MWANAMKE AUZA MTOTO WA KAKA YAKE SHILINGI MILIONI MOJA...

Kamanda DIwani Athumani.
Mkazi wa Kijiji cha Mpemba wilayani Momba, anashikiliwa na polisi mkoani Mbeya, kwa tuhuma za kumuuza mtoto wa kaka yake, ili apate fedha ya kusaidia kesi ya baba wa mtoto huyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athumani, alisema mwanamke huyo, Tabu Mwashipete (40), mkulima katika kijiji hicho, alikamatwa juzi saa 2:00 usiku akiwa katika harakati za kumuuza mtoto huyo, Hosea Mwashipete (5).
Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, Hosea alikuwa akiuzwa kwa mkazi wa Kijiji cha Mpemba, John Sinyinza (64), kwa gharama ya Sh milioni moja.
Sababu ya kumuuza mtoto huyo, kwa mujibu wa madai ya Kamanda Athumani, ni kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia katika kesi inayomkabili baba wa mtoto huyo, Simon Mwashipete anayekabiliwa na kesi ya mauaji nchini Malawi.
Kamanda Athuman alisema mama wa mtoto huyo alikwisha fariki dunia na kumwacha Hosea nyumbani kwa shangazi yake huyo, ambaye aliamua kumuuza ili kupata kiasi hicho cha fedha.
Inadawa tayari mwanamke huyo alishapokea Sh 100,000 na alikuwa katikia mazungumzo ya kumaliziwa Sh 900,000 zilizobakia ili amkabidhi Hosea kwa Sinyinza.
Hata hivyo, Kamanda Athumani alisema wakati mwanamke huyo akisubiria malipo hayo,  mteja wa biashara hiyo alitoa taarifa Polisi na kushiriki mtego   uliowezesha kukamatwa  kwa mwanamke huyo. 
Mwanamke huyo anaendelea kushikiliwa Polisi wakati taratibu za kisheria zikiendelea kufanyika, ili afikishwe mahakamani.
Wakati huo huo Kamanda Athuman alisema mchoma nyama, mkazi wa Iwambi jijini Mbeya, Leonard Kanyiki (35), ameuawa kwa kuchomwa kisu kifuani na mkazi mwenzake Abdul Saiboko(33), katika ugomvi uliozuka kwenye kilabu cha pombe za kienyeji.
Alisema mauaji hayo yalifanyika juzi saa moja usiku katika eneo la Iwambi, ambapo mtuhumiwa baada ya kuona mwenzake amekufa, alijichoma kisu kichwani kwa lengo la kujiua lakini hakufanikiwa.
Kamanda Athuman alisema baada ya mtuhumiwa kujichoma kisu kichwani, alikamatwa na watu waliokuwepo eneo hilo na kupelekwa katika  Hospitali ya Rufaa Mbeya ambako amelazwa na hali yake siyo nzuri.
Chanzo cha ugomvi kati yao hakijajulikana na uchunguzi unaendelea kufanyika.

No comments: