WALIMU 435 WAGOMEA RATIBA YA UGALI BUNDA...

Chuo cha Ualimu Bunda, mkoani Mara.
Wanachuo 435 wa mwaka wa pili katika Chuo cha Ualimu Bunda, mkoani Mara, juzi waligoma kula chakula cha jioni kutokana na madai mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubadilishiwa ratiba ya chakula kwa kutopikiwa wali kama ratiba ilivyokuwa inaonesha na badala yake wakapikiwa ugali.

Kufuatia hali hiyo, jana polisi wakiwa wamejiandaa kwa mabomu ya machozi na silaha mbalimbali walifika chuoni hapo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.
Aidha, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bunda, chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya, Joshua Mirumbe aliyewakilishwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Dominicus Lusasi ilifika chuoni hapo na kukutana na wanachuo hao ambao ni wa mwaka wa pili.
Katika kikao hicho iliamriwa kuwa kuanzia sasa ratiba ya chakula ifuatwe na wanachuo hao siku zinazoonesha ratiba ya kula wali wapikiwe chakula hicho.
Wakizungumza katika kikao hicho, waliyataja madai mengine kuwa ni kutorudishiwa kwa pesa zao walizotumia kununua vifaa vya kufundishia wakati wa mafunzo kwa vitendo.
Walisema kuwa wakati wa mafunzo kwa vitendo serikali ilikuwa haijaleta fedha za kununua vifaa vya kufundishia, hali iliyowalazimu kila mwanachuo kutoa fedha zake na kununua vifaa hivyo, ili kazi hiyo iende vyema.
“Tulitumia fedha zetu kununua vifaa vya kufundishia ili zoezi hilo liweze kwenda vizuri, lakini sasa tunashangaa hawataki kuturudishia,” alisema mwanachuo mmoja.
Walisema kuwa sasa wanautaka uongozi wa chuo hicho uwalipe fedha hizo kwani tayari wizara ilikwishazituma na kwamba kila mwanafunzi anatakiwa alipwe kiasi cha Sh 48,000.
Waliongeza kuwa, madai mengine ni pamoja na michango mbalimbali wanayodaiwa kuchangishwa, licha ya kuwepo waraka wa serikali wa kuzuia michango hiyo na kwamba sasa wanataka muafaka ili waweze kupewa fedha zao.
Alisema wamekuwa wakichangishwa Sh 5,000 za mahafali, lakini chakula wanachokula siku hiyo ni cha shule, wanafanyishwa kazi ya ulinzi, upasuaji kuni na mwaka jana pesa za chakula wakati wa mafunzo kwa vitendo zilikuwa Sh 50,000 kwa kila mwanafunzi lakini walipatiwa Sh 14,500.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Josephat Rweyemamu alikanusha madai yote ya wanachuo hao na kusema kuwa fedha hizo za vifaa vya kufundishia wizara ilitoa agizo kuwa zinunue vifaa vya kufundishia na sio kuwapatia pesa taslimu wanachuo hao.
Hata hivyo, Katibu Tawala alimwagiza mkuu wa chuo hicho kuiandikia barua wizara kuhusu madai ya wanachuo hao kuhusu fedha zao walizonunua vifaa vya kufundishia ili waweze kurejeshewa.

No comments: