TANZANIA YAITAKA MALAWI KUACHA KUTAPATAPA ZIWA NYASA...

Bernard Membe.
Serikali  imeitaka  Malawi  kuacha  kutapatapa kuhusu mgogoro wa mpaka baina ya nchi hizi mbili katika Ziwa Nyasa na imesisitiza kuwa na ushahidi wa kutosha wa uhalali wa  mipaka hiyo hata kama Malawi itawasilisha suala hilo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kama ilivyotishia.

Kauli ya Malawi ya kuwasilisha suala hilo ICJ, ilitolewa hivi karibuni na  Rais  wa nchi hiyo, Joyce Banda.
Akizungumzia msimamo huo wa Serikali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliviambia vyombo vya habari Dar es Salaam jana kuwa Malawi inapaswa kusubiri  uamuzi wa jopo la usuluhishi lifanye kazi na litoe uamuzi.
Katika mkutano huo, Waziri Membe alikanusha madai kuwa Serikali ya Tanzania ilipewa nyaraka za siri na Katibu wa jopo hilo, ambalo linahusisha marais wastaafu wa Afrika na wanasheria kama ilivyodaiwa na Rais Banda.
Rais Banda alikaririwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi hiyo, akimtaja Mtanzania, Dk John Tesha, kuwa ndiye aliyehusika na wizi wa nyaraka hizo za siri.
Waziri Membe alisema Tanzania na jopo hilo wameshtushwa na madai hayo na hatua ya Rais Banda kupoteza imani ya kuendelea na mazungumzo hayo ya kutafuta suluhu, kutokana na madai ambayo hayana ukweli.
Alisema hata kama anayedaiwa kuwa Dk Tesha angewasilisha nyaraka hizo za siri hawezi kuhusika katika suala hilo na kwamba hata marais wastaafu kutoka nchi zenye migogoro ya mipaka, pia hawatahusika katika utoaji uamuzi ili kuondoa uwezekano wa kutokea mgongano wa kimaslahi.
Alisema jopo hilo  linaloongozwa na Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano na marais wastaafu  Festus Mogae wa Botswana na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, ni jopo lenye watu wazoefu, wataalamu na wachapakazi. Pia alisema wapo wanasheria waliobobea katika migogoro kama hiyo.
Alitaja  wanasheria hao kuwa ni Jaji Raymond Ranjeva, Jaji mstaafu wa ICJ, Profesa George Kanyeihamba Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Uganda, Jaji Baney Afako Mshauri wa masuala ya sheria kwenye Umoja wa Afrika (AU) kuhusu mgogoro wa mpaka wa Sudan na Dk Gbanga Oduntun ambaye ni Profesa  wa  Sheria na Mjumbe wa Kamisheni ya mgogoro wa mpaka kati ya Nigeria na Cameroon.
Wanasheria wengine  waliotajwa na Waziri Membe ni Profesa Martin Pratt, Mkurugenzi wa Utafiti wa Jiografia na Mipaka; Dk Dire David Tladi, Mjumbe wa Kamisheni  ya Sheria ya Umoja wa Mataifa (UN) na Miguel Chisano, kiongozi wa Chuo cha Mipaka ya Baharini na Nchi Kavu. 
“Ni watu wenye heshima ya dunia, tusingetarajia Rais Banda  kusema hana imani na jopo hili!” alisema kwa mshangao.
Akizungumzia maafikiano  yaliyofanyika Novemba 17, mwaka jana, Waziri Membe alisema pande zote husika zilikubaliana kuwa chombo hicho kiwe cha mwisho katika kutoa uamuzi na hivyo suala la kwenda ICJ litafanywa baada ya pande hizo kushauriana na Rais Chissano.
Alisema katika kipindi ambacho pande hizo zinasubiri jopo hilo kufanya kazi, Serikali ya Tanzania inaiomba Malawi kutogusa eneo la Ziwa Nyasa hadi uamuzi utakapokuwa umetolewa.
“Tunaiomba serikali ya Malawi irudi katika jopo la usuluhishi na tutashangaa  ikiwa itakwenda kushitaki ICJ   kwa kuwa  ili  iende  huko ni lazima sisi  tukubali. Hata pale tutakaposhauriwa  ni lazima tukubaliane na Malawi.
“Tunaiomba iache kutapatapa; mara Uingereza, Marekani, Jumuia ya Madola na Umoja wa Afrika (AU) na kuona viongozi wa dunia, bali iamini jopo la Rais Chissano. Matokeo ya utafiti wao  upo uwezekano wa kuyakubali au kuyakataa,” alisisitiza Waziri Membe.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja tarehe ambayo jopo hilo litatoa ripoti yake kuhusu mgogoro huo, akisema Tanzania haina haraka juu ya hilo, kwani ina ushahidi wa mahali mipaka baina ya nchi hizo mbili ndani ya Ziwa Nyasa ilipo.
Alisema Tanzania ilipeleka wataalamu Uingereza na Ujerumani kupata uelewa wa kutosha  juu ya jambo hilo, hivyo ina ushahidi wa kutosha.
“Hatuna shaka, tunao ushahidi wa kutosha. Tunachosubiri ni kwa jopo la wataalamu kumaliza kazi na kutoa uamuzi wa uhalali wa mipaka hiyo,” alisema Waziri Membe.
Akihutubia Taifa Septemba mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alisema Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961, mjadala juu ya mpaka huo ulifikishwa bungeni, ambako ilikubaliwa kuwa juhudi zifanyike kuanzisha mjadala wa kumaliza mgogoro huo kwa maslahi ya wananchi wa nchi hizi mbili. 
Alisema Tanzania iliamua kwamba inapaswa isubiri mpaka Malawi ipate uhuru wake ili mazungumzo yafanyike baina ya nchi mbili zilizo huru.
“Lakini kwa bahati mbaya haikuwa hivyo na mambo yakawa magumu na yakajenga mazingira ya uadui. Miaka mitatu baada ya uhuru wa Malawi, Januari 2, 1967, Serikali ya Tanzania iliiandikia barua Malawi kuelezea masuala ya mpaka na kupendekeza nchi zetu mbili zizungumze na kuja na suluhisho,” alisema Rais.
Lakini bahati mbaya tena, Januari 24, 1967, Serikali ya Malawi ikajibu na kukiri kuipokea barua hiyo  na kuahidi kwamba watatoa majibu katika muda mfupi. Hata hivyo, alisema ilipofika Juni 27, 1967, Rais Kamuzu Banda wakati akihutubia Bunge la Malawi, alisema madai ya Tanzania hayakuwa halali na kwamba kihistoria Songea, Njombe na Mbeya zilikuwa sehemu ya Malawi, hivyo, mazungumzo yakasimama.
“Tanzania haikukata tamaa. Bakili Muluzi alipochaguliwa kuiongoza Malawi, juhudi mpya zilichukuliwa lakini hazikuzaa matunda. Juni 9, 2005, Rais wa tatu wa Malawi, Bingu wa Mutharika, ambaye hivi sasa ni marehemu, aliandika barua kwa Rais Benjamin Mkapa akimshauri kwamba nchi zetu hizi zijadiliane kuhusu mpaka wa Ziwa Nyasa,” alisema Rais.
Rais alisema hadi Septemba mwaka jana, mikutano mitatu ya pamoja ilishafanyika, wa kwanza ukifanyika Septemba 8 hadi 10, 2010, wa pili Julai 27 hadi 28, 2012 Dar es Salaam na wa tatu ukifanyika Mzuzu na Lilongwe Agosti 20 hadi 27 mwaka jana.
Alisema hatua kadhaa zimeshachukuliwa kufikia maafikiano, lakini hakuna kilichokwishakubaliwa juu ya madai ya Tanzania ya kutaka mpaka uwe katikati ya Ziwa na msisitizo wa Malawi kwamba mpaka uwe mwambao wa Tanzania.
Chanzo cha mgogoro kati ya nchi hizi mbili ni makubaliano kati ya Uingereza na Ujerumani juu ya mpaka kati ya nchi hizo yaliyofikiwa Julai mosi, 1890. Makubaliano hayo yaliyojulikana kama Mkataba wa Heligoland, yalisainiwa Berlin, Ujerumani, kati ya mataifa hayo mawili ya Ulaya.

No comments: