YABAINIKA! JENGO LILILOPOROMOKA LILIONGEZWA GHOROFA SITA KINYEMELA...

Jengo lililoporomoka katika mitaa ya Morogoro na Indira Ghandhi, Dar es Salaam Ijumaa iliyopita.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limedai mbia wake katika ujenzi wa jengo lililoanguka  Ijumaa iliyopita Dar es Salaam, kampuni M/S Ladha Construction Limited, iliongeza ghorofa sita za ziada ‘kinyemela’.

Akizunguimza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alidai kampuni hiyo haikuwasilisha nakala za vibali kutoka kwa mamlaka zinazohusika, vya kuongeza ghorofa hilo hadi gHorofa 16, kama ilivyo kwa mujibu wa mkataba. 
Awali Mchechu alisema mbia alipata kibali cha ujenzi wa jengo husika kutoka Manispaa ya Ilala, chenye namba BP34259 kilichomruhusu kujenga gorofa 10 tu katika kiwanja hicho.
Mchechu alisema makubaliano ya mkataba wa ubia kati ya NHC, yanaonesha kuwa kazi ya mbia ni kugharamia ujenzi wote na NHC ilikuwa na wajibu wa kutoa ardhi ya kujenga ambayo, ni kiwanja kilichotumika.
“Agosti 22,2012, mbia alituharifu kuwa ameshapata vibali kutoka mamlaka husika na kwamba angependa aingie mkataba mdogo na NHC, kutambua ongezeko hilo na mabadiliko ya tarehe ya kumaliza mradi.
“NHC ilimjibu kuwa hakutakuwa na kipingamizi, kama mbia ataleta nakala ya vibali  kutoka mamlaka husika kwa ajili ya kumbukumbu za shirika, na pia ili kufikia hatua za uamuzi wa ndani,” alisema Mchechu.
Mchechu alisema mkataba ulimtaka mbia, kuhakikisha anamtafuta mkandarasi na mshauri wa mradi walio na sifa stahiki, ambao watakuwa na wajibu wa kusimamia kikamilifu ujenzi wa jengo husika.
“Tunaamini wataalam aliowatafuta na kupata vibali vya mamlaka husika vya kuwatumia kujenga jengo hilo, wanaaminika na mamlaka zenye dhamana ya kuthibitisha sifa zao,” alisema Mchechu na kuongeza kwa mujibu wa mkataba, ni wajibu wa mbia kusimamia kazi zote, upatikanaji wa fedha, vibali na kuajiri wataalam husika.
Alisema mkataba wa ujenzi wa jengo hilo ulisainiwa Februari 4,2007 ambapo NHC ilikuwa iwe na hisa 25 na mbia 75 mara baada ya mradi kukamilika.
Hata hivyo, shirika lilitoa ardhi huku mbia akitakiwa kugharamia ujenzi wote pamoja na usimamizi wa ujenzi.
“NHC wangepata asilimia nyingine 25 baada ya miaka 12 na wabia wangebakiwa na asilimia 50,” alisema Mchechu na kuongeza kuwa vigezo anavyotakiwa kuwa navyo mbia, ni pamoja na uwezo wa kugharamia ujenzi na mipango ya uendelezaji katika eneo husika.
“Kilichofanyika pale kwenye kiwanja hata kama uko nje ya NHC kinakera sana, ni mchanga tu ulioonekana…huoni hata zege bali kilichobaki baada ya jengo kuanguka ni mchanga tena mweusi na nondo tena mpya,” alisema Mchechu.
Wakati huo huo, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, amesema endapo Serikali ingefuata mapendekezo yaliyotolewa na Kamati aliyoiunda mwaka 2008, baada ya jengo moja kuanguka na kuua, maafa yaliyotokea juzi kutokana na kuanguka kwa jengo la ghorofa 16 yasingekuwepo.
“Tume niliyoiunda ilifanya kazi yake vizuri na kubainisha hali halisi na kutoa mapendekezo yake, endapo yangefanyiwa kazi, sidhani kama haya yanayotokea leo yangetokea,” alisema Lowassa kwa kifupi na kuondoka.
Naye Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, tatizo kubwa ni uhaba wa wataalam.
Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha redio cha Clouds, Silaa alisema manispaa zinakabiliwa na changamoto ya kuwa na wataalam wachache na wengi hawana utaalam wa kutosha.
Alisema changamoto kubwa inayozikabili manispaa hasa za jijini Dar es Salaam, ni wataalam, akitolea mfano Manispaa ya Ilala kwamba ina wahandisi saba na fundi wasanifu 14, na kati ya hao wahandisi wa majengo ni wawili tu na kati yao mwenye nishani ni mmoja.
"Unapomchukua mtu wa chini kumsimamia mtu wa juu, ni changamoto kubwa kwa kweli na ni sawa na kumwambia daktari wa kawaida kumsimamia kazi daktari bingwa," alisema Slaa.
Alisema pamoja na uhaba huo wa wataalam katika Jiji kubwa kama la Dar es Salaam, kwa mwezi wanapokea maombi ya majengo zaidi ya 20 ambayo yanahitaji ukaguzi.
"Wizara zote ziko katika jiji hili, taasisi mbalimbali, vyombo mbalimbali, bandari, wakazi lakini bado mgao wa Serikali wa wataalam ni sawa na maeneo mengine yaani mikoani, kwa kweli kwa huduma zote tunazotakiwa kutoa lazima kutakuwa na upungufu," alisema Slaa.
Alisema katika ujenzi, kazi ya manispaa ni kutoa vibali baada ya kupokea maombi, na pia kufanya ukaguzi kuangalia kama muombaji anajenga kwa kufuata kibali achopewa na pia kuhakikisha ramani aliyoombea, ndiyo inayotumika.
Alisema Bodi ya Ukadiriaji Majengo na Ubunifu Majenzi Nchini (AQRB), Bodi ya Wakandarasi (CRB) na Bodi ya Wahandisi (ERB), ndizo zenye jukumu la kusimamia ubora wakati manispaa ikisimamia mpango.

No comments: