WAZEE WAKUMBUSHWA MEMA YA HAYATI EDWARD SOKOINE...

KUSHOTO: Gari alilokuwa akisafiria Edward Moringe Sokoine kutoka bungeni mjini Dodoma Aprili 12, 1984 likiwa eneo la ajali iliyotokea eneo la Dakawa, nje kidogo ya Morogoro baada ya kugongwa na gari aina ya Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na Dumisani Dube. KULIA: Hayati Edward Moringe Sokoine.
Wazee wa kimila wa Kimasai na wakazi wa Monduli wametakiwa kumuenzi aliyekuwa Waziri Mkuu, marehemu Edward Sokoine kwa kutunza mazingira na maeneo ya malisho aliyoacha enzi za uhai wake.

Ushauri huo ulitolewa jana na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa aliyeelezea kusikitishwa na hali mbaya ya mazingira ya Monduli Juu na eneo la malisho, huku akitaka wazee hao na wakazi wa eneo hilo kumuenzi Sokoine kwa  kutunza mazingira na ardhi ya malisho.
Alisema hayo kwenye hafla ya kumkumbuka Sokoine iliyofanyika Monduli Juu kuadhimisha ya miaka 29 tangu kifo chache siku kama ya jana mwaka 1984, kwa ajali ya gari Dakawa nje kidogo ya Morogoro wakati akitoka bungeni Dodoma.
“Nasikitika mazingira Monduli Juu ni mabaya … lile eneo lililotengwa na Sokoine kwa ajili ya malisho liko wapi, mnaligawa wenyewe. Miti imekatwa ovyo, mandhari yote nzuri aliyoacha imepotea.
“Kama Sokoine angefufuka leo, angewauliza ardhi yenu iko wapi na ile misitu pia iko wapi, mngemjibu nini?” Aliwahoji.
Alisema yeye akiwa Mbunge wa Monduli angeulizwa amefanya nini angekuwa na jibu la kumpa, kwamba ameendeleza kujenga shule aliyoacha na kuongeza nyingine.
Alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa moyo wa kuipenda Monduli kwa kusaidia kwa mambo mengi ya maendeleo. Alisema Rais Kikwete aliahidi kushiriki maadhimisho hayo mwakani ambapo marehemu Sokoine atakuwa anatimiza miaka 30 kaburini.
Akimwakilisha Rais Kikwete katika maadhimisho hayo, Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni, Dk Fenella Mukangara, alisema:“Tunahitaji kumuenzi Sokoine kwa vitendo vyake chanya, tuige moyo wake wa mapenzi wa kuhudumia wananchi bila kujali maslahi ya wachache.”
Alisema katika uhai wake, Sokoine alipiga vita watu wachache kuhujumu uchumi wa nchi. Alisema alikuwa kiongozi mfuatiliaji wa maagizo aliyotoa kwa watendaji na hakuwa mtu wa kusubiri ripoti ofisini.
Kutokana na ukweli huo, alitaka wananchi kumuenzi kwa kukataa wenye nia ya kupandikiza chuki, walalamishi kwa kila jambo na wasiotaka kuhudumia wananchi kwa maslahi ya Taifa.
“Tusimamie amani na utulivu hasa kwa wakati huu, huku tukijitathmini kuhusu umoja wetu bila kuruhusu wenye nia mbaya kuleta vurugu,” alisema.
Dk Mukangara alisema watu wa Dar es Salaam watamkumbuka Sokoine kwa kuruhusu usafiri binafsi wa daladala.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na viongozi wengine.

No comments: