SAKATA LA WILFRED LWAKATARE LAZUSHA MALUMBANO BUNGENI...

Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma.
Suala la kushitakiwa kwa Mkurugenzi wa Ulinzi wa Chadema, Wilfred Lwakatare limetinga bungeni baada ya Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) kuonesha ushahidi wa karatasi wa njama za kupangwa kuuawa kwa waandishi wa habari na kusema yuko tayari kutoa ushahidi huo mahakamani, bungeni na hata mbinguni.

Sambamba na hilo, amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata haraka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa kwa kuwa na mawasiliano ya vitendo vya kigaidi na Lwakatare, hali inayoonesha kuwa mpango wa kuua waandishi ni wa chama hicho.
Pamoja na kauli ya mbunge huyo, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alimjibu Nchemba bila kumtaja jina, kuwa ndiye aliyepanga na Polisi kumbambikia kesi ya ugaidi Lwakatare na kueleza kuwa wana ushahidi wa Januari mwaka huu, mbunge huyo kuwalipa polisi.
Sakata hilo lilianza kufikishwa bungeni na Nchemba wakati akichangia hotuba ya makadirio na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/14 ambapo alisema ana ushahidi wa karatasi yenye maandishi ya mwandiko wa Lwakatare, unaoonesha alama zake za vidole  wakati akihojiwa na kurekodiwa kuhusu njama za mauaji ya mwandishi wa habari.
Alisema aliyerekodi, alimpelekea yeye (Nchemba) ushahidi huo na wako tayari kuwasilisha ushahidi huo mahakamani, bungeni au hata mbinguni.
“Chadema mnahangaika kubadili picha, lakini aliyepanga ni huyo Mkurugenzi wenu wa Ulinzi na wakubwa juu wanafahamu hivyo, manake ni mpango wa chama…Mbowe na Katibu Mkuu wamekuwa na mawasiliano ya karibu na Mkurugenzi wao, nawashangaa polisi hadi leo hawajawakamata, polisi mnasubiri nini? Wakamateni.
“Nawashauri Chadema haraka kimbilieni makanisani au misikitini mkatubu, look at you shameless (oneni msivyo na aibu), viongozi mnataka nchi halafu mnapanga kuua!” Alishangaa.
Baada ya Nchemba kumaliza kuzungumza, Mbunge wa Mbulu, Mustapha Akunaay (Chadema) aliomba mwongozo wa Spika na kutaka suala la Lwakatare lisijadiliwe bungeni kwa kuwa kesi iko mahakamani, lakini Spika Anne Makinda alieleza kutokana na juzi Kiongozi wa Upinzani bungeni, Mbowe kulizungumzia suala hilo, hakuwa na budi kutoa nafasi upande mwingine, na kutaka wote kuangalia tu suala hilo na kufuata kanuni.
Juzi Mbowe akiwasilisha hotuba ya kambi ya upinzani, bila kutaja majina, alitaka waliopanga kesi dhidi ya Lwakatare ambao alisema pia ni magaidi nao washitakiwe.
Hata hivyo, alipopewa nafasi, Lissu alimjibu Nchemba bila kutaja jina akisema: “Kuna watu humu ndani wanashirikiana na polisi kupanga kesi za ugaidi na tuna ushahidi wakiwasiliana kwa simu halafu wanasema wamekamata watu kwa ugaidi.
“Siku mbili kabla ya kukamatwa, huyu aliyepo bungeni alimlipa polisi…ilikuwa Januari 14 na Desemba 28 mwaka jana; kuna ushahidi mwingine wa mawasiliano na magaidi hivyo na yeye (Nchemba) ni gaidi, akamatwe”.

No comments: