RATIBA YA MAZIKO YA BILIONEA WA ARUSHA YATOLEWA...

Nyaga Mawalla.
Ratiba ya maziko ya Wakili Nyaga Mawalla ilitolewa jana, ambapo misa ya kuaga mwili wa marehemu, inatarajiwa kufanyika kesho katika Kanisa la Uhuru Highway Lutheran Church, lililopo Nairobi nchini Kenya.

Taarifa fupi iliyotolewa kwa vyombo vya habari na   Kampuni ya Mawalla Advocates, ilieleza kuwa ibada hiyo inatarajiwa kuanzia saa 3 asubuhi na kufuatiwa na   maziko katika makaburi ya karibu na kanisa hilo kuanzia saa 5 asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, iliyosainiwa na Joseph Nuwamanya, baada ya maziko hayo, ibada nyingine ya kumuombea Wakili Nyaga ambaye anatajwa kuwa bilionea kijana, itafanyika keshokutwa kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana nyumbani kwa baba yake mzazi eneo la Nkomo YMCA, Moshi mkoani Kilimanjaro.
Hata hivyo, Nuwamanya katika taarifa hiyo, alikanusha  madai kwamba wakili huyo alijirusha ghorofani huko Kenya, alipokuwa akipatiwa matibabu, na kutaka vyombo vya habari kusubiri uchunguzi wa Polisi nchini humo, kuhusu chanzo cha kifo hicho.
“Tunatambua kwamba kumekuwa na hisia au maelezo tofauti tofauti ya kupotosha kuhusu kifo cha mpendwa wetu Mawalla kwenye vyombo vya habari na mitandao mbalimbali ya kijamii nchini.
Tungependa kuchukua nafasi hii kukanusha na kueleza kusikitishwa kwetu kwa habari hizo, ambazo hazina ukweli wowote. Taarifa rasmi ya sababu za kifo cha Mawalla bado haijatolewa na uongozi wa Hospitali ya Nairobi, kutokana na kutokukamilika kwa uchunguzi unaoendelea,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilivitaka vyombo vya habari na jamii, kuepuka kutoa habari ambazo sio sahihi na zisizo na ukweli wowote, kuhusu kifo na maisha yake.
“Ni vyema kushirikiana na familia pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu katika kipindi hiki kigumu kwa kumuenzi na kutafakari yale mema na mazuri mengi aliyoyafanya hapa duniani enzi za uhai wake.
Kwa upande wetu ni kipindi kigumu tunachokipitia baada ya kumpoteza mpendwa wetu Mawalla ambaye kwetu sisi na wengine wengi alikuwa ni kiongozi, baba, kaka na rafiki. Ni mtu ambaye ameacha pengo kubwa katika maisha ya kila mmoja wetu ambalo halitozibika,” ilieleza taarifa hiyo.
Kabla ya kutolewa kwa taarifa hiyo, kifo cha Mawalla kiliamsha vuta nikuvute baada ya kuibuka kwa mgogoro wa kifamilia, kuhusu mahali pa kuzikwa.
Katika mgogoro huo, mama wa marehemu ambaye jina lake halijafahamika, alitaka mwanawe azikwe Marangu Moshi, huku kukiwa na taarifa kwamba mwenyewe alielekeza azikwe katika shamba lake kubwa, lenye mandhari ya hali ya juu, lililopo Momela wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Baba yake, Juma Mawalla, ambaye ni Wakili wa siku nyingi, naye alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa hatohudhuria mazishi ya mwanawe, iwapo atazikwa eneo tofauti na Marangu.
Hata hivyo, wakati mgogoro huo ukiendelea,  Wakili wa marehemu, Fatuma Karume alitoa wosia wake, ambao alielekeza azikwe Kenya.
Katika wosia huo, Mawalla anatajwa alielekeza katika wosia huo maeneo mawili ya kuzikwa, kulingana na mazingira ya kifo chake.
Kwanza, alielekeza kwamba siku akifia Tanzania, azikwe katika shamba hilo lililopo Momela wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Pili, alielekeza katika wosia huo wa kisheria, kwamba akifa nje ya nchi,  maziko yake yafanyike katika nchi hiyo hiyo.

No comments: