BAYERN MUNICH YAWA TIMU YA KWANZA KUTWAA UBINGWA ULAYA MSIMU HUU...

Wachezaji wa Bayern Munich wakishangilia moja ya mabao yao.
Timu ya soka ya Bayern Munich imeweka rekodi kwa kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa katika ligi za barani Ulaya msimu huu.

Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Eintracht Frankfurt jana lililowekwa kimiani na Bastian Schweinsteiger katika dakika ya 52 uliwahakikishia miamba hao wa Ujerumani ubingwa mechi sita kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo.
Bayern Munich imetwaa taji hilo ikiwa na rekodi ya kushinda mechi 24, kutoka sare 1 na kupoteza 3, huku ikiwa mbele kwa tofauti ya pointi 20 dhidi ya Borussia Dortmund iliyo katika nafasi ya pili, ambayo iliifunga Augsburg mabao 4-2. Dortmund imeshinda ubingwa wa Bundesliga miaka miwili mfululizo iliyopita.
Bayern Munich imeweka rekodi kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo mara 23. Hakuna timu yeyote nyingine iliyoweza kutwaa ubingwa huo zaidi ya mara 10. Imejikusanyia pointi 75, sita zaidi za rekodi ya Bundesliga iliyowekwa na Dortmund msimu uliopita.
"Safi sana. Zaidi ya yote, ninafurahia wachezaji wangu, ambao wamefanya kazi kubwa nzuri kwa msimu mzima," alisema kocha wa Bayern Jupp Heynckes, ambaye nafasi yake itachukuliwa na Pep Guardiola kwa ajili ya msimu ujao.

No comments: