MWANAMKE AFUKIWA NA KIFUSI CHA JENGO MASAA 36 NA KUTOKA AKIWA HAI...

Wafanyakazi wa ukoaji baada ya kumnasua mwanamke huyo kutoka kwenye kifusi.
Mwanamke mmoja aliyejeruhiwa amelazimika kunyofolewa akiwa hai kutoka kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka baada ya kukaa kwa masaa 36 chini ya kifusi hicho.

Mwanamke huyo aliburutwa kutoka kwenye jengo hilo baada ya wafanyakazi wa uokoaji kusikia sauti yake na kutumia kamera kuweza kujua eneo aliko chini ya kifusi hicho.
Wafanyakazi wa uokoaji wamekuwa wakiwasaka walionusurika kifo tangu kuporomoka kwa jengo hilo lenye ghorofa saba Alhamisi jioni karibu na jiji la India la Mumbai.
Takribani watoto 19 ni miongoni mwa watu 72 waliothibitishwa kuwa wamekufa kufuatia kuanguka huko kwa jengo hilo.
Wafanyakazi wa uokoaji wakitumia magreda waliendelea na msako katikati ya vyuma na zege baada ya jengo hilo la ghorofa saba kuporomoka 'mithili ya  karata zilizopangwa' Alhamisi jioni, maofisa na mashuhuda walisema.
Uhaba wa makazi nafuu katika nchi hiyo ya tatu kwa uchumi imara barani Asia umechochea ongezeko la ujenzi wa kinyume cha sheria na wajenzi ambao wanatumia nyenzo duni na njia za mkato ili kufanikisha makazi nafuu kwa wafanyakazi wa kipato cha chini.
"Jengo hilo lilianguka mithili ya karata ndani ya sekunde tatu au nne," alisema Ramlal, mkazi wa eneo hilo.
"Lilitikisika kidogo na kuporomoka," alisema.
Wakazi walisema vibarua wanaolipa kodi ya pango takribani Dola za Marekani 5 kwa siku walikuwa wakiishi kwenye jengo hilo.
Jengo hilo, ambalo lilikuwa katika eneo la bustani katika jiji la Thane, lilijengwa kwa kutumia nyenzo duni na bila uthibitisho rasmi, alisema Sandeep Malvi, msemaji wa mamlaka za utoaji leseni katika Shirika la Manispaa ya Thane.
Alisema watu 72 wamekufa na 36 kujeruhiwa na kwamba wamelazwa kwenye hospitali kadhaa za mjini humo.
"Kuna uwezekano wa kuwapo miili zaidi ndani," aliongezea Malvi.
"Zoezi la uokoaji bado linaendelea."
Mtoto mchanga wa miezi 10 alinyofolewa kutoka kwenye kifusi hicho Ijumaa.
Kamishna Msaidizi wa Manispaa katika eneo hilo amesimamishwa kazi kufuatia kuporomoka huko kwa jengo, ambalo waziri wa mambo ya ndani alisema ilisababishwa na jengo hilo kujengwa kinyume cha sheria, viliripoti vyombo vya habari vya mjini humo.
Polisi wanawasaka wajenzi hao na watawashitaki kwa kusababisha mauaji kuhusiana na ajali hiyo.
Mnamo mwaka 2012, uhaba wa makazi nchini India ulikadiriwa kukaribia nyumba milioni 19, kwa mujibu wa ripoti kutoka Wizara ya Nyumba na Upunguzaji Umasikini Mjini.
Ofisa wa juu wa zamani Mumbai, G.R. Khairnar, alisema maofisa wa serikali walioruhusu ujenzi huo haramu wanatakiwa kukamatwa sambamba na wajenzi hao.
Katika moja ya ajali mbaya zaidi hivi karibuni za kuporomoka jengo, karibu watu 70 waliuawa Novemba 2010 pale jengo la makazi katika eneo lenye msongamano New Delhi lililopoanguka. Jengo hilo lilikuwa na ghorofa mbili zaidi ya inavyoruhusiwa kisheria na msingi wake unaelekea kuwa ulidhoofishwa na uharibifu wa maji.

No comments: