TUCTA YATAKA KODI YA MAPATO IPUNGUZWE...

Nicholaus Mgaya.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) limeazimia kushinikiza Serikali katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2013/14, ipunguze kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE) hadi asilimia 11 na kuongeza pensheni kwa wastaafu.

Katika azimio hilo, Tucta imepanga kuchukua hatua za kupinga ilichokiita uonevu kwa wafanyakazi, ikiwa kodi hiyo haitapunguzwa.
Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Nicholaus Mgaya, alisema hayo jana alipotangaza maazimio ya Baraza Kuu la Tucta, ikiwamo kumwalika Rais Jakaya Kikwete, kuwa mgeni rasmi katika sikukuu ya Mei Mosi.
Mbali na PAYE, Mgaya alisema Baraza pia, linakusudia kuanzisha mjadala, ili masuala ya matibabu kwa mfanyakazi, yabebwe na mifuko ya hifadhi za jamii iliyopo, badala ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Alisema Tucta imekuwa ikiisihi Serikali ipunguze kiwango cha kodi hiyo, lakini imekuwa ikipuuza na badala yake kufanya marekebisho ya kodi kulingana na kupanda kwa kima cha chini cha mshahara, utaratibu ambao haukubaliki.
“Baraza Kuu limeazimia uvumilivu sasa basi! Kwa nini wafanyakazi wachache wabebeshwe mzigo mkubwa wa kodi, huku wafanyabiashara wakubwa wakisamehewa au kulipa kodi ndogo isiyoendana na biashara zao?”Alihoji Mgaya.
Kuhusu bima ya afya, Mgaya alisema Baraza linahoji ulazima wa mwanachama kuhudumiwa matibabu na mifuko miwili, huku yote ikichangiwa na mwanachama na mwajiri.
“Ili kupunguza makato kwenye mshahara mdogo wa mfanyakazi, Baraza Kuu linataka kuanzishwe mjadala haraka iwezekanavyo, ili masuala ya matibabu kwa mfanyakazi yabebwe na mifuko ya hifadhi za jamii,” alisema.
Akizungumzia malipo ya uzeeni, alisema Baraza limebaini kuwa kasi ya maboresho ya mifuko ya hifadhi ya jamii ni ndogo, kwani wafanyakazi wameendelea kustaafu kwa malipo kidogo ya pensheni, huku mifuko ikiendelea kuneemeka.
“Baraza limetoa kipindi cha mwaka mmoja 2013/14 kwa Serikali, kukamilisha maboresho ya pensheni ikiwa ni pamoja na kima cha chini cha pensheni kuwa asilimia 80 ya mshahara wa aliyestaafu, na kuongezeka kulingana na ongezeko la mishahara,” alisema.
Mbali na hayo, Mgaya alisema Baraza hilo liliazimia kutoa mwaka mmoja 2013 hadi 2014 kwa Serikali, kuhakikisha wafanyakazi katika sekta zote wanalipwa kima cha chini cha mshahara, kinachokidhi mahitaji ya msingi ya maisha.
“Endapo Serikali itashindwa kufanya hivyo, shirikisho na vyama shiriki hatutasita kuchukua hatua za mgomo shinikizi kadri itakavyoonekana inafaa,” alihadharisha.
Mgaya alibainisha kuwa kiwango cha chini cha mishahara cha Sh 350,000 walichokuwa wakiomba, kilipatikana baada ya kufanya utafiti wa mwaka 2006. Alisema mpaka sasa Serikali haijakifikia wakati kimepitwa na wakati.
Baraza Kuu kwa mujibu wa Mgaya, pia liliazimia  maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Kitaifa, yafanyike mkoani Mbeya.
Alisema katika maadhimisho hayo, watamwalika Rais Kikwete, kuwa mgeni rasmi huku ikiwa na kauli mbiu “Katiba mpya izingatie usawa na haki kwa tabaka la wafanyakazi.“

No comments: