IDADI YA WALIOKUFA JENGO LILILOPOROMOKA YAONGEZEKA, SASA NI 30...

Waokoaji wakinasua moja ya miili iliyopatikana jana jioni kwenye kifusi cha jengo hilo.
Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ajali ya kuanguka ghorofa jijini Dar es Salaam imefikia 30 baada ya miili mingine mitatu kuokolewa kwenye kifusi cha jengo hilo usiku wa kuamkia jana.

Aidha majengo matatu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) yaliyokuwa karibu na ghorofa lililobomoka, yatakuwa chini ya uangalizi kubaini kama yatafaa watu kuishi au yabomolewe na kujengwa upya.
Akizungumza jana, Mkuu  wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema NHC itagharimia sanda, jeneza na kusafirisha miili ya watu waliokufa kwenye janga hilo.
Akizungumzia majengo hayo matatu yanayodaiwa kuwa hatarini, alisema, “Haya majengo matatu ni ya siku nyingi yana umri wa kati ya miaka 40 hadi 50, hivyo kutokana na mtikisiko wa kubomoka kwa ghorofa, yatakuwa yamepata mtikisiko na hatujui usalama wake baada ya mengine kuonyesha nyufa,” alisema Sadiki.
Kati ya maiti 26 waliookolewa katika kifusi , 21 ni za wanaume, nne za watoto na  mwanamke. Waliookolewa usiku wa kuamkia jana na kutambuliwa, ni Hamad Milambo (Tandale), mtoto Zahili Mohamed Ganji.
Maiti mwingine alikutwa na vitambulisho viwili vyenye majina tofauti. Kadi ya kupigia kura ilisomeka ni Salimu Mwaliko wa Kijiji cha Mgambo, Handeni mkoani Tanga huku kadi ya Benki ya Efata ikisomeka, Daniel Maligeli.
Miili mingine iliyotambulika ni Hamadi Mussa, Kessy Ally (aliyefia hospitali), Boniface Bernard, Gebe na aliyekutwa na karatasi mfukoni ikiwa na jina Selemani. Majina ya watoto ni Yusufu Papi, Salimin Damji na Suley Karimu.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hadi jana, watu wanane wanaodaiwa kuhusika na ujenzi wa jengo hilo walikuwa wanashikiliwa na Polisi.
Wanaoshikiliwa  ni mmiliki wa jengo Raza Hussein Damji, mtoto wa mmiliki wa jengo,  Ally Raza Damji. Wengine ni Mhandisi wa jengo,  Ugare Salu, Mhandisi wa Manispaa, Goodluck Mbaga na Mkaguzi wa Manispaa,  Wilbroad Mugyabusi.
Watuhumiwa wengine ni mmiliki wa Kampuni ya Lucky inayodaiwa kujenga ghorofa hilo, Mkandarasi Ibrahimu Kisoki  ambaye ni Diwani wa Kata ya Goba, Wilaya ya Kinondoni. 
Aidha Mhandisi Mshauri  Zonazea Anange  na Mshauri binafsi ambaye aliyekuwa akitumiwa na wamiliki wa jengo hilo, Mohamed Abudlkadir wanashikiliwa.
“Kwa sasa bado tunawahoji tukikamilisha hatua za sheria zitachukuliwa kwa waliohusika. Tunaamini watu wote hawa kila mmoja wake kwa nafasi yake angefanya kazi kwa umakini madhara kama haya yasingekuwapo,” alisema na kuongeza kuwa ni imani yao kuwa kazi hiyo ingemalizika jana.
Aidha, Kova alisema baada ya kuondoa kifusi wamebaini kuwapo kwa mifuko ya saruji na nondo jambo ambalo linaloashiria ujenzi wa ghorofa hili ulikuwa unaendelea.
Wakati huo huo baadhi ya madereva ambao magari yao yalikuwa yakitumika kubeba kifusi kwenda kumwaga Jangwani, walifanyia biashara vifusi hasa vile vyenye nondo nyingi wakiuza kwa wastani wa Sh 100,000.
Alipoulizwa hilo, Kova alisema: “Ndio kwanza nasikia habari hizo kwenu, ngoja nifanyie kazi. Kuuza kifusi hicho ni kosa kwani ni moja ya ushahidi wa kesi hii tunatarajia wataalamu kwenda kuchunguza kifusi hicho.”
Katika hatua nyingine, Kova alisema Jeshi lake limebaini wataalamu wa majanga na uokozi  na kuwaorodhesha ili kuwatumia katika kutoa maoni ya nini kifanyike kwa majanga yanapotokea.
Naibu Waziri wa Ardhi Godluck ole Medeye alisema  Serikali itatoa tamko kuhusu tukio hilo baada ya uchunguzi kukamilika.
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema majengo mengi katika Jiji la Dar es Salaam hayako salama kwa watu kuishi kutokana na kujengwa chini ya kiwango. Aliitaka Serikali kuhakikisha inafanya ukaguzi wa uimara wa majengo na yale yasiyofaa, watu waondolewe.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa alieleza kusikitishwa na ajali hiyo. Hata hivyo alihadharisha kwa kusema huu usiwe wakati wa kunyoosheana vidole kwa kuwa zipo mamlaka zinazohusika zinashughulikia suala hilo. 
Hata hivyo alisema, “Hili si janga la kwanza kutokea nchini, lazima tubadilike. Ajali nyingine zinaweza kuzuilika kama watu watafuata maelekezo ya kitaalamu,” alisema.

1 comment:

Anonymous said...

Simply desire to say your article is as amazing. The clarity in
your publish is just great and i could think you're a professional on this subject. Well together with your permission let me to grab your RSS feed to keep updated with impending post. Thanks a million and please keep up the enjoyable work.

my website: http://www.slideshare.net/IanRoach/what-exactly-does-pinterest-followers-take-care-of