MKE WA RAIS KIKWETE ASOMESHA 'YATIMA FEKI'...

Mama Salma Kikwete.
Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete amefichua kuwa, amewahi kupelekewa yatima `feki’ katika shule anayoisimamia ya Wama Nakayama iliyopo Rufiji mkoani Pwani, ambayo ni maalumu kwa watoto yatima na waliotoka katika mazingira magumu.

Kutokana na mazingira hayo, amezitaka taasisi zinazosaidia watoto kielimu kuwa makini kwani zinaweza kujikuta zikisaidia wasiostahili, huku wenye kustahili msaada huo wakiachwa.
Alisema hayo jana Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 10 ya Fao la Elimu linalotolewa na Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) yaliyokwenda sambamba na kukabidhi zawadi  kwa watoto waliofanya vizuri katika mitihani yao naambao walisomeshwa na PPF baada ya wazazi wao kufariki dunia.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa shule kuisaidia PPF kuhakikisha inatoa fedha kwa watoto halisi wa marehemu na kuwataka kuwa makini, la sivyo walengwa ambao ni watoto wa marehemu watakuwa hawafikiwi na msaada huo, jambo ambalo litakwamisha malengo ya mfuko huo.
“Mimi nina shule ya Wama Nakayama ambayo iko Rufiji ambapo lengo la kuianzisha ni ili kuwafikia watoto yatima na walio katika mazingira magumu ambapo tuliletewa watoto ambao si walengwa kama ambavyo mfuko ulilenga kuwasaidia,” alisema Mama Kikwete wakati akijibu moja ya changamoto za PPF katika kutekeleza azma ya mfuko.
Alisema suala hilo linaumiza sana kwa sababu lengo ni kuwafikia walio na matatizo, lakini mwisho wa siku unajikuta mwenye fursa ya kusoma anaipata na asiyekuwa na fursa hiyo anaikosa kutokana na uzembe wa baadhi ya viongozi katika kujipa wao fursa wao wenyewe.
Na ili kuepuka kupokea wanafunzi 'mamluki’, amewataka walimu kujitahidi kufikisha taarifa sahihi za wanafunzi kwa mfuko huo ili PPF iweze kujitathmini pamoja na kufuatilia taarifa za wanafunzi wanaowasomesha.
Pamoja na hilo, ameitaka PPF iangalie uwezekano wa kuwasomesha watoto hao zaidi hadi Kidato cha Sita.
Katika hatua nyingine, alisema si wasimamizi wote wa mirathi ama ndugu ambao huwa waadilifu, kwani baadhi yao hujinufaisha kwa mali za marehemu, huku wakiwasambaratisha watoto, kuwasahau na kuwatelekeza kabisa.
Alisema wengine hufikia hata hatua ya kutawanya ama kujitwalia mali iliyoachwa na marehemu huku wakiwaacha watoto wa marehemu wakihangaika na maisha na kuwa na mzigo mzito wa maisha, ambapo ubunifu wa PPF kuwasomesha watoto wa wanachama wao ni mzuri na unaostahili kuigwa.
Kadhalika, aliwataka wazazi kutokuwa na tabia ya kuwagawa watoto kwa kupendelea wale waliowazaa peke yao huku wakisahau watoto wa ndugu ama jamaa wanaowalea baada ya wazazi wao kufariki, kwani katika maisha hawawezi kujua atakaowasaidia ni nani.
“Utakuta katika familia baba ama mama kuna watoto wa ndugu wa mmoja wao, lakini kila wanaponunua kitu kizuri ama kuwa na vipaumbele fulani huanzia kwanza kwa watoto wao huku wakiwanyanyasa ama kuwatenga watoto walio wa ndugu, ilhali wakijua kuwa wazazi wao walishafariki na hawana msaada,” alisema Mama Kikwete.
Alisema mwanaume anapooa na kumkuta mkewe alikuwa na mtoto kabla ya ndoa, huyo naye ampende kama mmojawapo wa watoto wa familia na kuacha tabia ya kubagua.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya PPF, Profesa Adolf Nkenda alisema changamoto kubwa inayoukabili mfuko, hasa katika Fao la Elimu ni kupata tabu juu ya ukweli wa watoto ambao wanasomeshwa na PPF kama ndio halisi wa marehemu na pia ndugu kuchelewa kutuma taarifa za kifo cha mwanachama, jambo ambalo linaweza kumcheleweshea mtoto haki yake ya kuendelea na masomo.
Alisema Fao la Elimu linasomesha watoto wanne wa mwanachama aliyefariki akiwa kazini na baada ya kuchangia mfuko huo kwa miaka mitatu ambapo humsomesha mtoto kwa kumlipia karo pamoja na mahitaji mengine kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha nne.

No comments: