MWANAJESHI WA DRC AKIRI KUBAKA WANAWAKE 53, WAMO WATOTO WA MIAKA MITANO...

Mmoja wa wanajeshi wa DRC akizungumza na watoto kwenye ukanda wa vita.
Mwanajeshi wa Congo amekiri kubaka wanawake 53 wakiwamo watoto wenye umri wa hadi miaka mitano wakati yeye na wenzake walipovamia mji mmoja katika vita ya kutisha ya wenyewe kwa wenyewe.

Mwanajeshi huyo alikuwa mmoja kati ya maelfu ambao waliteremka Minova, karibu na Ziwa Kivu katika Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, na kutumia siku mbili kubaka, kupora na kuua kabla ya maofisa kufanikiwa kudhibiti hali hiyo.
Ushahidi huo wa kutisha umekuja huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague juzi kuahidi kutumia Pauni za Uingereza milioni 10 kukabiliana na vurugu na mateso dhidi ya wanawake kwenye ukanda wa vita.
Mwanajeshi huyo mwenye miaka 22, akizungumza karibu na mahali ambako alifanya uhalifu huo, alieleza jinsi yeye na wenzake zaidi ya 24 walivyojumuika na kuamua kuwabaka wanawake 10 kila mmoja kabla ya kuanza kufanya ukatili huo.
"Nimebaka wanawake 53," alisema, "na watoto wenye umri wa miaka mitano au sita."
Yeye na wanajeshi wenzake walishindwa mapambano dhidi ya wapiganaji waasi wa kundi la M23 katibu na mji wa Goma. Miundo ya amri ilivunjika na walikuwa wametahayari, hasira na kushindwa kujizuia.
Waliwasili Minova wakiwa wamelewa, wenye njaa na wenye shari, na kuingiza mji huo katika siku mbili za njozi za damu kabla ya jeshi kuweza kurejesha nidhamu.
Daktari mmoja alisema hospitali yake ilitibia zaidi ya wanawake 100 kutokana na majeraha yaliyotokana na kubakwa.
Hatahivyo, mwanajeshi huyo ambaye ameongea hadharani kuhusu uhalifu wake alisema yeye na wenzake hawakufanya uhalifu wao kwa chuki, lakini kwa kujifurahisha.
"Tungeweza kufanya chochote tulichotaka," alisema.
Ubainikaji huo utaongeza uharaka katika jitihada za kundi la G8 la mataifa yaliyoendelea kupambana na mashambulio ya ubakaji katika ukanda wa vita, ambao unasukumwa na nyota wa Hollywood, Angelina Jolie.
Jolie, ambaye ni mjumbe maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, aliungana na Hague katika mkutano wa mawaziri wa nchi za nje wa kundi la G8 mjini London juzi mchana wakati Waziri wa Mambo ya Nje alipotangaza mchango huo wa Uingereza wa Pauni milioni 10.
Ahadi hiyo ya Uingereza itachangia sehemu kwenye ahadi ya jumla ya Pauni milioni 23 iliyotolewa na mataifa yanayounda kundi la G8.
Hague alisema sehemu ya fedha hizo itakwenda moja kwa moja katika mafunzo ya wakuu wa jeshi juu ya jinsi ya kushughulikia matukio ya ubakaji.
Lakini katika kesi hiyo iliyoibuliwa jana, walikuwa wanajeshi wao wenyewe wa DRC ambao walipatikana na hatia ya uhalifu wa ubakaji pale walipoanzisha mashambulizi yao Minova mnamo Novemba 22 mwaka jana.
Wengiwa waathirika wao walilazimika kwenda kwenye vituo vya wakimbizi wa ubakaji - kutokana na kukataliwa na familia zao na waume zao - hawana sehemu nyingine iliyobaki ya kwenda.
 Akizungumza kutoka katika kambi moja, Nzigire Chibalonza, mwenye miaka 60, alisema kwanza alipigwa vibaya mno na wanajeshi ambao walivamia dukani kwake, kabla ya watatu kati yao kumbaka.
"Sasa mume wangu kanifukuza," alisema. "Ananiita mke wa mwanajeshi. Amenikataa."
Jeshi la Congo linasema linachukua hatua kushughulika na wabakaji hao kwa uwezo wake. Endapo waathirika hawawezi kuwatambua washambulizi wao, waendesha mashitaka wametishia kuwakamata maofisa ambao wameshindwa kudhibiti vikosi vyao.

No comments: