KIKWETE AAGIZA UCHUNGUZI WA JENGO LILILOPOROMOKA UHARAKISHWE...

Wasamaria wakishiriki kazi ya uokoaji katika jengo lililoporomoka hivi karibuni.

Rais Jakaya Kikwete, ameagiza uchunguzi wa chanzo cha kuporomoka jengo la ghorofa 16 katika makutano ya barabara za Indira Ghandi na Morogoro, Dar es Salaam, ufanyike haraka.

Ametaka ukweli ujulikane na wanaopaswa kuadhibiwa na kuwajibika, wafanye hivyo mara moja, ili kuporomoka kwa jengo hilo Machi 29 na kusababisha vifo vya watu 34 na majeruhi 18, mkondo wa sheria uchukue nafasi yake ili liwe fundisho.
Wakati Rais akiagiza hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, amesema Serikali imedhamiria kutoacha mtu aliyehusika katika tukio hilo. 
Agizo la Rais lilitolewa jana katika ukumbi wa PTA, kwenye viwanja vya Maonesho ya Sabasaba vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam alipokuwa akipongeza wadau waliosaidia kuokoa maisha ya watu na kuopoa miili iliyofukiwa na kifusi baada ya ajali hiyo.
Katika hafla hiyo, viongozi wa Serikali, taasisi za kidini na vyama vya siasa walihudhuria. Na kabla ya hotuba ya Rais, Sadiki alimhakikishia Rais na Watanzania kuwa hakuna aliyehusika katika ajali hiyo atakayepona, na tayari watu 11 wamefikishwa mahakamani.
 “Niliguswa sana na mwitikio wa watu na jitihada za kuokoa wenzetu, kazi kubwa ilikuwa kuondoa vifusi na kufikia walikofukiwa, kazi imefanyika. 
“Watu binafsi, kampuni na taasisi zilijitokeza, Jeshi lilikuwa pale, japo ni moja ya majukumu yake, lakini hawakusubiri amri yangu, sina maneno mengi bali nasema ahsanteni sana,” alishukuru Rais Kikwete.
Alisema pamoja na kwamba viongozi wa dini waliotoa dua  walisema kila mtu ana njia yake ya kufikwa na mauti, lakini Serikali haitaishia hapo.
“Lazima tutafute kwa nini jengo halikusimama? Mpaka sasa hatua kadhaa zimeshachukuliwa na wanaoendelea na uchunguzi wafanye haraka, tuepushe haya yasitokee kwingine,” alisema Rais Kikwete.
Alitaka Watanzania kuendeleza moyo wa uzalendo katika matukio mengine ya ghafla, na kusisitiza kuwa ingawa si maombi yake kuwa majengo yabomoke kama hilo, lakini kwa kuwa ajali haina kinga, inapotokea, watu wanapaswa kutoa msaada kama walivyofanya katika ajali hiyo ya jengo.
Rais Kikwete alisema kikao cha jana ni moja ya mwitikio wake kwa ombi la Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, kupongeza washiriki wa uokoaji na uopoaji siku kazi hiyo ilipokamilika, Aprili mosi. 
Sadiki kabla ya kumkaribisha Rais kutoa vyeti vya kutambua wadau hao na kisha kuhutubia maelfu ya waliohudhuria kikao hicho, alimweleza Rais kuwa hatua kadhaa zimeshachukuliwa na hatasalia hata mmoja aliyehusika.
“Rais wewe mwenyewe ulifika siku ya tukio na viongozi wengine wa juu wa Serikali na kujionea hali na kazi ilivyokuwa ikifanyika, waokoaji hawakulala, walifanya kazi saa 24, hatua kadhaa za kusimamisha ujenzi wa jengo pacha zimechukuliwa wakati uchunguzi ukiendelea na watu 11 tayari wamefikishwa mahakamani,” alisema Sadiki. 
Sadiki alimwomba Rais kubeza waliokejeli hatua hiyo ya kupongeza wadau hao na kudai kuwa wanaobeza hata kwenye tukio hilo hawakuonekana na mtaa wenyewe wa Indira Ghandi, hawajui ulipo na jana hakukuwa na sherehe bali kikao.
Akitoa dua kabla ya kikao kuanza, Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum na Mchungaji George Fute wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), walimwomba Mungu alinusuru Taifa dhidi ya majanga, ufisadi na uchakachuaji.
Viongozi hao wa dini, walitaka Watanzania wasilalamikie Serikali, bali waisadie kukabiliana na changamoto zilizopo.
Katika kikao hicho, Yusuf Abubakar, alishangiliwa na washiriki baada ya kupewa cheti kwa niaba ya wananchi wa kawaida,  kwa  kutumia ujuzi mkubwa wa fimbo kuchomeka kwenye kifusi na kubaini mtu chini ya kifusi usawa wa fimbo. Alisema ujuzi huo aliupata Sudan.
Utoaji vyeti katika hafla hiyo ulifanywa kwa makundi  saba; la Uratibu (Kamati ya Maafa ya Mkoa), vikosi vya uokoaji, huduma ya matibabu, ulinzi na usalama, huduma ya mahitaji ya jamii, mwakilishi wa wananchi na waandishi wa habari. 
Miongoni mwa taasisi na kampuni zilizopewa vyeti vya kuthamini mchango wao katika tukio hilo, katika kundi la waandishi wa habari ni Kampuni ya Tanzania Standards Newspapers (TSN) Limited, inayochapisha HabariLeo, Daily News na gazeti la michezo la SpotiLeo.
Wengine katika kundi la vyombo vya habari ni African Media (Channel Ten), Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Jambo Leo, Uhuru, Majira, Mwananchi, New Habari (2006) na vingine.

No comments: