MAALBINO 73 WAUAWA, WENGINE 34 WAJERUHIWA...

Wasanii wa kikundi cha watu wenye ulemavu wa ngozi wakitumbuiza katika moja ya maadhimisho ya kitaifa.
Maalbino 73  wameuawa na wengine 34 kujeruhiwa nchini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2007.
Sambamba na hilo, makaburi 19 ya watu hao yamefukuliwa kwenye maeneo mbalimbali nchini katika kipindi hicho.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mratibu wa Uhusiano wa Nje wa asasi isiyo ya Serikali ya Under The Same Sun (UTSS), Seif Kondo alipozungumza na wahariri wa  vyombo vya habari nchini  katika hafla ya asasi hiyo kutimiza miaka minne, iliyofanyika Dar es Salaam.
Kuhusu kesi za watuhumiwa wa vitendo hivyo, Kondo alisema mpaka sasa zilizosikilizwa ni nne huku akitupa lawama kwa Serikali kushindwa kusikiliza kesi zingine kwa maelezo ya ukosefu wa fedha.
“Hizo nne zimesikilizwa kutokana na ufadhili wa nje, lakini tuna imani kwamba Serikali ina uwezo wa kukamata na kufungua kesi dhidi ya watuhumiwa na kuzimaliza,” alisema Kondo.
Kuhusu sababu za kutaka kesi zao ziharakishwe tofauti na za mauaji mengine, Kondo alisema kundi la wenye albinism ni maalumu na hivyo kesi zao nazo zinapaswa kuchukuliwa kwa mwelekeo huo huo.
Alitumia fursa hiyo pia kufafanua juu ya kuitwa majina ya kudhalilishwa kama zeruzeru, wenye ulemavu wa ngozi, albino na majina mengine, akisema kuwa wao wanapenda kuitwa watu wenye albinism.
“Majina tunayoitwa yanatudhalilisha na kutunyanyapaa, sisi tunataka tuitwe kwanza watu kwa sababu ni … wenye albinism,” alisema na kusisitiza licha ya kuambiwa kuwa albinism si neno la Kiswahili, lakini akang’ang’ania kuwa linapaswa kutoholewa.
Meneja Uzalishaji wa UTSS, Rachel Moyo alishukuru wanahabari nchini kwa kufichua mauaji ya wenye albinism na kuomba ushirikiano zaidi kwa kutoa elimu kwa umma juu ya hali hiyo na jinsi ya walio nayo kujitunza. Katika sherehe hiyo keki ilikatwa na shampeni kufunguliwa.

No comments: