UZIMAJI MITAMBO YA ANALOJIA KUENDELEA KAMA ILIVYOPANGWA...

Profesa Makame Mbarawa.
Serikali imesisitiza kwamba uzimaji wa mfumo wa analojia kwenda dijitali utaendelea kama kawaida na kusema hakuna visimbuzi vitakavyositishwa wakati kazi hiyo ikiendelea.

Akizungumza jana na mwandishi, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema awamu ya kwanza inayomalizika Aprili 30 kwa kuzima mkoani Mbeya, itafuatiwa na tathmini ya kina kuhusu kazi iliyokwishafanyika huko nyuma.
“Tumeshazima katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Dodoma, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro na sasa tunakwenda Mbeya na baada ya hapo tutafanya tathmini ya changamoto tulizokumbana nazo na kuzifanyia kazi,” alisema Waziri.
Aliongeza kuwa baada ya hapo itafuata miji 14 ambayo hata hivyo hakuitaja lakini akasema kampuni ya Star Media Tanzania Limited kama ilivyoahidi, itakuwa imejenga mitambo katika maeneo hayo.
Lakini akasema katika baadhi ya maeneo ambako hakuna analojia kazi itaendelea bila matatizo kwa kuingia kwenye digitali moja kwa moja.
Aliendelea kuwaomba wadau kutoa ushirikiano kwa Serikali katika utekelezaji wa kazi hii ya kuingia katika mfumo wa ditigali kwani haukwepeki.
Alisema nia ni kuhakikisha kuwa ifikapo Juni 17, 2015 dunia nzima itakapozima mfumo wa analojia  Tanzania iwe imeingia katika mfumo huo wa kisasa.
Hatua hiyo inakuja huku wamiliki wa vituo vya televisheni nchini wakiitaka Serikali iruhusu mifumo ya digitali na analojia iende sambamba kutokana na vituo hivyo kuanza kukosa matangazo kwa kilichodaiwa ni baadhi ya watu kushindwa kumudu gharama za visimbuzi.
Hiyo ilisababisha pia Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuishauri pia Serikali iangalie uwezekano wa kusitisha utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia na kuwasha ya dijitali katika mikoa iliyosalia, ombi ambalo linaonekana kugonga mwamba.

No comments: