Madaktari wakiwa katika moja ya mikutano yao wakati wa mgomo wao. |
Madaktari 20 walioshiriki mgomo mwaka jana na kufutiwa usajili, kutokana na agizo la Baraza la Madaktari Tanganyika, wameanza kujitetea, lakini kupitia Chama cha Madaktari nchini (MAT).
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari wiki iliyopita na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dk Donan Mbando ilieleza kuwa madaktari hao wamefutiwa usajili, baada ya kushindwa kuitika mwito wa kwenda kujibu tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.
Kutokana na hatua hiyo ya Baraza, madaktari hao waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo baada ya kusomea taaluma yao kwa miaka mitano, hawaruhusiwi kufanya kazi ya udaktari popote nchini.
Kwa mujibu wa Baraza hilo, madaktari waliofutiwa usajili kuanzia Aprili 12, mwaka huu ni Lilian Komba, Emmanuel Luchagula, Nerbert Benjamin, Ahmed Kombo, Moses Karashani, Deo Mwanakulya, Lucy Laurent, Elias Paschal, Ahmed Ahmed na Malaja Ng’wigulu.
Wengine ni Malaba Raphael, Biswaro Malima, Said Ibrahim, Peter Kyabaroti, Mamelita Basike, Veronica Lyandala, Meshack ole Sabaya, Musyangi Tekele, Kasirye Collins na Baraka Yessaya.
Akizungumza na mwandishi mwishoni mwa wiki, Makamu wa Rais wa MAT, Dk Primus Saidia alisema baadhi ya madaktari hao, walikuwa nje ya nchi na wengi hawakuwa na taarifa.
“Unajua wengi hawakujua wataitwa lini na nini kitaendelea. Walienda nje ya nchi kusoma huku wengine wakijiunga na taasisi nyingine kufanya kazi, lakini pia hawakupata taarifa ya kuitwa kuhojiwa,” alisema.
Alisisitiza kuwa wanamalizia kazi ya kuwatafuta wote waliofutiwa usajili, na kuzungumza nao kuhusu sababu za kutohudhuria katika Baraza kujibu tuhuma zilizokuwa zikiwakabili, na baadaye watatoa uamuzi katika kikao kitakachofanyika wiki hii.
“Suala la kutangazwa kuwa umefutiwa usajili bila kupewa nafasi ni kunyanyaswa, hivyo tunasikiliza malalamiko ya madaktari hao, ili tufanye uamuzi,” alisema Dk Saidia.
Mtoa habari aliye karibu na madaktari hao, alilieleza gazeti hili kwamba baada ya kusimamishwa kazi, baadhi yao waliomba kujiendeleza kimasomo nje ya nchi.
“Wakati ule hakukuwa na kinachoendelea, baada ya kutoka nafasi (za kusoma nje ya nchi), waliamua kujaza fomu za maombi na walipopata nafasi, wakaenda kuanza masomo Septemba mwaka jana huku Baraza likianza kuhoji madaktari Desemba,” alisema mtoa habari wetu.
Kwa mujibu wa madai ya mtoa habari huyo, madaktari hao wanasoma kwa ufadhili wa nchi rafiki na Tanzania na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na balozi zilizoko katika nchi hizo zina taarifa.
Alidai wanafunzi hao wanasoma China, Ukraine na Urusi na kusisitiza kwamba waliomba kusoma Juni mwaka jana na kuondoka nchini Septemba kwa ufadhili wa nchi husika.
Inadaiwa mmoja kati ya madaktari hao alirejea nchini kwa matatizo ya kifamilia na kwenda wizarani kupata ufafanuzi, kuwa yuko nchini China akisoma na hakuhojiwa, lakini wizara ilimtoa wasiwasi na kumtaka akimaliza masomo, aripoti tu wizarani.
Mwenyekiti wa Baraza, Mbando alipotafutwa kujibu madai hayo, simu yake ilikuwa ikiita bila majibu. Pia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi simu yake haikupatikana.
Kiini cha mgomo huo, kilikuwa maslahi makubwa waliyoyadai, ambayo Serikali ilieleza kuwa haina uwezo wa kuwalipa. Madaktari hao walitaka walipwe mshahara wa Sh milioni 3.5 kwa mwezi kwa daktari anayeanza kazi kutoka chuoni.
Pia, walitaka posho za kila mwezi ikiwamo asilimia 10 ya mshahara huo kwa ajili ya posho ya kuitwa kazini, ambayo ni Sh 350,000 na asilimia 30 ya mshahara huo iwe posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi, ambayo ni Sh 1,050,000.
Posho nyingine walizodai katika mlolongo huo wa maslahi ni kupewa posho ya nyumba daraja A au asilimia 30 ya mshahara iwe posho ya makazi ambayo ni Sh 1,050,000 na posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu ambayo ni asilimia 40 ya mshahara huo sawa na Sh milioni 1.4.
Madaktari hao pia walitaka posho ya usafiri asilimia 10 ya mshahara huo sawa na Sh 350,000 ambapo posho na mshahara kwa pamoja kwa mujibu wa madai hayo, daktari anayeanza kazi katika kima cha chini, alipaswa kulipwa Sh milioni 7.7 kwa mwezi.
Madai mengine ambayo hawakuyaweka katika kiwango cha fedha ni pamoja na kupewa kadi ya kijani ya Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Serikali ilikubali suala la usafiri na kuwataka madaktari watumie fursa ya utaratibu uliopo ili wakopeshwe magari, pikipiki, samani na matengenezo ya magari.
Pia, ilikubalika kwamba utekelezaji utaanza kwa kuwapa madaktari kadi ya kijani ya NHIF na katika hatua za kinidhamu, dhidi ya watendaji wakuu wa Wizara, uongozi wa juu wa wizara ulibadilishwa na sasa kuna uongozi mpya.
Hata hivyo, pamoja na Serikali kubadilisha uongozi huo, Waziri mpya wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Mwinyi alipowataka madaktari hao waonane kuzungumzia hoja zao, walikataa kumwona kwa madai kuwa hawaoni sababu kwa vile wamezungumza na Kamati yake kwa miezi mitatu bila mafanikio.
No comments:
Post a Comment