KUMBUKUMBU YA MIAKA 41 YA KIFO CHA MZEE ABEID KARUME YAFANA...

Baadhi ya viongozi wakishiriki dua wakati wa maadhimisho ya miaka 41 ya kifo cha Mzee Abeid Karume. Kutoka kulia ni Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Seif Ali Iddi.
Rais Jakaya Kikwete, jana  aliungana na wananchi wa Zanzibar, kushiriki katika dua na kumbukumbu ya miaka 41, tangu kuuawa kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya  1964 na  Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amaan Karume.

Rais Kikwete ambaye alifuatana na Mama Salma na Rais  mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliwasili kwenye Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar  saa 4:15 asubuhi, tayari kwa shughuli hiyo ya kumbukumbu ya kiongozi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar.
Katika ofisi hiyo, Rais Kikwete alijumuika pamoja na viongozi wengine wakuu, akiwemo Makamu wa Rais   Dk Mohamed Gharib Bilal na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Iddi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amaan Abeid Karume ambaye ni mtoto wa kwanza wa Hayati Karume.
Baada ya dua na mawaidha, viongozi hao walitembelea kaburi la Mzee Karume, ambalo liko kwenye bustani pembeni mwa ofisi hiyo ya CCM Kisiwandui.
Baadaye waliweka mashada ya maua kwenye kaburi kama kitendo cha kumbukumbu ya kifo cha Mzee Karume.
Miongoni mwa walioweka maua kwenye kaburi ya Mzee huyo, ni Rais Kikwete, Rais Shein, mwakilishi wa mabalozi wadogo wanaoziwakilisha nchi zao Zanzibar na  mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini.
Wengine ni mwakilishi wa familia ya Mzee Karume, mwakilishi wa wazee ambao Mzee Karume alishirikiana nao katika Mapinduzi ya Zanzibar, na mjukuu mmoja wa kiongozi huyo.
Aidha, viongozi wa dini mbalimbali nchini, wakiwemo Waislamu na Wakristo, waliomba dua na kutoa sala za kumwombea kwa Mwenyezi Mungu, aendelee kuiweka pema peponi roho ya marehemu.
Mzee Karume ambaye aliongoza kwa mafanikio makubwa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Januari 12, mwaka 1964, aliuawa kwa kupigwa risasi na wapinga Mapinduzi jioni ya Aprili 7, mwaka 1972, wakati alipokuwa akizungumza kwa faragha na kucheza zumna na wazee wenzake kwenye ofisi hiyo hiyo ya Kisiwandui.
Rais Kikwete aliondoka Kisiwandui kurudi Uwanja wa ndege wa Zanzibar moja kwa moja baada ya shughuli hiyo kwa safari ya kurejea Dar es Salaam.

No comments: