TANZANIA YAULA MABILIONI MENGINE YA MILLENNIUM CHALLENGE...

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa MCC, Daniel Yoannes (katikati) alipomtembelea Ikulu, Dar es Salaam. Kushoto ni Balozi wa Marekani hapa nchini, Alfonso Lenhardt.
Tanzania, imeshinda kwa mara ya pili katika mchakato wa kupata ufadhili katika miradi ya kukabiliana na umasikini, unatolewa na Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), la Serikali ya Marekani.

Mara ya kwanza Desemba 2005, shirika hilo lilitangaza na kutoa dola za Marekani milioni 698, sawa na zaidi ya Sh bilioni 700, ambazo Serikali ya Tanzania ilizitumia kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara, umeme, viwanja vya ndege na maji.
Tayari Rais Jakaya Kikwete, juzi alipozungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa MCC, Daniel Yoannes, Ikulu Dar es Salaam, alishukuru taifa hilo kubwa na shirika hilo, kwa uamuzi wa kutoa awamu ya pili ya msaada kama huo kwa Tanzania, ambao maandalizi yake yameshaanza.
“Msaada wenu umetuwezesha kufanya mambo makubwa kama kujenga barabara, katika maeneo ambako hakuna mshirika mwingine yoyote wa maendeleo alikuwa tayari kutusaidia, na sisi wenyewe tulikuwa hatujapata uwezo wa kiraslimali wa kujenga barabara hizo.
“Baadhi ya barabara hizo ni kutoka Tunduma hadi Sumbawanga na Namtumbo hadi Songea. Kuna kiongozi wa nchi moja ambaye nilipata kumwomba msaada wa kuijenga barabara hii, akasema kuwa ilikuwa vigumu kwa nchi yake kujenga barabara, kwa kuwa inatoka kusikojulikana kwenda kusikojulikana. Nawashukuru nyie kwa msaada wenu mkubwa,” alisema.
Akizungumza katika ofisi za Ubalozi wa Marekani jana baada ya  kukutana na waandishi wa habari, Yohannes alisema kulikuwa na nchi nyingi zilizowania kufadhiliwa na mfuko huo.
“Ni ngumu mno kupata nafasi, mara nyingi washiriki ni nchi zaidi ya 100 lakini zinazopata ni 25 tu, ni jambo la kujivunia kwa nchi yenu kupata fursa hii,” alisisitiza Yohannes.
Alisema kulikuwa na vigezo zaidi ya 20, vilivyotumika kuwezesha nchi kuchaguliwa kupata nafasi hiyo, vikiwemo vigezo vya utawala bora na udhibiti ya vitendo vya rushwa, na Tanzania imefanikiwa katika maeneo hayo na kuchaguliwa kwa mara nyingine kufadhiliwa na shirika hilo.
Vigezo vingine vinavyotumika kuchagua washindi mbali na utawala bora na udhibiti wa rushwa, ni uchumi huria na uwekezaji katika miradi inayogusa wananchi.
Kwa mujibu wa Yohannes, maeneo yatakayo fadhiliwa na MCC,  yanatokana na mchanganuo ulioainishwa na Serikali ya Tanzania, ambapo katika taarifa za awali, ilipendekeza maeneo ya nishati, usafirishaji na ardhi.
“Namshukuru Rais Jakaya Kikwete na Serikali yake kwa kuwa kiongozi anayejituma, nina wahakikikishia kuwa lengo letu sisi MCC ni kuhakikisha kuwa miradi hii inawanufaisha Watanzania,” alisema.
Kuhusu kiwango cha fedha kitakachotolewa kwa Tanzania katika mradi huo wa MCC awamu ya pili, Yohannes alisema ni mapema mno kuzungumzia, kwani watatumia mchanganuo wa nchi husika na safari hii, shirika hillo litatoa fedha kutokana na namna nchi husika itakavyoeleza jinsi sekta binafsi itakavyoshiriki katika miradi hiyo.
Hata hivyo alibainisha kwamba kwa mwaka huu, shirika hilo linatarajia  kuwekeza katika nchi za Afrika kiasi cha dola za Marekani bilioni 9.3.
Naye Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, alisema Yohannes pia atakwenda Zanzibar na kukutana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Akiwa Zanzibar, kwa kushirikiana na Dk Shin, Yohannes atazindua miradi uliofadhiliwa na MCC, wa kulaza nyaya za kusafirishia umeme chini ya Bahari ya Hindi kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar na Mradi wa Ujenzi wa Barabara Pemba.
Katika mkoa wa Tanga, Rais Kikwete na Yohannes watazindua barabara ya lami ya Tanga mpaka Horohoro, na Dodoma watazindua njia ya kusafirisha umeme na kuusambaza katika wilaya mbali mbali nchini kutokea mkoani humo.

No comments: