MIKONGO YA MAWASILIANO ILIYOKATIKA KUKAMILIKA APRILI 15...

Wataalamu wakishughulika uunganishaji wa mkongo wa mawasiliano chini ya bahari.
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imesema hadi Aprili 15 matengenezo ya mikongo miwili ya mawasiliano ya Easy na Seacom itakamilika na kuwezesha huduma kurudi kwa asilimia 100.

Aidha, imesema kwa sasa, huduma inapatikana kwa kiasi kikubwa lakini inatokana na njia mbadala ambazo zinaelezwa huenda zikaendelea kutumika hata baada ya mikongo hiyo kukamilika, ili kuepusha madhara yaliyotokea hivi karibuni nchini na mataifa mengine.
Mikongo hiyo ya baharini ilikatika wiki mbili zilizopita na kusababisha athari kubwa za mtandao. Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura, mkongo wa Easy ulikatika Misri, kilometa 17 na 19 katika bahari ya Mediterranean huku wa Seacom ukikatika Marseille, Ufaransa.
Akifafanua kuhusu maendeleo ya mazungumzo yaliyokuwa yakifanywa baina ya TTCL na kampuni ya Telcom ya Afrika Kusini na taarifa kutoka kwa mkongo wa Seacom kuhusu matengenezo, Mkuu wa Mauzo wa TTCL, Kisamba Tambwe alisema hadi Aprili 15 mikongo hiyo itakamilika.
Hilo la Aprili 15 lilielezwa pia na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Peter Ngota alipozungumza na waandishi wa habari jana, katika uzinduzi wa huduma mbili mpya za TTCL; ya kampeni ya Basti na huduma ya Bando na TTCL.
“Sisi TTCL ni wateja wa Seacom na wabia wa Easy, kilichofanyika kwa sasa ni kututafutia njia mbadala wakati matengenezo yakiendelea, kwa mfano Easy wametusogeza njia ya Afrika Kusini ili Telecom itufikishe Ulaya, mazungumzo yanaendelea Ijumaa hii tunakutana tena,” alisema Tambwe.
Kwa upande wa Seacom, alisema wamewatafutia njia mbadala ya Kusini kati ya mbili zinazotumika ambazo ni Kaskazini na Kusini na kuwezesha huduma kuendelea kwa kiwango kilichopo na kueleza kuwa wameelezwa hadi Aprili 15 sehemu iliyokatika ya mkongo itakuwa imetengenezwa.
Kwa mujibu wa Ngota, zaidi ya mikongo mitano ilikatika katika mataifa kadhaa inakopita kuelekea Ulaya yaliko mawasiliano na hivyo madhara yalipata watu wa mataifa hayo ya India, Uarabuni, Misri, Msumbiji, Kenya, Tanzania na kwingineko.

No comments: