uzalishaji Mali (Corporation Sole) la Jeshi la Polisi ambalo uanzishwaji wake
utakamilika hivi karibuni. Kwa sasa
tumekamilisha ujenzi wa maghorofa 90 yaliyotoa nafasi ya makazi bora kwa askari
360 pamoja na familia zao. Jeshi la Polisi litaendelea kutumia fedha za bajeti
ya maendeleo kujenga nyumba za askari kadri uwezo utakavyoruhusu.
25. Mheshimiwa Spika, lengo la tano ni kujenga vituo vya Polisi katika
kila Tarafa nchini. Mikakati ya kupunguza tatizo la makazi itatumika pia
kupeleka huduma ya polisi karibu na wananchi kwa kujenga vituo vya polisi
katika kila Tarafa. Kutokana na mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kwa ajili
ya ujenzi wa vituo vya polisi, Jeshi la Polisi litatumia Shirika la Uzalishaji
Mali litakaloanzishwa na mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi
kujenga vituo vya Tarafa kwa awamu. Hivi sasa Jeshi la Polisi litaendeleza
utekelezaji wa Polisi Jamii kwa kuwatumia Wakaguzi 526 wa Tarafa na askari
Kata kutoa huduma za polisi kwa kutumia vituo vilivyopo karibu na Tarafa zisizo
na vituo vya polisi hasa maeneo ya vijijini.
26. Mheshimiwa Spika, lengo la sita ni kuwapatia wananchi mafunzo ya Ulinzi Shirikishi ili wawe tayari
kujilinda katika maeneo yao. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeanzisha
kampeni mahsusi ya kuhamasisha Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali
kuzingatia ukweli kwamba zinao wajibu wa kujenga miundombinu ya amani katika
ngazi za Mikoa, Wilaya, Tarafa na Kata kwa kutumia sheria na taratibu zilizopo.
Jeshi la Polisi limeendelea kuwatumia Wakaguzi wa Tarafa/Jimbo na Askari
Kata/Shehia kuwaelimisha wananchi kwamba
kila mmoja anawajibika kwa ulinzi wake binafsi, familia yake, jirani yake na
jamii kwa ujumla tofauti na fikra potofu za baadhi ya watu kwamba usalama wa
raia na mali zao ni jukumu la Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali pekee.
27. Mheshimiwa Spika, lengo la saba ni kuimarisha mafunzo ya askari wa
vyombo vya ulinzi na usalama. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba
2012 askari 12,276 kutoka Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na
Uhamiaji wamepatiwa mafunzo katika fani mbalimbali ambapo Polisi ni 9,407,
Magereza 2,413, Zimamoto na Uokoaji 72 na Uhamiaji 384. Mwaka 2013/2014,
mafunzo yatatolewa kwa jumla ya askari 32,957 ambapo Polisi ni 30,000, Magereza
2,307 na Uhamiaji 650.
28. Mheshimiwa Spika, lengo la nane ni kuimarisha uzalishaji wa mbegu
bora za kilimo katika maeneo ya Magereza. Katika mwaka 2012/2013, Jeshi la
Magereza kwa kushirikiana na Wakala wa
Mbegu za Kilimo nchini katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Manyara, Lindi, Iringa,
Mbeya, Kilimanjaro na Morogoro na vile vile kwa kushirikiana na Kampuni ya Highland Seed Growers Ltd na TANSEED katika Mikoa ya Rukwa, Ruvuma
na Kigoma kwa ujumla limelima hekta 990.2 za mashamba ya mbegu bora za kilimo na
matarajio ni kuvuna tani 2,000 za mbegu
bora. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la
Magereza linatarajia kuhudumia hekta 3,175 za mazao mbalimbali kwa mategemeo ya
kupata mavuno ya tani 4,500 iwapo hali ya hewa itakuwa nzuri.
29. Mheshimiwa Spika, lengo la tisa ni kutoa vitambulisho vya Taifa.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ina jukumu la kusimamia mfumo wa
utambuzi na usajili wa watu pamoja na utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa
Watanzania, wageni wakaazi na wakimbizi wanaostahili. Huu ni mfumo mpya ambao
utakuwa na manufaa kwa Taifa katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiusalama.
30. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua mfumo wa utambuzi na usajili wa
watu hapo tarehe 7 Februari 2013 Jijini Dar es Salaam. Tukio la uzinduzi
liliambatana na Mheshimiwa Rais kukabidhiwa kitambulisho cha kwanza cha Taifa katika
historia ya Tanzania. Hili ni jambo jema linalohitaji Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa nchini kupongezwa. Aidha, vitambulisho vilitolewa pia kwa vikundi
mbalimbali vinavyowakilisha jamii na viongozi Wakuu wa Kitaifa wakiwemo Marais
wastaafu, Mawaziri Wakuu wastaafu, Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Waheshimiwa
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
31. Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni kuendelea kutoa vitambulisho
vya Taifa kwa wafanyakazi wa Wizara,
Idara na Wakala wa Serikali wa Mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar pamoja na
vyombo vya ulinzi na usalama wapatao 290,000, wakaazi 220,000 wa Wilaya ya
Kilombero Mkoani Morogoro, wakaazi 2,159,182 wa Mkoa wa Dar es Salaam na
wakaazi 165,825 wa Zanzibar. Napenda kuwataarifu Watanzania wote kupitia Bunge
lako Tukufu kwamba zoezi la utoaji wa vitambulisho vya Taifa ni endelevu ambalo
litafanyika katika Mikoa na Wilaya zote za Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa vile zoezi
hili haliendeshwi kwa kuzingatia misingi ya itikadi za kisiasa, kidini au
kikabila, natoa rai kwamba sote tuweke mbele suala la uzalendo na kutoa
ushirikiano wa dhati kwa NIDA katika kufanikisha utoaji wa vitambulisho hivi
kwa maslahi ya Taifa letu.
32. Mheshimiwa Spika, lengo la kumi ni kuimarisha Vikosi vya Zimamoto
na Uokoaji vyenye wataalam na zana za kisasa ili kukabiliana na majanga ya moto. Katika kipindi cha mwezi Julai hadi
Desemba 2012 askari wa Zimamoto na Uokoaji 72 wamepatiwa mafunzo. Kati yao 12
wamepatiwa mafunzo nje ya nchi ya uokozi kwenye maji (7) na majengo marefu (5)
na askari 60 wamepatiwa mafunzo ndani ya nchi. Jeshi pia limepata msaada kutoka
Ujerumani wa kompyuta 100 na vifaa vya kinga ya moto. Ili kusogeza huduma za zimamoto
na uokoaji karibu na wananchi, ujenzi wa kituo cha Zimamoto na Uokoaji eneo la
Mwenge – Dar es Salaam unaendelea.
IV.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/2013 NA MALENGO YA MWAKA 2013/2014
33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi ilipangiwa kukusanya mapato ya shilingi 96,449,327,801. Hadi tarehe 28 Februari,
2013, Wizara ilikuwa imekusanya shilingi 76,990,955,792 sawa na asilimia 79.8 ya
lengo la mwaka. Katika mwaka 2013/2014, Wizara ina lengo la kukusanya mapato ya
shilingi 145,024,760,000. Nguvu
zaidi zitaelekezwa katika kuziba mianya ya uvujaji wa mapato hususan katika kuimarisha
na kuboresha matumizi ya benki kwa ajili ya kufanya malipo ya huduma zitolewazo
na taasisi za Wizara.
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara
iliidhinishiwa kutumia shilingi 555,540,268,000 kwa ajili ya bajeti ya matumizi
ya kawaida na miradi ya maendeleo. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Februari,
2013 jumla ya shilingi 337,534,661,068 zilikuwa zimetumika sawa na asilimia 60.8
ya bajeti ya mwaka mzima kama ifuatavyo:- Shilingi 178,838,875,099 zimetumika
kulipia mishahara, Matumizi Mengineyo shilingi 148,977,021,516 na fedha za maendeleo
ni shilingi 9,718,764,453. Katika mwaka 2013/2014, Wizara imetengewa shilingi 741,131,711,000
kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.
JESHI LA POLISI
35. Mheshimiwa Spika, kama
nilivyotangulia kusema hapo awali kwamba amani, utulivu na usalama wa nchi yetu
ni mihimili mikuu ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wananchi
wetu. Kuongezeka kwa tishio la uhalifu, fujo, migogoro na kuzorota kwa usalama
wa raia huathiri mfumo mzima wa ustawi wa nchi
katika maeneo hayo matatu na kwa ujumla hudhoofisha nguvu za wananchi
katika kujiletea maendeleo. Jeshi la Polisi Tanzania ndilo lenye jukumu la kuhakikisha amani, utulivu na usalama
vinakuwepo wakati wote kwa kuweka mazingira salama kwa wananchi kuendesha
shughuli za kujiletea maendeleo yao na
wakati huo huo kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza
mitaji yao katika sekta za kiuchumi kwa faida ya maendeleo ya nchi yetu.
Pamoja na ukweli huo, mafanikio ya hatua za Polisi yanategemea mashirikiano ya
jamii na mtu mmoja mmoja.
Kuzuia
na Kudhibiti Vitendo vya Uhalifu na Ajali za Barabarani
36.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi liliendelea
kutekeleza jukumu lake la kisheria la kuhakikisha usalama, amani na utulivu
vinakuwepo hapa nchini. Pamoja na changamoto zilizojitokeza, Jeshi la Polisi
lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuwalinda wananchi na mali zao, kusimamia
utii wa sheria za nchi, kuzuia makosa ya jinai na usalama barabarani,
kupeleleza makosa ya jinai, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wa
makosa ya jinai na makosa ya usalama barabarani. Mafanikio haya yanathibitishwa
na kupungua kwa makosa makubwa ya jinai yakiwemo mauaji na unyang’anyi wa
kutumia silaha kwa kiwango cha asilimia 4.3 na kupungua kwa ajali za barabarani
kwa asilimia 1.9. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha
doria, misako na operesheni maalum ili kupunguza matishio ya uhalifu, makosa
makubwa ya jinai na ajali za barabarani kwa kiwango cha asilimia 10.
Programu
ya Maboresho ya Jeshi la Polisi
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi liliendelea
kutumia fedha za bajeti zilizoidhinishwa na Bunge lako Tukufu kuimarisha mifumo
ya kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu na makosa ya usalama barabarani na
kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kazi za Polisi. Pia Jeshi la Polisi
liliendelea kuimarisha mifumo ya menejimenti ya rasilimali watu na ustawi wa
askari kijamii na kiuchumi, kuandaa mikakati mipya ya kupunguza tatizo la uhaba
na uchakavu wa kambi na vituo vya Polisi, kupunguza tatizo la uhaba wa vitendea
kazi hususan magari na pikipiki na kuhamasisha wananchi na wadau wa usalama wa
raia kuhusu Ulinzi Shirikishi na Utii wa Sheria Bila Shuruti.
38. Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa kama
sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Maboresho, Jeshi la Polisi limeanza
utekelezaji wa mfumo wa kupima kiwango cha ufanisi wa Maafisa, Wakaguzi na
askari kwa kutumia mkataba wa utendaji (Performance Contract) uliosainiwa kati
ya mtendaji mmoja mmoja na kiongozi wake wa kazi. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi
la Polisi litapima ufanisi wa utendaji kwa ngazi ya Mkoa/Kikosi, Wilaya,
Tarafa/Jimbo na Kata/Shehia na litaendelea kutekeleza malengo na shabaha
zilizomo katika maeneo saba ya maboresho
kama yalivyoidhinishwa na Baraza la Mawaziri mnamo tarehe 31 Machi 2011.
Mkakati
wa Kupunguza Uhalifu
39. Mheshimiwa Spika, mkakati wa kupunguza uhalifu unaotumiwa pia na
majeshi mengine ya Polisi duniani umelisaidia Jeshi la Polisi nchini kubaini,
kuzuia na kudhibiti uhalifu na wahalifu kwa kiwango kikubwa katika mwaka
2012/2013. Mkakati huo unaelekeza mbinu na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kabla
uhalifu haujatendeka, baada ya uhalifu kutendeka, mshtakiwa anapofikishwa
mahakamani na ufuatiliaji wa wahalifu wa kawaida na wahalifu wazoefu baada ya
kumalizika kwa kesi zao mahakamani. Matumizi ya mbinu hizi yanahusisha ushirikiano
wa karibu kati ya Jeshi la Polisi na vyombo vinavyounda Jukwaa la Haki Jinai
pamoja na raia wema.
40. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mbinu zinazotumika kuzuia uhalifu kabla
haujatendeka ni pamoja na kutambua maeneo hatarishi ambayo uhalifu hutendeka
mara kwa mara na kuongeza doria ya askari Polisi na vikundi vya ulinzi
shirikishi katika maeneo hayo na kufuatilia nyendo za wahalifu wazoefu mara
wanapomaliza kutumikia adhabu gerezani. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi
litaendelea kutumia mkakati wa kupunguza uhalifu ili kila Mkoa wa Kipolisi
ufikie shabaha ya kupunguza uhalifu kwa asilimia 10.
Mauaji
ya Wazee na Vikongwe Kwa Imani za Kishirikina
41. Mheshimiwa Spika, kumekuwa na wimbi la mauaji ya wazee na vikongwe
hasa katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora, Mbeya, Rukwa, Iringa na
Singida. Katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2012, takwimu za Jeshi la Polisi
zinaonyesha kwamba jumla ya wazee na vikongwe 1,271 waliuawa katika Mikoa hiyo
kutokana na imani za kishirikina. Kati ya idadi hiyo, wanaume walikuwa 532 sawa
na asilimia 41.9 na wanawake 739 sawa na asilimia 58.1. Serikali inalaani kwa
nguvu zake zote mauaji haya ya wazee na imani za kishirikina katika karne hii
ya 21.
42. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hali hiyo, Jeshi la Polisi
limeweka mikakati ifuatayo:-
i) Kuendelea kuwahamasisha wananchi
kutekeleza kwa vitendo falsafa ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi kama
mkakati mkuu wa kuzuia uhalifu katika maeneo wanayoishi
ii) Kuendelea kushirikiana na raia
wema, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi zinazoratibu shughuli za waganga
wa jadi kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani waganga wanaothibitika
kupiga ramli za uchochezi na kusababisha mauaji ya wazee na vikongwe
iii) Kuendelea kushirikiana na raia wema
na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani
wahalifu wanaokodishwa kufanya mauaji ya wazee na vikongwe
iv) Kuendelea kutumia taarifa za
kiintelijensia kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani wanaotuhumiwa
kutoa fedha kwa waganga wa jadi kwa lengo la kuambiwa waliowaua ndugu zao au
kupewa mbinu na masharti ya kupata utajiri wa haraka
v) Kuendelea kukiimarisha Kitengo cha
Intelijensia cha Jeshi la Polisi kwa rasilimali watu na vitendea kazi
kuanzia ngazi ya Makao Makuu hadi ngazi
ya Kata/Shehia ili kujenga uwezo wa kupata mapema taarifa za uhalifu Mijini na
Vijijini
vi) Kuendelea kutumia Vikosi Kazi vya
Kitaifa, Mikoa na Wilaya kuendesha operesheni maalum za kuzuia na kudhibiti
ongezeko la mauaji ya wazee na vikongwe katika Mikoa iliyokithiri kwa mauaji
hayo.
Natoa wito kwa Watanzania wote
kushirikiana na Serikali kukomesha mauaji, hofu na unyanyasaji kwa wazee.
Huduma
za Polisi Katika Tarafa/Jimbo, Kata/Shehia na Maeneo Maalum ya Uwekezaji
43. Mheshimiwa Spika, idadi ya watu na mahitaji ya huduma ya usalama
wa raia na mali zao yanazidi kuongezeka kila mwaka hususan kwenye ngazi ya
Tarafa/Jimbo, Kata/Shehia na maeneo mapya ya makazi na uwekezaji. Katika mwaka
2012/2013, Jeshi la Polisi lilinunua pikipiki 564 kwa ajili ya kuimarisha
utendaji kazi wa Wakaguzi wa Tarafa kwa Tanzania Bara na Majimbo kwa Zanzibar.
Aidha, vitengo vipya vilivyoanzishwa Makao Makuu ya Polisi kwa ajili ya
kuratibu usalama katika migodi, ulinzi wa mazingira na usalama wa watalii
vilianza kazi rasmi kwa kupatiwa watendaji hadi ngazi ya Kituo cha Polisi.
Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaongeza idadi ya askari katika
Kata/Shehia ambazo ni tishio kwa uhalifu na kununua pikipiki kwa ajili ya
kuimarisha doria na misako katika Kata /Shehia
hizo.
Kuongeza
Matumizi ya TEHAMA Katika Kazi za Polisi
44. Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya mbinu za kutenda uhalifu na
maendeleo ya Sayansi na Teknolojia duniani ni changamoto kwa Jeshi la Polisi
hivyo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni ya lazima ili kuongeza
uwezo wa Jeshi la Polisi kubaini na kutanzua uhalifu nchini. Katika mwaka 2012/2013,
Jeshi la Polisi limeajiri wataalam 355 wa fani ya TEHAMA ambao wanaendelea na
mafunzo ya awali ya uaskari katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi. Mfumo wa
kisasa wa kuchukua alama za vidole za watuhumiwa (Automated Fingerprints Information System - AFIS) umeendelea kusimikwa
katika vituo vya Polisi. Aidha, Mkandarasi atakayesimika mfumo wa ufuatiliaji
wa washtakiwa (Offender Management
Information System - OMIS) ameanza kazi za awali katika Mkoa wa Dar es
Salaam na Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai. Katika mwaka
2013/2014, Jeshi la Polisi litawapanga askari wapya wenye fani ya TEHAMA
kufanya kazi katika Mikoa yote nchini na litaendelea kutekeleza awamu
zinazofuata za miradi ya AFIS na OMIS kwa mujibu wa mikataba na uwezo wa
kibajeti.
Jukwaa
la Haki Jinai
45. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, ushirikiano wa kiutendaji
kati ya Jeshi la Polisi na taasisi nyingine zinazounda Jukwaa la Haki Jinai
ambazo ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Jeshi la Magereza na Mahakama
uliendelea kuimarika. Viongozi wa Taasisi hizo walishiriki katika mkutano mkuu
wa Maafisa Waandamizi wa Polisi uliofanyika Mjini Dodoma mwezi Februari 2013 na
kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha utoaji wa haki hapa nchini. Jeshi la
Polisi lilijikita katika eneo la kuongeza ufanisi katika upelelezi wa makosa ya
jinai na hivyo kufanikiwa kuongeza kiwango cha washtakiwa kupatikana na hatia kutoka
asilimia 5 mwaka 2011 hadi asilimia 11.6 mwaka 2012. Katika mwaka 2013/2014,
Jeshi la Polisi litaanza rasmi kutumia mitihani ya kupima ujuzi ili kujenga na
kuongeza weledi wa askari wake katika fani za Intelijensia na upelelezi.
Udhibiti
wa Uzagaaji wa Silaha Ndogondogo
46. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi liliendelea kuweka alama maalum
katika silaha ndogondogo zinazomilikiwa na taasisi za Serikali, makampuni na
watu binafsi kwa lengo la kudhibiti uzagaaji wa silaha na matumizi ya silaha
hizo katika uhalifu. Katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013, jumla
ya silaha 15,003 zimewekewa alama hiyo hivyo kufanya jumla ya silaha 52,607 zilizowekewa alama hiyo tangu zoezi hili lilipoanza
mwaka 2009. Hadi sasa zoezi la kuweka alama kwenye silaha limefanyika katika
Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, Tabora,
Manyara, Singida, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara. Taasisi ambazo silaha zao
zimewekewa alama maalum ni pamoja na Tanzania National Parks Authority (TANAPA),
BARRICK GOLD, Bank of Tanzania (BoT), GRUMET GAMES RESERVES na Ngorongoro
Conservation Area Authority (NCAA). Katika mwaka 2013/2014, zoezi hilo litaendelea
kutekelezwa na sheria mpya ya kusimamia na kudhibiti umiliki na utumiaji wa
silaha za kiraia inatarajiwa kuanza kutumika.
Ushirikiano
wa Polisi Kikanda na Kimataifa
47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi
lilishiriki katika mafunzo, ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia,
operesheni za kikanda na lilikuwa mwenyeji wa vikao vya kamati na mkutano mkuu
wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) ambavyo
vilifanyika Zanzibar na Dar es Salaam mwezi Septemba 2012 na Machi, 2013. Kwa
mpangilio huo, Jeshi la Polisi liliendelea kushirikiana na Mashirika ya Polisi
ya kikanda na kimataifa katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu hapa nchini.
Mashirika hayo ni pamoja na Shirikisho
la Polisi la Kimataifa – Interpol,
Shirikisho la Polisi la nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika – EAPCCO na Shirikisho la Polisi la nchi
za Kusini mwa Afrika SARPCCO. Katika
mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na majeshi mengine ya
polisi kikanda na kimataifa ili kuimarisha udhibiti wa makosa yanayovuka mipaka
ukiwemo ugaidi, uharamia, biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya
kusafirisha binadamu, uhamiaji haramu, wizi wa magari, wizi wa kutumia mitandao
ya TEHAMA, bidhaa bandia, biashara haramu ya silaha na uchafuzi wa mazingira.
Kuimarisha
Mifumo ya Menejimenti ya Rasilimaliwatu
48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, jumla ya askari 3,024
waliajiriwa na 5,637 wa vyeo mbalimbali walihudhuria mafunzo na kupandishwa
vyeo. Mafunzo ya upandishwaji vyeo yalifanyika kama ifuatavyo:- Uofisa (200),
Ukaguzi mdogo (597), RSM (47), Sajini Taji (404), Sajini (882) na Koplo (3,502).
Aidha, Inspekta Jenerali wa Polisi alihamisha Maafisa, Wakaguzi na askari
wapatao 540 kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji katika komandi za Jeshi
la Polisi nchini na kuziba nafasi zilizoachwa wazi kutokana na Maafisa na
askari kwenda nje ya nchi kushiriki katika Ulinzi wa Amani. Katika mwaka 2013/2014,
Jeshi la Polisi litaajiri askari wapya 3,000 na kuwapandisha vyeo jumla ya
askari 7,110 wakiwemo NCO wenye elimu ya shahada ya kwanza na shahada ya
uzamili. Pia Jeshi la Polisi litaendelea kuwaruhusu Maafisa, Wakaguzi na askari
kufanya mitihani maalum inayowawezesha kushiriki katika Operesheni za Ulinzi wa
Amani ndani na nje ya nchi.
49. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, jumla ya Maafisa watano
wamesimamishwa kazi, 12 mashtaka ya kijeshi yanaendelea dhidi yao na wengine 28
wameandikiwa barua za kujieleza kwa nini wasishtakiwe kijeshi kutokana na
makosa mbalimbali ya kinidhamu.
Ushughulikiaji
wa Malalamiko
50. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kupokea na
kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya watendaji wachache wanaojihusisha
na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo kuomba na kupokea rushwa. Katika
mwaka 2012 malalamiko yaliyopokelewa yalikuwa 314 ikilinganishwa na malalamiko
340 yaliyopokelewa mwaka 2011. Malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi
yalikuwa 193 na 121 yalikuwa ni madai ya askari kuhusu stahiki zao mbalimbali. Malalamiko
213 kati ya 314 yamejibiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kutokana na ushughulikiaji wa
malalamiko mbalimbali ya ukiukwaji wa maadili askari 99 walishtakiwa kijeshi na
kufukuzwa kazi na mwingine mmoja amesimamishwa kazi kutokana na kukiuka maadili
ya ajira ndani ya Jeshi la Polisi hali iliyosababisha askari wanafunzi 95
kutopokelewa kuanza mafunzo katika Chuo cha Polisi Moshi.
51. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho askari 13 walitunukiwa sifa
na zawadi ya jumla ya shilingi 7,540,000 kwa kukataa kupokea rushwa. Askari hao
ni wa Mikoa ya Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Rukwa, Shinyanga, Temeke na
Kaskazini Pemba. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia
nidhamu na maadili ya Maafisa, Wakaguzi na askari wake ikiwa ni pamoja na kutoa
ufumbuzi wa haraka wa malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi. Jeshi
litaendelea pia kutekeleza Programu ya Kupambana na Rushwa nchini inayofadhiliwa
na Shirika la Misaada la Uingereza (DFID).
Kuimarisha
Miundombinu na Vitendea Kazi vya Polisi
52. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Polisi liliendeleza ujenzi wa jengo
la Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi Dar es Salaam, kuanza hatua za awali za kusimika
mfumo wa OMIS na kukamilisha awamu ya kwanza ya
utekelezaji wa mradi wa kuimarisha usalama wa mizigo na huduma
zinazosafirishwa kupitia barabara kuu za Tanzania hususan barabara kuu ya Dar
es Salaam hadi Rusumo. Miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni
10.1 haikuendelezwa kutokana na ufinyu wa bajeti ya maendeleo. Aidha, taratibu
za kisheria za kuanzisha Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi (Police
Force Corporation Sole) zimekamilika. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi
litaendeleza ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi, Kituo cha
Polisi Vikokotoni, kukamilisha ujenzi wa nyumba za askari katika Mikoa ya
Mwanza, Kagera, Mara na Iringa na kuendeleza miradi ya AFIS na OMIS. Kuhusu
vitendea kazi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inakamilisha taratibu za kupata
magari ya aina mbalimbali kwa ajili ya kazi za Jeshi la Polisi kupitia
ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Serikali ya Watu wa China na India.
JESHI LA MAGEREZA
Usafirishaji
wa Mahabusu Kwenda Mahakamani na Kurudi Magerezani
53. Mheshimiwa Spika, jukumu la kuwasindikiza mahabusu kwenda
Mahakamani na kurudi Gerezani linaendelea kutekelezwa katika Mikoa ya Dar es
Salaam na Pwani. Hivi karibuni jukumu hili
limeanza kutekelezwa katika Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Dodoma katika Wilaya tatu
za Dodoma Mjini, Dodoma Vijijini na Mpwapwa. Utaratibu huu umeonyesha mafanikio
katika suala zima la kupunguza msongamano wa mahabusu Magerezani kwa sababu
mahabusu hufikishwa Mahakamani kwa tarehe walizopangiwa na Mahakama ambapo
wengine huachiliwa kwa dhamana au kesi zao kufutwa na nyingine kumalizika kwa
mujibu wa sheria. Lengo la mwaka 2013/2014, ni kutekeleza jukumu hili katika
Wilaya za Mkoa wa Dodoma zitakazokuwa zimesalia na kuanza katika Mkoa wa
Mwanza.
Programu za Urekebishaji wa Wafungwa
54. Mheshimiwa Spika, mradi wa uendeshaji wa shughuli za wafungwa kwa kutumia
mtandao wa kompyuta kwa awamu ya pili unaendelea baada ya awamu ya kwanza
kukamilika. Utekelezaji wa awamu ya pili umeanza kwa kusimika miundombinu
katika Magereza ya Butimba – Mwanza, Uyui - Tabora na ofisi za Magereza katika
Mikoa hiyo. Kazi kama hiyo inatarajiwa kufanyika katika ofisi ya Magereza Mkoa
wa Dodoma, Gereza Kuu la Isanga na Msalato. Kwa ujumla mfumo huu umesaidia
kujenga uwezo wa Jeshi la Magereza katika upatikanaji wa taarifa za wahalifu
zilizo sahihi na kwa wakati, kujua maendeleo na mwenendo mzima wa wahalifu
katika maeneo mbalimbali yaliyounganishwa katika mfumo huu. Katika mwaka
2013/2014, Jeshi la Magereza litaendelea na awamu ya pili ya utekelezaji wa
mpango huu kwa Mikoa mingine mitatu ambayo itaanzia na vituo vya Magereza Makuu
ya Ruanda - Mbeya, Maweni – Tanga na Arusha kisha kumalizia ofisi za Magereza
katika Mikoa ya Mbeya, Tanga na Arusha.
Ajira na Mafunzo
55. Mheshimiwa Spika, kibali cha kuajiri askari wapya 1,000 kimepatikana
na mchakato wa ajira umeanza. Jumla ya watumishi 2,413 wamepatiwa mafunzo. Katika
mwaka 2013/2014, Jeshi la Magereza linatarajia kuajiri askari wapya 1,020 na
watumishi raia 15 wa fani mbalimbali na kuwapatia mafunzo watumishi 520 nje ya Vyuo vya Jeshi la Magereza na askari
1,787 ndani ya vyuo vya Jeshi.
Uimarishaji
wa Magereza Yenye Ulinzi Mkali
56. Mheshimiwa Spika, ukarabati na uboreshaji wa majengo na miundombinu
ya Magereza yenye ulinzi mkali umefanyika na unaendelea katika Gereza la
Butimba sehemu za wanawake, kiwanda na mahabusu. Katika mwaka wa fedha wa
2013/2014, ukarabati wa majengo na miundombinu utaendelea chini ya Programu ya
Maboresho ya Sekta ya Sheria nchini ( LSRP) katika Sehemu ya Wanawake ya
Magereza ya Ruanda – Mbeya, Karanga – Kilimanjaro, Musoma – Mara, Isanga –
Dodoma na Lilungu – Mtwara.
Upanuzi,
Ukamilishaji, Ukarabati na Ujenzi wa Mabweni ya Wafungwa
57. Mheshimiwa Spika, kazi ya ujenzi wa mabweni ya wafungwa katika
Gereza la Wilaya ya Chato unaendelea. Ukarabati wa ukuta wa ngome, upanuzi wa
sehemu ya wanawake na kuezeka upya mabweni ya wafungwa iliendelea katika
Magereza ya Kilwa na Bukoba. Katika
mwaka wa fedha wa 2013/2014, lengo ni kuanza kazi ya ukarabati wa mabweni ya
wafungwa katika Gereza la Mahabusu Sumbawanga na kuendeleza ujenzi wa mabweni
mapya katika Gereza Mkuza – Pwani.
Ujenzi
wa Ofisi za Wakuu wa Magereza wa Mikoa
58. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Jeshi la Magereza limeendelea
na ukamilishaji wa ujenzi wa Ofisi ya Magereza Mkoa wa Singida na ujenzi wa
Ofisi ya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi
litakamilisha ujenzi wa Ofisi ya Magereza Mkoa wa Singida, kuendeleza ujenzi wa
Ofisi ya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam na kuanza ujenzi wa Ofisi ya Magereza
Mkoa wa Tanga.
Matumizi
ya Nishati Mbadala Magerezani
59. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na
matumizi makubwa ya kuni Magerezani na hivyo kuwepo na tishio la uharibifu wa
mazingira, Jeshi la Magereza limeendelea kuchukua hatua za kuanza kutumia gesi
asilia (natural gas), gesi itokanayo na tungamotaka (biogas) na makaa ya mawe kama nishati mbadala kwa
kupikia chakula cha wafungwa Magerezani. Mfumo wa gesi itokanayo na tungamotaka
katika Gereza Ukonga umekamilika na umeanza kutumika. Matumizi ya makaa ya mawe
yanaendelea katika Magereza ya Mkoa wa Mbeya. Kwa sasa Jeshi la Magereza lipo
katika mchakato wa kutumia majiko yanayotumia kuni kidogo ambayo yameanza kutumika
katika Gereza Karanga – Moshi na Ilagala – Kigoma. Matarajio ni kueneza
matumizi ya nishati hii katika Magereza mengine yenye matumizi makubwa ya kuni
kadri uwezo wa fedha utakavyoruhusu.
Ujenzi
na Ukamilishaji wa Nyumba za Askari
60. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limekamilisha ujenzi wa jengo
la ghorofa la kuishi askari Mkoani Iringa na limeanza kutumika. Aidha, Jeshi
linaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba zilizojengwa kwa njia ya
ubunifu katika Magereza ya Ngara, Kasulu, King’ang’a, Mwanga, Masasi, Ngudu,
Kenegele, Nzega na Kambi ya Bugorola. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Jeshi
la Magereza litaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba katika Magereza ya
Butimba, Karanga na Mugumu. Aidha, nyumba zilizojengwa kwa ubunifu wa askari ambazo
zipo katika hatua mbalimbali pia zitaendelea kupewa kipaumbele katika
ukamilishaji wake.
Uimarishaji
wa Mifumo ya Majisafi na Majitaka
61. Mheshimiwa Spika, Magereza yaliyo mengi yanakabiliwa na tatizo la
ukosefu wa maji na uchakavu wa miundombinu ya majisafi na majitaka ambayo pia
inaelemewa na tatizo kubwa la msongamano wa wafungwa na mahabusu. Katika mwaka
wa fedha wa 2012/2013, ujenzi wa miundombinu ya majisafi umeendelea katika
Gereza Isupilo - Iringa na ujenzi wa mfumo wa majitaka unaendelea katika Gereza
Mkwaya – Mbinga. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, lengo ni kukarabati mfumo
wa majitaka na kuboresha mfumo wa majisafi katika Gereza Kuu Isanga.
Kilimo cha Umwagiliaji
62. Mheshimiwa
Spika, Jeshi la Magereza liliendelea na mchakato wa ujenzi wa miundombinu
ya kilimo cha umwagiliaji katika Gereza la Idete – Morogoro. Hatua mbalimbali
za kufanya tathmini ya athari za mazingira na usanifu wa michoro kwa ajili ya
mradi huo zimekamilika. Aidha, taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi
zinaendelea. Katika mwaka wa fedha wa
2013/2014, Jeshi la Magereza litaanza mchakato wa mradi wa umwagiliaji katika
Gereza Kitengule – Kagera uwezo wa fedha ukiruhusu.
Ununuzi wa Magari na Zana za Kilimo
63.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza bajeti ya mwaka 2012/2013, Jeshi la
Magereza halikuweza kununua matrekta kutokana na ukosefu wa fedha. Malengo kwa
mwaka 2013/2014, ni kuendelea kuyafanyia matengenezo matrekta yaliyopo pamoja
na zana zake. Aidha, katika kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji
Magerezani, Jeshi la Magereza linatarajia kununua magari madogo matatu kwa
ajili ya shughuli za utawala.
Shirika la Magereza
64.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Magereza limeendelea na uzalishaji wa bidhaa
zitokanazo na viwanda vidogo vidogo kwa kutengeneza samani za ofisi na bidhaa
za ngozi kwa ajili ya taasisi na Idara za Serikali na watu binafsi. Kwa upande
wa kilimo, eneo la ekari 6,400 limelimwa kwa matarajio ya kuvuna tani 8,640 za mazao
mbalimbali. Vile vile Shirika kupitia Kikosi Ujenzi cha Magereza limeendelea kufanya
kazi za ujenzi wa majengo ya taasisi za Serikali na watu binafsi. Kazi hizo ni
pamoja na ujenzi wa uzio wa Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii,
ukarabati wa majengo ya Idara ya Uhamiaji Mkoani Tanga, ujenzi wa Rest House ya
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na ujenzi wa mfumo wa majitaka Baraza la
Mitihani la Taifa. Matarajio ya mwaka 2013/2014, ni kuongeza shughuli za
uzalishaji kupitia miradi ya kilimo, mifugo na kutumia ipasavyo soko la samani
za ofisi, bidhaa za ngozi na shughuli za ujenzi ambalo linaendelea kupanuka.
HUDUMA KWA JAMII
65. Mheshimiwa Spika, Programu ya Huduma kwa Jamii ilianza rasmi mwaka 2005
kama adhabu mbadala ya kifungo gerezani. Hivi sasa programu hii inatekelezwa
katika Mikoa 16 ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara,
Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Iringa, Kagera, Mara, Shinyanga,
Ruvuma, Pwani, Geita na Morogoro. Katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari,
2013 jumla ya wafungwa 903 wamefaidika na programu hii. Wafungwa hao hutumikia
vifungo vyao nje ya magereza kwa kufanya kazi bila ya malipo katika taasisi za
umma. Changamoto kubwa ya programu hii ni Mikoa mingine kushindwa kunufaika
nayo kutokana na ufinyu wa bajeti, uhaba wa Maofisa wa Probesheni na baadhi ya Mahakimu
kujikita katika kutoa adhabu ya kifungo gerezani badala ya kutumia adhabu
mbadala.
IDARA YA UHAMIAJI
66. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji ina jukumu la kudhibiti
uingiaji, utokaji na ukaaji wa wageni, na pia kuwawezesha raia wa Tanzania
kupata hati za kusafiria. Aidha, Idara hii ndio inayoratibu mchakato wa maombi
ya uraia wa Tanzania kwa wageni.
Hali ya Ulinzi na Usalama Mipakani
67. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari,
2013 Idara iliendelea kutoa huduma katika mipaka kwa wageni wanaoingia na
kutoka nchini. Katika kipindi hicho, jumla ya wageni 801,676 waliingia na
wengine 729,078 walitoka. Kiujumla hali ya mipaka ni shwari na idadi ya
Wasomali na Waethiopia wanaosafirishwa
kwenda Kusini mwa Afrika kwa makundi imepungua kufikia 627 mwaka 2012 ikilinganishwa na 1,424 katika kipindi kama hiki mwaka 2011. Aidha, huduma zilizotolewa na
Idara ya Uhamiaji ni kama inavyoonyesha katika Jedwali Na. 4.
Tatizo
la Wahamiaji Haramu
68. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji imeendelea kupambana na
tatizo la wahamiaji haramu nchini. Tatizo hili linatokana na sababu za
kihistoria kama kuwepo kwa masalia ya wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa
Afrika, wakimbizi hususan wale wa muda mrefu waliotoroka toka makambi ya
wakimbizi pamoja na kundi la wahamiaji haramu hususan kutoka nchi za Pembe ya
Afrika kama Somalia, Ethiopia na Eritrea, ambalo lilianza kujitokeza mwaka
2007.
69. Mheshimiwa Spika, kundi hili la raia toka Pembe ya Afrika linakuwa
kubwa kutokana na mtandao wa usafirishaji unaoendesha biashara haramu ya
binadamu. Mtandao huo huanzia nchi wanazotoka hadi kule wanakoelekea Kusini mwa
Afrika kupitia hapa nchini na kuendesha biashara hii kwa kupata kipato. Kundi
hili linawajumuisha wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu (victims
of human trafficking) na raia wa kigeni wanaohiari wenyewe kusafirishwa na
mawakala haramu kuelekea nchi nyingine bila kufuata taratibu zilizowekwa
(smuggled persons). Makundi yote haya kwa ujumla yanatengeneza kundi moja la
wahamiaji haramu ambalo kwa sasa ni tatizo la kitaifa.
70. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari,
2013 Idara ya Uhamiaji iliendelea kufanya doria na misako yenye lengo la
kudhibiti wahamiaji haramu nchini ambapo jumla wahamiaji haramu 2,319
walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikilinganishwa na
wahamiaji haramu 5,603 waliokamatwa katika kipindi kama hiki mwaka jana.
71. Mheshimiwa Spika, kuhusu wahamiaji waliotokana na masalia ya
wapigania uhuru pamoja na wakimbizi waliotoroka makambini, Serikali imeamua kwa
kuushirikisha uongozi wa Mikoa husika kufanya operesheni ya kuwabaini na
kuwaondosha wahamiaji haramu hao. Mikoa ambayo itahusika na zoezi hilo ni Kagera, Kigoma, Rukwa na Mara kwa upande wa
Kaskazini na Magharibi mwa nchi yetu. Operesheni hii pia itafanyika katika Mikoa
ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa upande wa Kusini.
72. Mheshimiwa Spika, katika kupambana na tatizo linalokua la
usafirishaji wa binadamu, Serikali imebainisha biashara hii kuwa ni moja ya
uhalifu mkubwa wa kimataifa (Serious Crime). Serikali imeanzisha Kikosi Kazi
kinachopambana na wasafirishaji wa biashara hii haramu. Hadi sasa Serikali
imekamata na kutaifisha vyombo vya usafiri vinavyotumiwa na wasafishaji hao.
Kwa kuwa tatizo hili linazigusa nchi mbalimbali katika ukanda wanakotoka, wanakopitia
na kule wakoishia wahamiaji haramu, Serikali imefanya juhudi ya kuwa na vikao
vya pamoja na nchi hizo ili kutengeneza mikakati itakayowezesha kupata
suluhisho la pamoja katika kukabiliana na tatizo la wahamiaji haramu.
73. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji pia imeendelea kukabiliana na
tatizo hili kwa kufanya yafuatayo:- Kuendelea kushirikiana na nchi jirani kwa
kufanya mikutano ya ujirani mwema ya mara kwa mara pamoja na kuingia
makubaliano ya kufanya misako na kupeana taarifa ya biashara haramu ya binadamu
na wahusika kuchukuliwa hatua, kuendelea na zoezi la kuwaorodhesha wahamiaji
walowezi ili kuwatambua na kuwa na kumbukumbu sahihi. Kushirikisha wadau
wengine wa masuala ya Uhamiaji katika zoezi la kuwaondosha nchini wahamiaji
haramu waliokamatwa, kuendeleza mfumo wa Maafisa Uhamiaji Kata kwa lengo la
kushirikiana kwa karibu zaidi na jamii katika kutekeleza sheria ya Serikali za
Mitaa ya kumtaka kila mwenyeji kutoa taarifa ya mgeni yeyote anayeingia au
kuishi mahali popote ugenini, na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara
ya kuwahifadhi na kuwapa kazi wahamiaji haramu bila kuwa na vibali halali.
Vibali
Mbalimbali Vilivyotolewa kwa Wageni
74. Mheshimiwa Spika, Idara imetoa vibali kwa wageni wawekezaji, wageni
waliopata ajira katika makampuni na wageni wengine walioingia nchini kwa
malengo mbalimbali. Jumla ya wageni 12,878 walipewa hati za ukaazi kwa mchanganuo
ufuatao:- daraja “A” 1,191, daraja “B” 7,037, daraja “C” 2,571, hati za ufuasi
297 na hati za msamaha 1,782. Hati za msamaha ni vibali vya kuishi
vinavyotolewa kwa wageni bila malipo yoyote. Wageni hao ni wale wanaofanyaka
kazi katika Taasisi za Kimataifa zilizoko nchini (International Organizations),
Wawakilishi wa nchi pamoja na wafanyakazi katika Ofisi za Balozi mbalimbali
hapa nchini pamoja na wategemezi wao, wanafunzi toka nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki na nchi nyingine, pamoja na wageni toka nchi Washirika wa
Maendeleo wanaofanya kazi katika Mashirika ya Umma, Asasi za Kiserikali au katika
sekta mbalimbali Serikalini.
Hati
za Kusafiria
75. Mheshimiwa Spika, Idara imetoa jumla ya hati za kusafiria 31,347 kwa
Watanzania waliotaka kusafiri nje ya nchi kwa madhumuni mbalimbali. Kati ya hati
hizo 30,202 ni za kawaida, 818 za Afrika Mashariki, 212 za kibalozi na 115
za kiutumishi. Aidha, kukua kwa hali ya utandawazi kumesababisha kubadilika kwa
teknolojia ya udhibiti wa pasipoti na hati nyingine za safari. Kutokana na
mabadiliko hayo, Idara ya Uhamiaji imeanza mchakato wa kupata mitambo mipya ya
kuchapisha hati za safari itakayokuwa na uwezo wa kutoa hati zenye “ Biometric
Features” ili kuepuka tatizo la pasipoti za Tanzania kughushiwa kirahisi.
Wageni
Waliopatiwa Uraia wa Tanzania
76. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari,
2013 wageni 64 walipatiwa uraia. Wageni waliopata uraia ni wa kutoka India (27),
Kenya (7), Uingereza (2), Pakistani (5), Somalia (1), Japan (1), Lebanon (6),
Malawi (1), Burundi (6), Rwanda (1), Uganda (4), DRC (1), China (1) na Umoja wa
Falme za Kiarabu (1). Hivi sasa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaendelea kuandaa
Sera ya Uhamiaji na Uraia ili kushughulikia masuala ya uhamiaji na uraia nchini
kwa ufanisi zaidi.
Watanzania
Waliopatiwa Uraia wa Mataifa Mengine
77. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Watanzania 37 walipata uraia wa mataifa mengine kama
ifuatavyo:- Uingereza (1), Ujerumani (9),
Norway (14), Uganda (2), Uholanzi (1), Denmark (3), Namibia (5) na Zambia (2)
hivyo kupoteza haki ya kuwa raia wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995.
Wasomali
Waliovuliwa Uraia
78. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiwapa raia wa kigeni uraia wa
Tanzania wageni wakaazi walioomba na kukubaliwa baada ya kukidhi vigezo
vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria ya uraia. Hata hivyo kutokana na baadhi yao
kutokuwa waaminifu, kama Waziri mwenye dhamana kwa mamlaka niliyonayo chini ya
kifungu Na. 15(1) cha Sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995, nilifuta uraia wa
Tanzania kwa watu 102 raia wa Somalia (wakimbizi) waliokuwa wamepewa uraia wa
Tanzania kwa tajnisi baada ya kuthibitika kwamba waliwasilisha taarifa na
vielelezo visivyokuwa sahihi wakati wanaomba uraia. Hivyo kuanzia tarehe 6
Julai, 2012 wahusika wote walipoteza uraia wa Tanzania na wanatakiwa kuishi
nchini kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Na. 7 ya mwaka 1995 na Sheria ya
Wakimbizi Na. 8 ya mwaka 1998.
Ajira
na Mafunzo
79. Mheshimiwa Spika, watumishi wapya 52 wameajiriwa na wengine 385 walioko
kazini wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu. Kati yao tisa wamepata
mafunzo ya muda mfupi nje ya nchi, mmoja mafunzo ya muda mrefu nje ya nchi, 324
wamepata mafunzo ya muda mfupi ndani ya nchi na 51 walipatiwa mafunzo ya muda
mrefu ndani ya nchi. Katika mwaka 2013/2014, Idara inatarajia kutoa mafunzo kwa
watumishi 650 waliopo kazini.
Vyombo
vya Usafiri
80. Mheshimiwa Spika, Idara imenunua jumla ya magari 34 ambapo magari
10 ni aina ya Toyota Landcruiser Hardtop na 24 Toyota Hilux Pickup. Aidha,
imenunua mabasi madogo matatu (3) na pikipiki 100. Katika mwaka 2013/2014,
Idara ya Uhamiaji inatarajia kununua
magari 12, pikipiki 56, boti za doria tano na lori moja. Vyombo hivi vya
usafiri vitasaidia kuimarisha shughuli za misako na doria dhidi ya wahamiaji
haramu katika sehemu mbalimbali nchini zikiwemo zile za mipakani.
Majengo
ya Ofisi
81. Mheshimiwa Spika, Idara imekamilisha ujenzi wa ofisi za Uhamiaji
katika Mikoa ya Shinyanga na Morogoro. Aidha, ujenzi wa ofisi za Uhamiaji
katika Mikoa ya Ruvuma na Manyara unaendelea na mchakato wa kuwapata
Wakandarasi wa ujenzi wa ofisi za Uhamiaji katika Mikoa ya Pwani, Lindi na
Singida umeanza. Katika mwaka 2013/2014, Idara inatarajia kuanza ujenzi wa
ofisi mpya katika Mikoa ya Mtwara na Geita, ofisi ya Wilaya ya Ifakara Mkoani
Morogoro na kituo cha Kirongwe Mkoani Mara. Idara pia itaendelea na ukarabati wa
ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mbeya.
Makazi
ya Askari
82. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, Idara imenunua
maghorofa mawili Mkoani Tabora kwa ajili ya makazi ya askari yenye uwezo wa
kuishi familia 12 pamoja na nyumba tano za Maafisa Uhamiaji zenye uwezo wa
kuishi familia tano. Aidha, ujenzi wa nyumba tano za viongozi wa Idara ya Uhamiaji
Makao Makuu unaendelea Mtoni Kijichi – Dar es Salam. Katika mwaka 2013/2014,
Idara itaanza ujenzi wa nyumba za askari Kisongo Jijini Arusha na Chakechake – Pemba.
83. Mheshimiwa Spika, Idara imekamilisha ukarabati wa nyumba za askari Igoma - Mwanza na pia ukarabati
unaendelea katika vituo vya Horohoro – Tanga, Borogonja – Mara, Tunduma –
Mbeya, Tanga Mjini, Dodoma Mjini na mabweni ya Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda
Moshi. Katika mwaka 2013/2014, Idara inatarajia kufanya ukarabati wa nyumba za askari
zilizoko Mtoni Kijichi – Dar es Salaam.
Mapambano
Dhidi ya VVU/UKIMWI
84. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji imeendelea kutoa elimu pamoja
na kuwahudumia watumishi wanaoishi na VVU/UKIMWI kwa lengo la kupunguza
maambukizo mapya ya UKIMWI mahala pa kazi na kwa familia za askari. Aidha,
Idara imesambaza vipeperushi katika vituo vya kuingilia nchini vinavyolenga
kutoa elimu juu ya maambukizo ya VVU na UKIMWI pamoja na athari zake.
JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI
85. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji limeendelea kuokoa maisha na mali kwenye majanga ya moto na
majanga mengineyo yanayolikumba Taifa letu. Pamoja na majukumu haya ya msingi,
katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Februari, 2013, jumla ya maeneo 5,149 yalifanyiwa
ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kama ilivyofafanuliwa katika Jedwali Na. 5. Pia jumla ya magari
makubwa na madogo 6,455,447 yalikaguliwa. Huduma hii inatolewa kwa mujibu wa
Sheria ya Zimamoto na Uokoaji Na. 14 ya
mwaka 2007.
86. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji limefanikiwa kuwapatia mafunzo askari 72, ndani ya nchi askari
60 na nje ya nchi 12. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
litaendelea na zoezi la ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto, kuendelea kutoa
elimu juu ya kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo mbalimbali, na
litaendelea kuimarisha huduma zake kwa kujenga vituo vya Zimamoto na Uokoaji
kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.
IDARA YA WAKIMBIZI
87. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na jitihada mbalimbali zenye
lengo la kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la kuwepo maelfu ya wakimbizi hapa
nchini, ambao baadhi yao walikuwa wanasita kurejea kwenye nchi zao za asili
pamoja na kuwa hali ya usalama katika nchi hizo ilikuwa imeimarika vya kutosha.
Katika kukabiliana na tatizo hilo niliwavua hadhi ya ukimbizi, kwa mujibu wa
sheria, wakimbizi wa Burundi wapatao 38,000 na kuwataka kurejea kwenye nchi yao
ya asili na wale ambao wangekataa kutekeleza agizo hilo wangechukuliwa hatua.
Uamuzi huo uliwezesha raia wa Burundi wapatao 35,000 waliokuwa wanaishi kwenye
kambi ya Mtabila Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma kurejea nchini Burundi kwa kusaidiwa
na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNHCR na International Organization for Migration (IOM) na kuwezesha kambi
hiyo kufungwa rasmi tarehe 31/12/2012. Hivi sasa UNHCR wanafanya ukarabati wa
miundombinu ya kambi hiyo ili eneo la kambi likabidhiwe rasmi kwa uongozi wa
Mkoa wa Kigoma.
88. Mheshimiwa Spika, baada ya kufunga kambi ya Mtabila, kwa sasa
Tanzania inayo kambi moja tu ya Nyarugusu Wilayani Kasulu ambayo inahifadhi
wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Pamoja na kwamba hali
ya usalama katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini nchini DRC ambako
wakimbizi hao wanatoka bado sio ya kuridhisha, tunaamini kuwa yapo baadhi ya
maeneo katika majimbo hayo ambayo hali ya usalama inaridhisha ambapo wakimbizi
wa DRC wanaweza kuanza kurejea huko. Kwa kuzingatia hali hiyo, katika mwaka wa
fedha wa 2013/2014, Tanzania inakusudia kuitisha Kikao cha Pande Tatu
kitakachojumuisha Serikali ya Tanzania, Serikali ya DRC na UNHCR ili
kukubaliana namna ya kuwapa fursa wakimbizi wanaotoka maeneo ya Kivu Kaskazini
na Kusini kurejea nchini kwao bila ya kikwazo chochote. Aidha, katika kipindi
cha Julai hadi Desemba, 2012 wakimbizi 96 wa DRC walirejea kwao. Lengo pia ni
kuwezesha wakimbizi wote wa kambi ya Nyarugusu kurejea kwao na kambi hiyo
kufungwa.
89. Mheshimiwa Spika, vile vile Serikali imeendelea na mchakato wa
kutoa uraia kwa wakimbizi wa Somalia wa makazi ya Chogo yaliyopo Wilayani
Handeni ambao wametimiza sifa na masharti yaliyowekwa. Lengo ni kufunga makazi
hayo. Pamoja na jitihada hizo zilizofanya idadi ya wakimbizi kupungua, Tanzania
imeendelea kuwahifadhi wakimbizi ambapo takwimu zinaonyesha kuwa hadi tarehe 31
Desemba, 2012 ilikuwa inahifadhi jumla
ya wakimbizi 100,489 wakiwemo Warundi
35,343, Wakongo 63,330, Wasomali 1,574 na
242 wakimbizi wa mataifa mbalimbali kama ilivyofafanuliwa katika Jedwali Na. 6.
90. Mheshimiwa Spika, lipo kundi maalum la wakimbizi wa Burundi wapatao
162,000 walioingia nchini mwaka 1972 ambao wanaishi kwenye makazi ya Katumba na
Mishamo Mkoani Katavi na Ulyankulu Mkoani Tabora ambapo Serikali ipo kwenye
mchakato maalum wa kupata ufumbuzi wa kudumu wa hadhi yao.
MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA
91. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeajiri
watumishi 89, imenunua vitendea kazi muhimu vya ofisi vikiwemo vifaa vya
elektroniki na kuendelea na ukarabati wa ofisi katika Mkoa wa Dar es Salaam na
Zanzibar. Aidha, NIDA imempata Mkandarasi wa kujenga ofisi za utambuzi na
usajili za Wilaya zote nchini. Katika mwaka 2013/2014, NIDA itaendelea na zoezi
la utambuzi na usajili wa watu, kuajiri watumishi 542, kununua magari 20, kuendelea
kuweka mfumo wa mawasiliano kati ya ofisi za Wilaya na Makao Makuu ya NIDA, kuendelea
na uboreshaji wa upanuzi wa Makao Makuu ya NIDA na kukamilisha mchakato wa
kutunga sheria ya usajili na utambuzi wa watu.
V. TAARIFA YA
UTEKELEZAJI WA AHADI ZA SERIKALI BUNGENI 2012/2013
92. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Serikali
Bungeni katika mwaka 2012/2013, umezingatiwa katika hotuba hii katika eneo la III -Taarifa ya utekelezaji wa malengo
ya Ilani ya Uchaguzi na la IV - Mapitio ya utekelezaji wa bajeti
ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2012/2013. Ahadi hizo zipo katika
maeneo ya vitendea kazi, ajira na
mafunzo, misako na doria, ujenzi na ukarabati wa ofisi, vituo, nyumba na
magereza, zoezi la utambuzi na usajili wa
watu, kuwarejesha wakimbizi kwao na kuweka alama maalum katika silaha
zinazomilikiwa na taasisi za Serikali, makampuni na watu binafsi. Kwa ujumla
wake, taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali zilizotolewa Bungeni katika
mwaka 2012/2013, ni kama inavyoonyesha katika Kiambatisho Na. 1 cha hotuba hii.
VI.
SHUKRANI
93. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Anna
Margareth Abdallah Mbunge Viti Maalum kwa kuyapitia na kuyachambua Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Maelekezo na ushauri wa Kamati hiyo utaisaidia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
katika kutekeleza majukumu yake.
94. Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee nazitoa kwa Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Pereira
Ame Silima, Mbunge wa Chumbuni, Katibu Mkuu Ndugu Mbarak Abdulwakil, Naibu
Katibu Mkuu Ndugu Mwamini Malemi, Inspekta Jenerali wa Polisi Ndugu Saidi Mwema,
Kamishna Jenerali wa Magereza Ndugu John Minja, Kamishna Jenerali wa Zimamoto
na Uokoaji Ndugu Pius Nyambacha, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Ndugu Magnus Ulungi,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Ndugu Dickson Maimu, Mkurugenzi
wa Wakimbizi Ndugu Judith Mtawali, Mkurugenzi wa Huduma kwa Jamii Ndugu Fidelis Mboya, Wakuu wote wa
Idara na Vitengo, Makamanda, askari pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi ambao wamefanikisha maandalizi ya hotuba hii na pia kwa
kusaidia kufanikisha majukumu ya Wizara.
95. Mheshimiwa Spika, nachukua pia fursa hii kuwashukuru nchi wahisani ikiwemo
China, Marekani, Ujerumani, Misri, Botswana, Nigeria na taasisi za INTERPOL, IOM, EU, UNHCR, DFID, UNICEF,
WFP, Hanns Seidel Foundation na Pharm Access pamoja na wadau wengine wote kwa
misaada yao ambayo imeongeza uwezo wa kiutendaji katika Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi.
96. Mheshimiwa Spika, mwisho ingawa sio mwisho kwa umuhimu, ninawashukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal kwa maelekezo yao mbalimbali na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb), Waziri
Mkuu kwa kuhimiza utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
VII.
MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2013/2014
97. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naliomba Bunge lako
Tukufu lipitishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi kwa mwaka 2013/2014 ya shilingi 741,131,711,000 kwa ajili ya bajeti ya
matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Kati ya makadirio hayo, shilingi
578,284,694,000 ni za matumizi ya kawaida ambapo shilingi 271,572,291,000 ni
Matumizi Mengineyo na mishahara shilingi 306,712,403,000. Makadirio ya shilingi
162,847,017,000 ni kwa ajili ya mipango ya maendeleo. Mchanganuo ni kama
ifuatavyo:-
Fungu
14: Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Matumizi Mengineyo shilingi 18,610,590,000
Mishahara shilingi 1,812,194,000
Maendeleo shilingi 0.00
Jumla
shilingi 20,422,784,000
Fungu
28: Jeshi la Polisi
Matumizi Mengineyo shilingi 149,600,221,000
Mishahara shilingi 205,663,241,000
Maendeleo shilingi 8,980,451,000
Jumla
shilingi 364,243,913,000
Fungu
29: Jeshi la Magereza
Matumizi Mengineyo shilingi 53,510,022,000
Mishahara shilingi 72,758,378,000
Maendeleo shilingi 2,666,566,000
Jumla
shilingi 128,934,966,000
Fungu
51: Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Matumizi Mengineyo shilingi 2,107,467,000
Mishahara shilingi 2,711,513,000
Maendeleo shilingi 0.00
Jumla
shilingi 4,818,980,000
Fungu
93: Idara ya Uhamiaji
Matumizi Mengineyo shilingi 47,743,991,000
Mishahara shilingi 23,767,077,000
Maendeleo shilingi 151,200,000,000
Jumla
shilingi 222,711,068,000
98. Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote
kwa kunisikiliza.
99. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
3 comments:
This is my first timе go to ѕеe at here аnԁ і
аm actually haρρy to read еvеrthing
at sіngle place.
Μу blog poѕt Sixpack
I’m not thаt muсh of a іnternet readеr to be hοnest but your
sіtes геally nіce, kееp it up!
I'll go ahead and bookmark your website to come back in the future. All the best
Visit my web blog - home acne products
I am no longer positive the place you are getting your info, but good topic.
I needs to spend some time learning more or working out more.
Thank you for magnificent information I used to be in search of this info for my mission.
Post a Comment