ZANZIBAR YAELEMEWA NA ONGEZEKO KUBWA LA WATU...

Baadhi ya wakazi wa Zanzibar wakipata mahitaji yao sokoni.

Kuna kila dalili kuwa maono ya muasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Abeid Amaan Karume, kuwa iko siku kisiwa hicho kitajaa na kulazimika kupata ardhi Tanzania Bara, kuanza kutimia.

Maono hayo yametajwa kuwa miongoni mwa sababu za Karume na Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kuunganisha nchi hizi mbili katika Muungano wa kihistoria uliodumu miaka 49 sasa mbali na sababu ya udugu kati ya watu wa Bara na Visiwani hata kabla ya uhuru.
Mwandishi alipata kumnukuu mmoja wa mawaziri waliokuwapo wakati Muungano unaasisiwa, Hassan Nasoro Moyo, kwamba Mzee Karume, aliwaambia Zanzibar ni kisiwa kidogo na kinaliwa na bahari na Tanzania Bara ni nchi kubwa, hivyo baada ya Muungano, Wazanzibari watapata fursa ya kupata ardhi na kuishi Bara.
Maono hayo ya waasisi wa Muungano wa 1964, yameanza kudhihirishwa na Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, na taarifa za Serikali kuhusu upatikanaji wa maji na kupotea kwa visiwa vidogo.
Ripoti hiyo kuhusu idadi ya watu iliyotolewa wiki iliyopita,  inabainisha kuwa Zanzibar imejaa na sasa wastani wa wananchi wake kwa eneo, umezidi wastani wa kimataifa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya watu visiwani humo ni milioni 1.3 huku mkoa wa Mjini Magharibi, ukiwa na watu 593,678 na msongamano mkubwa wa watu 2,581 kwa kilometa moja ya mraba. Wastani wa idadi ya watu kwa kilometa moja ya mraba nchini Tanzania ni watu 51.
Waziri wa Ardhi, Maji, Makazi na Nishati wa Zanzibar, Ramadhan Abdalla Shaaban aliyehudhuria uzinduzi huo, alizungumzia msongamano huo na kusema itawalazimu Zanzibar kujenga maghorofa, vinginevyo hawatakuwa na maeneo ya kulima. 
Wakati ripoti hiyo ikionesha msongamano wa watu Zanzibar, jana Waziri Shaaban, alisema katika Baraza la Wawakilishi, kwamba kisiwa hicho pia kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji.
Kwa mujibu wa Shaaban, maji yalikuwa yakipatikana lita bilioni tatu na nusu kwa siku miaka mitano iliyopita, lakini sasa maji yanayopatikana ni lita bilioni moja na nusu tu.  
Akitetea hoja za Muswada wa Kuanzishwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Maji (ZURA), kwa lengo la kuimarisha mikakati zaidi, ili huduma hiyo ipatikane kwa ufanisi, Shaaban alisema wanafanya utafiti wa kusarifu maji ya chumvi, kwa ajili ya matumizi ya kunywa majumbani. 
Akifafanua hali hiyo, alisema Zanzibar inakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji safi na salama, kutokana na uvamizi wa vyanzo vya maji na kasi ya ujenzi wa nyumba za kudumu za wananchi.  
Alitaja sababu zaidi za uhaba wa maji,  kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia hivi sasa. 
“Dunia inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya tabia ya nchi ambapo Zanzibar nayo imekumbwa na tatizo hilo,” alisema.
Wakati idadi ya watu ikipunguza maeneo ya kilimo, sambamba na maji safi ya kunywa kupungua, visiwa vidogo Zanzibar pia vinakabiliwa na hatari ya kutoweka kutokana na kumegwa kwa kasi na maji ya bahari yanayoshambulia nchi kavu. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Alhabib Fereji, alithibitisha hilo jana katika Baraza la Wawakilishi, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mtambwe, Salum Abdalla Hamad (CUF). 
Hamad katika swali lake, alitaka kujua mikakati ya kukabiliana na athari za mazingira, ikiwamo kukabiliana na hatari inayokumba kisiwa cha Mtambwe Mkuu, kinachovamiwa na maji ya bahari. 
Akifafanua, Fereji alisema kisiwa hicho kinakabiliwa na tatizo la maji ya bahari kuvamia maeneo ya makazi ya wananchi, kutokana na wananchi kukata miti aina ya mikoko, kwa matumizi ya ujenzi wa nyumba za kuishi. 
“Napenda kusema kwamba nilipata nafasi ya kutembelea eneo la kisiwa hicho na kujionea athari za kimazingira, ambapo ni kweli maji ya baharini yanavamia maeneo ya makazi ya wananchi kwa kasi kubwa,” alisema. 
Fereji alisema pia uvamizi wa maji ya bahari, umeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kilimo katika baadhi ya vijiji Pemba. 
Alisema Serikali imechukua hatua za awali, ikiwamo kutoa ushauri wa kupandwa mikoko, pembeni mwa bahari ambayo hutumika kuzuia kasi ya nchi kavu kumegwa na bahari. 
Mbali na kutoa ushauri, pia Serikali imetafuta mshauri mwelekezi, kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina ya athari za mazingira, zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. 
Fereji alisema kazi ya mshauri mwelekezi, ni kuangalia maeneo ya athari za mazingira, ikiwamo visiwa vidogo, ambavyo vinakaliwa na wananchi kikiwamo cha Pemba. 

No comments: