DK MWAKYEMBE AFUNGUKA, ASEMA HANA NDOTO ZA URAIS...

Dk Harrison Mwakyembe.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison  Mwakyembe amesema hana mpango wa kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Katika hatua nyingine Waziri huyo ameshangazwa na baadhi ya wana-CCM kuanza kampeni za urais wakati Rais aliyepo madarakani, Jakaya Kikwete ana deni la kutekeleza Ilani ya Uchaguzi itakayomalizika mwaka 2015.
Waziri Mwakyembe aliyasema hayo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alipowahutubia waandishi wa habari kwenye Bonanza la Waandishi wa Habari maarufu kama Media Day Bonanza linalofanyika kila mwaka na kuandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA).
Waziri huyo alisema kutokana na kusaka urais, baadhi ya wahusika wa mpango huo wamekuwa wakileta choko choko za kidini na za kisiasa hatua ambayo imeifanya Tanzania kuingia kwenye migogoro ambayo haikuzoeleka kabla.
“Nimeulizwa sana kama nina mpango wa kugombea urais. Wapo wanaohusisha hata jitihada zangu za kuiboresha Bandari ya Dar es Salaam na taasisi zilizo chini ya Wizara yangu na suala la urais. Naomba niwahakikishie kwamba sina mpango huo. Mpango wangu ni kuwa Waziri bora wa Uchukuzi,” alisema.
Akiwazungumzia walioanza kampeni hizo za urais, Dk Mwakyembe alisema wanafanya makosa kwa vile wanatibua mikakati ya Rais Kikwete na CCM katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi.
“Rais  hajamaliza muda wake na ana deni la ahadi alizozitoa kwa wananchi. Kwa hawa watu kujitokeza na kuanza kufanya kampeni za urais badala ya kusaidia katika utekelezaji wa Ilani kunaleta shida na kunadhoofisha nguvu ya pamoja ya kuwatumikia wananchi.
“Hizi choko choko za kidini na vurugu nyinginezo chanzo ni hawa watu, naomba niwaeleze wazi kwamba mipango yao inatuletea shida sana. Mimi siwezi kuwa miongoni mwao nitaendelea kufanya kazi zangu kama Waziri wa Uchukuzi kwa bidii ili niwe Waziri bora kuliko wote waliowahi kuongoza Wizara ya Uchukuzi,” alisema.
Katika hatua nyingine Waziri Mwakyembe alisema ataangalia kwa kina mazingira yaliyosababisha Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kubariki upandishaji wa nauli za mabasi ya abiria ndani ya miji na mikoani ili kuangalia kama nauli zilizowekwa hazina athari kwa wananchi.
Alisema katika mazingira yoyote yale Serikali haitakuwa radhi kukubali ongezeko la nauli litakalokuwa mzigo kwa wananchi na kuwaongezea ugumu wa maisha.
“Niseme tu kwamba nilikuwa jimboni (Kyela) na nimelisikia suala la nauli, lakini lilikuwa halijanifikia rasmi mezani kwangu. Kwa vile leo limenifikia rasmi nitalichunguza kwa kina  na ninawahakikishia wananchi kwamba Serikali itakuwa upande wao katika kuhakikisha kuwa wanalipa nauli inayokubalika,” alisema.
Hivi karibu Sumatra ilitangaza ongezeko la nauli kwa daladala na mabasi ya mikoani kwa karibu asilimia 24, kiwango kilichopangwa  kuanza kutumika rasmi Aprili 12, mwaka huu. Hata hivyo Waziri Mwakyembe alisema atatoa msimamo wa Serikali kabla ya tarehe husika kufika.
Akizungumzia madai yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwamba amehusika katika kashfa ya ufisadi kwa kuipatia Kampuni ya Jitegemee Trading zabuni ya ujenzi wa Bandari ya Nchi Kavu kinyume cha sheria, Waziri Mwakyembe alisema madai hayo hayana msingi.
Hivi karibuni Chadema walisema Waziri Mwakyembe  alitoa zabuni ya ujenzi huo wa Bandari ya Nchi Kavu katika Viwanja vya Sukita kwa Kampuni inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinyume cha sheria za ununuzi.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila alisema juzi: “Mwakyembe aseme alitoa zabuni hiyo kwa Jitegemee kwa kuzingatia vigezo gani? Kampuni ngapi zilishindanishwa katika mchakato huo na asipofanya hivyo hastahili kukaa wizarani hapo bali apelekwe Segerea gerezani kwani ni kosa kubwa kutoa zabuni kinyemela.”
Akijibu mapigo hayo jana Waziri Mwakyembe alisema tuhuma hizo si za kweli na kwamba zinatolewa na mafisadi aliosema walitaka kulinunua eneo hilo kwa njia za kifisadi ili baadaye walikodishe kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kwa gharama kubwa, mpango ambao aliunasa na kuukomesha.
“Nataka niwahakikishie kwamba taratibu zote zilifuatwa lakini hawa watu wana chuki kutokana na kutaka kulichukua eneo hilo. Hili ni eneo muhimu sana kwa Wizara yangu maana tutapata eneo la kutosha la kuhifadhi magari na bidhaa nyingine zinazotoka bandarini na kutuepushia shida tunayoipata sasa.
“Hata kama watalipata eneo hilo kutokana na mipango yao ya kifisadi ikiwepo ya kukitumia chama cha Chadema, napenda niwahakikishie kwamba kamwe hawataingia zabuni na TPA ili wawakodishie na kujipatia mabilioni ya fedha kama walivyokuwa wamepanga,”  alisema Waziri Mwakyembe.

No comments: