PASAKA NYINGINE YAJA MACHI 14 MWAKA HUU...

Wakati asilimia kubwa ya Wakristo duniani wakiwa wanaadhimisha  Sikukuu ya Pasaka, Kanisa la Watch Tower lililojichimbia nchini na kufanya makao makuu yake ya dunia katika Kitongoji cha Kitika wilayani Kalambo katika Mkoa wa Rukwa, linaiadhimisha tofauti.

Madhehebu hayo yenye mfumo wa utawala, ambao kiongozi wake wa duniani anaitwa Papa kama ilivyo kwa Wakatoliki, limesema kama ilivyo kwa Wakristo wengine, pia lina siku maalumu ya kuadhimisha kufufuka kwa Yesu Kristo lakini kwa tarehe tofauti.
Wakati katika Ukristo zipo kalenda mbili; ya Gregori na Julias zinazotumika ikiwa ni pamoja na katika tarehe za kuadhimisha Pasaka, Kanisa hilo la Watch Tower haliangukii katika tarehe hizo isipokuwa lina tarehe yake.
Pasaka inayoadhimishwa leo (jana) inatokana na kalenda ya Gregori inayotumiwa na Makanisa ya Magharibi yaani Wakatoliki na Waprotestanti . Jina hilo limetokana na Papa Gregori XIII aliyeamua kutumia kalenda hiyo tangu tarehe 15 Februari 1582 badala ya Kalenda ya Julias inayohesabu mwaka wa siku 365 tangu kuzaliwa kwake Kristo.
Kalenda nyingine ni ya Juliasi ambayo inatumiwa na  wa-Orthodoksi katika liturgia yao na Pasaka yao itaadhimishwa Mei 5 mwaka huu.  Kalenda hiyo ilianzishwa kwa amri ya Julius Caesar mwaka 46 Kabla ya Kristo katika Dola la Roma kuchukua nafasi ya kalenda ya Kirumi.
Hata hivyo kwa upande wa Kanisa la Watch Tower, sikukuu yake ya Pasaka itakuwa Aprili 14 mwaka huu isiyoangukia katika kalenda yoyote kati ya hizo mbili.
Kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa na makao makuu ya kanisa hilo mwishoni mwa wiki,   mkesha wa Pasaka utahudhuriwa na waumini  kutoka  sehemu  mbalimbali  mkoani Rukwa  na nchi  za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi  ya Kongo (DRC) .
Hata hivyo madhehebu hayo ambayo yanadaiwa kukumbwa na mgogoro wa uongozi baada ya kuibuka mapapa watatu tofauti, katika maadhimisho ya Pasaka mwaka huu,  kila Papa atakuwa  akisherehekea  akiwa  na waumini wake kwenye makao makuu hayo yaliyoko kitongoji  cha Kitika  wilayani  Kalambo.
Viongozi hao wanaopingana ni Wilson Sikazwe (73) anayesisitiza kwamba yeye ndiye mrithi halali wa Upapa. Wengine ni Jonas Simulunga (65)  na Joseph Simgomba (50), ambaye  ni mkazi  wa Turiani, Morogoro.
Kanisa hilo linatajwa limeshakuwa na Baba Watakatifu watano ambao ni muasisi Sindani, Samwel Mwimanzi, John Chamboko, Edwin Simugala na sasa Sikazwe ambaye  hata hivyo anapingwa na hao wawili waliojitangaza kuwa na wadhifa huo. 
Kanisa hilo la Watch Tower lilianzishwa miaka 99 iliyopita katika Kitongoji  hicho  cha Kitika  ambacho kinatajwa kwamba ndipo yalipo makazi ya kudumu. Inasadikiwa lina waumini 70,000 duniani wengi wakitoka  Tanzania, Zambia, Malawi na DRC. Papa wa kanisa hilo anaitwa Wilson Sikazwe (73).
Kwa mujibu wa Sikazwe, tangu kuanzishwa kwa Kanisa hilo, limeshakuwa na Papa watano. Wa kwanza alikuwa Enock Sindani ambaye inadaiwa aliwahi kuishi na kufanya kazi Marekani, kabla ya kuja kuanzisha kanisa hilo na mfumo huo nchini.
Papa wengine waliotangulia baada ya Sikazwe mbali na muasisi Sindani, ni Samwel Mwimanzi, John Chamboko na Papa Edwin Simugala.
Akielezea imani ya kanisa hilo, Sikazwe alisema lina msimamo mkali na linaongozwa na amri 10 za Mungu. Waumini na viongozi wake, wanalazimika kushika amri hizo kwa uaminifu na uadilifu kinyume chake, wanatengwa au kuvuliwa madaraka.
Alifafanua kwamba hawana mfadhili na kanisa hilo limejengwa kwa nguvu za waumini wao na pia hawalipwi mshahara . Waumini wa kanisa hilo wanaamini Papa ni chaguo la Mungu hata akiwa hajui kusoma na kuandika. Sikazwe anasema Mwenyezi Mungu huwajaza hekima, busara na uwezo wa kutawala kupitia Roho Mtakatifu na sala.
Gazeti la HabariLEO liliwahi kuandika taarifa ya kina kuhusu kanisa hilo ikaelezwa mgogoro ulitokana na mmoja wa viongozi, kuhukumiwa na Mahakama kifungo cha miezi sita au kulipa faini kwa kukutwa na hatia ya kuiba kuku wanne.
Alilipa faini na kumrejeshea kuku wanne mtu aliyedai kuibiwa lakini  kiongozi huyo ambaye sasa ni marehemu, aliondolewa madarakani na kanisa likamtawaza Edwin Simgala kuwa Papa. Lakini Simgala ambaye pia ni marehemu sasa,  alituhumiwa kwa kashfa ya kukamatwa ugoni.

No comments: