BAADA YA MGOGORO, KKKT YATANGAZA NAFASI YA KATIBU MKUU...


Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, limetangaza nafasi ya Katibu Mkuu, ili kumpata msimamizi atakayeendesha Dayosisi hiyo kuanzia Julai Mosi.

Tangazo hilo limetolewa jana wakati Katibu Mkuu aliyepo, Israel Karyongi, Desemba 12 mwaka jana, aliongezewa mkataba wa mwaka mmoja na Kanisa hilo, uliokuwa uishe Desemba 12 mwaka huu.
Kabla ya kutangazwa kwa nafasi hiyo jana, Kanisa hilo lilikumbwa na mgogoro baada ya kuweka mali za Kanisa rehani na kuchukua mkopo, ambao ulihatarisha mali hizo kunadiwa. 
Hali hiyo imesababisha baadhi ya waumini wa Dayosisi hiyo, kutupia lawama uongozi wa Kanisa hilo na kuutaka ujiuzulu, akiwamo Karyongi. 
Habari za kutoka ndani ya Dayosisi hiyo, zilidai kuwa miradi inayodaiwa kuwa fedha zake zimetumika vibaya, ni hoteli ya Corridor Springs na Hospitali ya Rufaa ya Selian, ambayo kwa pamoja iligharimu Sh bilioni 11 kutoka michango ya waumini na misaada ya wafadhili. 
Hata hivyo, wakati ikidaiwa kuwa fedha hizo zimetokana na michango ya waumini na wafadhili, kulikuwa na madai mengine kuwa fedha hizo zilikopwa katika moja ya benki nchini kwa ajili ya uanzishwaji wa miradi hiyo. Benki ya CRDB, ilipata kukiri kukopesha Kanisa hilo kwenye miradi yake.
Kutokana na hatari ya kunadiwa kwa miradi hiyo, waumini zaidi ya 600,000 wa Dayosisi hiyo, walitakiwa kuchangia Sh 20,000 kila mmoja ili ‘kuokoa jahazi’. Kama waumini wote hao wangetoa mchango wao kama ilivyotarajiwa, zingepatikana   Sh bilioni 12.
Dayosisi hiyo imetoa sifa anazotakiwa kuwa nazo mwombaji wa nafasi hiyo ya, ikiwamo kuwa raia wa Tanzania, Mkristo Mlutheri aliyeoa au kuolewa kwa ndoa ya kikristo, anayeshiriki meza ya bwana na anayetokana na Dayosisi ya Kaskazini Kati. 
Pia anatakiwa kuwa na elimu ya Shahada ya chuo kikuu katika fani tofauti kama za Fedha, Uchumi, Sheria na Utawala pamoja na Ualimu.
Ilielezwa kuwa sifa nyingine ni kuwa na uzoefu katika uongozi kwa muda usiopungua miaka mitatu, kuwa na uwezo wa kuzingatia maagizo, sheria na kanuni, kusimamia utekelezaji na kuzitolea taarifa.
Anatakiwa pia awe na  umri wa kati ya miaka 40 na 55 na kuwa tayari kuanza kazi Julai mosi.  
Barua zote zinatakiwa kupitia kwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa mwombaji na mwisho wa kupokea maombi hayo ni Mei 10.

No comments: