UHURU KENYATTA SASA RAIS HALALI WA KENYA...

Uhuru Kenyatta.
Mahakama Kuu ya Kenya imeamua kuwa Rais mteule Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza William Ruto, walichaguliwa kwa njia huru na ya haki katika uchaguzi uliofanyika Machi 4, mwaka huu.

Uamuzi huo una maana kuwa Uhuru Kenyatta ndiye atakayeapishwa kama Rais mpya wa Kenya, sherehe itakayofanyika Aprili 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa michezo wa Moi Kasarani. Aidha, siku hiyo imetangazwa itakuwa Siku ya Mapumziko kwa Wakenya.
Awali ilikuwa aapishwe Machi 26 mwaka huu, lakini pingamizi lililowasilishwa katika Mahakama  hiyo ya juu zaidi na mpinzani mkuu wa Kenyatta, Raila Odinga, baada ya uchaguzi huo, ndilo lililotibua mambo, hivyo kusubiri uamuzi wa mahakama.
Matokeo rasmi yalionesha kuwa Kenyatta alishinda uchaguzi huo kwa kumpiku Odinga kwa asilimia 50.07 dhidi ya asilimia 43.28 alizozipata yeye. Matokeo haya yalizuia kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi kwa kura 8,100.
Odinga aliyekuwa Waziri Mkuu katika Serikali iliyomaliza muda wake ya Mwai Kibaki, aliishutumu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya kwa kuhujumu matokeo ya uchaguzi huo ili kumpa ushindi Kenyatta.
Uchaguzi wa urais, wabunge na wajumbe wengine wa Serikali, ulifanyika Machi 4, ukiwa wa kwanza tangu uchaguzi uliokumbwa na ghasia mwaka 2007 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1,200.
Kenyatta na mgombea mwenza, Ruto, wanakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kwa kuchochea ghasia hizo za mwaka 2007. Hata hivyo wamekanusha mashtaka hayo.
Mahakama hiyo ilikuwa na uwezo wa kuthibitisha ushindi wa Kenyatta au kuubatilisha na hivyo kuitisha uchaguzi mpya, jambo ambalo halijatokea.
Mapema jana, Rais mstaafu Mwai Kibaki aliwataka Wakenya kuwa watulivu na kukubali uamuzi wa Mahakama hiyo wakati ambao Wakenya wana imani kubwa na Idara ya Mahakama baada ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa.
Mawakili wa Odinga walisema kuwa kesi yao ilihusisha madai ya kuhujumu hesabu ya kura pamoja na matatizo ya usajili wa wapiga kura na vile vile matatizo ya mitambo ya usajili wa wapiga kura. Mawakili hao walikubaliana na uamuzi huo wa mahakama.

No comments: