MATUMAINI YA KUSITISHWA NAULI MPYA SASA YATOWEKA...

Dk Harrison Mwakyembe.
Matumaini ya abiria watumiao vyombo vya moto kusafiri nchi kavu ya kupunguzwa nauli yametoweka, baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kubariki ongezeko.

Kwa maana hiyo, nauli hizo za daladala, treni na mabasi yaendayo mikoani zitaendelea kama zilivyotangazwa hivi karibuni na Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Waziri Mwakyembe alisema Serikali imejiridhisha, kwamba taratibu zote za upandishaji viwango hivyo vipya vya nauli, zilizingatiwa.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, kabla ya kuridhia nauli hizo, Serikali iliihoji Sumatra na Baraza la Watumiaji Huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka hiyo.
Alisema walibaini wadau walipitia maombi ya upandishaji nauli, ambayo yalikuwa kutoka Sh 300 hadi Sh 872 kwa nauli za daladala kwa njia yenye urefu wa kilometa 15 sawa na Sh 58.13 kwa abiria kwa kila kilometa.
Wadau waliotoa maoni hayo kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, ni Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), vyama vya madereva, vyama vya kutetea abiria, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.
“Wawakilishi wote wa abiria waliambiwa kama ongezeko hilo dogo la Sh 100 hawaridhiki nalo, sheria inaruhusu kukata rufani katika Baraza la Ushindani, lakini hakuna aliyefanya hivyo kama kawaida ya Watanzania tumezoea kulalama nje ya utaratibu.
“Mimi kama Waziri wa Uchukuzi, sina tatizo na ongezeko hili dogo la nauli za daladala, tatizo langu ni tabia ya Watanzania kukacha vikao halali vinavyojadili mambo yanayotuhusu na kulalamika baadaye,”  alisema.
Dk Mwakyembe alisema baada ya majadiliano kati ya Serikali na Sumatra, walikubali nauli hiyo iongezwe kwa Sh 100 tu kwa watu wazima, na Sh 50 kwa wanafunzi, ili kugawana maumivu ya gharama za uendeshaji kwa watoa huduma.
Alisema ni kweli gharama za uendeshaji kwa wenye mabasi zimeongezeka, ikiwamo bei ya mafuta na vifaa mbalimbali, ikiwamo bei za matairi, hivyo Serikali imeona wananchi na wenye vyombo vya usafiri wagawane gharama hizo.
Kabla ya mabadiliko hayo, kwa mujibu wa tangazo la Sumatra la kupandisha nauli, wanafunzi wa shule ambao hutakiwa kuonesha vitambulisho wanaposafiri, nauli yao ilitakiwa kupanda kutoka Sh 150 hadi Sh 200 kwa safari ya umbali wowote ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa watu wazima, nauli ilikuwa tofauti ambapo ilitakiwa kupanda kwa kilometa na si kwa Sh 100, kama ilivyotangazwa na Dk Mwakyembe, katika marekebisho yaliyotokana na kikao chake na Sumatra.
Kwa tangazo la Sumatra, nauli kwa watu wazima kwa umbali wa kilometa sifuri hadi 10, ilipaswa kuwa Sh 400 na mfano wa njia ya umbali huo, ilikuwa Kivukoni-Ubungo.
Kwa umbali wa kilometa 11 hadi 15, nauli ilipaswa kuwa Sh 450 na mfano wa njia hiyo ilikuwa Mwenge-Temeke.
Kwa njia za kilometa 16 hadi 20, nauli ilipaswa kuwa Sh 500 na mfano wa njia hiyo ilikuwa Tabata Chang’ombe-Kivukoni na kwa kilometa 21 hadi 25, nauli ilipaswa kuwa Sh 600 na mfano ilikuwa kutoka Pugu Kajiungeni-Kariakoo.
Nauli ya juu kabisa Dar es Salaam, ilipaswa kuwa Sh 750 kwa njia za umbali wa kilometa 26 hadi 30 na mfano wake ni njia ya Kibamba-Kariakoo.
Dk Mwakyembe pia aliunga mkono ongezeko la nauli katika usafiri wa reli na mabasi yaendayo mikoani.
“Natoa onyo kwa watoa huduma za usafiri kuheshimu sheria,  najua wataendelea na nauli wanazozijua nje ya nyongeza hii, nawaagiza Sumatra kuendesha kampeni nchi nzima kubaini wanaotoza nauli kubwa kuliko iliyopendekezwa,” alisema Dk Mwakyembe.
Nauli mpya za mikoani kuanzia leo zitaongezeka kwa asilimia 20.3 kwa mabasi ya kawaida, asilimia 16.9 kwa mabasi ya daraja la kati na asilimia 13.2 kwa mabasi ya daraja la juu.
Kutokana na hatua hiyo, kwa basi la kawaida kwa njia ya lami kwa kilometa moja, nauli itakuwa Sh 36.89 badala ya Sh 30.67 na kwa njia ya vumbi, nauli itakuwa Sh 46.11 kwa kilometa badala ya Sh 37.72.
Kwa basi la hadhi ya kati bila kujali katika lami au vumbi, nauli itakuwa Sh 53.22 kwa kilometa badala ya Sh 45.53. Kwa wanaopenda kusafiri na basi la hadhi ya juu pia bila kujali ni katika lami au vumbi, nauli  itakuwa Sh 58.47, kwa kilometa badala ya Sh 51.64.
Ili kubaini daraja la basi husika na kulipa nauli kuendana na gharama, Sumatra iliahidi kuanza na Tanga, ambapo mabasi yatawekwa vibao vyenye rangi kuonesha basi la daraja la juu litakalokuwa na rangi nyekundu, la kati bluu na la kawaida nyeupe.
Kwa upande wa mabasi ya njia ndefu, ili  viwango vipya vya nauli viendane na ubora wa huduma, Sumatra iliagiza wamiliki wa mabasi ya masafa marefu kutotumia wapiga debe kuuza tiketi, bali ziuzwe kwenye ofisi au ndani ya mabasi kwa walio njiani.
Viwango vipya vya nauli za usafiri wa reli kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma kwa daraja la kwanza, ni Sh 75,700 badala ya Sh 60,599.
Dar es Salaam-Mwanza Sh 74,800 badala ya 59,818, Dar-Tabora,  Sh 54,800 badala ya Sh 43,859 na Dar-Dodoma Sh 34,700 badala ya Sh 27,788.
Kwa daraja la pili, Dar-Kigoma Sh 55,400 badala ya Sh 44,305, Dar-Mwanza Sh 54,700 badala ya Sh 43,747, Dar-Tabora Sh 40,500 badala ya Sh 32,364 na Dar-Dodoma ni Sh 26,400 badala ya Sh 21,092.
Kwa daraja la tatu; Dar-Kigoma ni Sh  27,500 badala ya Sh 19,084, Dar-Mwanza Sh 27,200 badala ya Sh 18,860, Dar-Tabora ni Sh 20,400 badala ya Sh 14,173 na Dar-Dodoma ni Sh 13,500 badala ya Sh  9,374.
Kutokana na ongezeko hilo, Shirika la Reli Tanzania (TRL), walielekezwa kutumia mfumo wa utunzaji taarifa za abiria, ambapo walipewa mwaka mmoja kukamilisha uanzishwaji wa matumizi ya mfumo huo.
Pia walitakiwa kuboresha mfumo wa kudhibiti mapato ya shirika, ili kuzuia uvujaji wa makusanyo ya fedha katika vituo ndani ya mabehewa, ambapo walitakiwa kutekeleza kwa miezi mitatu.
Pamoja na kuboresha huduma ya usafirishaji abiria, pia walitakiwa  kuhakikisha kuna mabehewa yenye huduma muhimu kama taa, maji safi, huduma za chakula na kuwa na vyoo bora na safi na abiria wakikata tiketi na kupakia, waoneshe vitambulisho.

No comments: