WATUHUMIWA MAUAJI YA DEREVA WA BAJAJI KUANIKWA HADHARANI LEO...

Polisi wakipita mbele ya eneo la tukio kutuliza ghasia hizo zilizozuka baada ya dereva wa bajaji kuuawa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela, leo anatarajia ‘kuweka’ hadharani majina ya askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania(JWTZ) kambi ya Lugalo, wanaoshikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa Bajaj, Yohana Cyprian (20).

Akizungumza na mwandishi, Kenyela alisema uchunguzi wa suala hilo bado ulikuwa ukiendelea kufanywa na Polisi kwa lengo la kuwabaini watu wote waliohusika na ‘unyama’ huo ili waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili kulingana na taratibu na  sheria za nchi zilizopo.
“Kesho (leo) nitazungumzia suala hilo na mahali tulipofikia tangu kuanza kwa uchunguzi wetu, ikumbukwe kuwa tayari tulishasema kuwa tunawashikilia watu watano kutokana na tukio hilo, hivyo tutawataja kuwa ni akina nani ambao walihusika na baadaye kuwapeleka mahakamani” alisema Kenyela.
Awali akizungumzia tukio hilo, Kenyela alidai kuwa Machi 3 mwaka huu, Saa 9 alasiri eneo la Mbezi Beach kwa Mboma, watu hao wanadaiwa kumshambulia dereva huyo sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kumuua baada ya kutokea kwa purukushani zilizofanywa na wanajeshi hao katika ‘kijiwe’ kinachotumiwa kwa ajili ya uvutaji bangi.

No comments: