Marehemu Jaji mstaafu Ernest Mwipopo. |
Jaji mstaafu Ernest Mwipopo (63) ambaye pia ni mmoja wa wajumbe wa Tume ya kurekebisha sheria, amekufa katika ajali ya gari iliyotokea jana mchana kijijini Mkata, Kata ya Doma, wilayani Mvomero katika barabara kuu ya Iringa-Morogoro.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema ajali hiyo iliyohusisha gari lenye namba za usajili T 691 AUL aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Chafasi Mgohamwende (38) mkazi wa Kawe, Jijini Dar es Salaam.
Kamanda alisema kwamba gari hili lilipofika maeneo ya Mkata matairi yote mawili ya mbele yalipasuka, kuacha njia na kupinduka. Jaji huyo alikuwa akitokea wilayani Mafinga, Iringa akielekea Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi Mkoa wa Morogoro, katika ajali hiyo watu watatu walijeruhiwa, wakiwemo wanawake wawili na mtoto mmoja, sambamba na dereva wa gari hilo na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Hata hivyo, alisema mwili wa Jaji huyo umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ukisubiri taratibu nyingine.
No comments:
Post a Comment