MNYIKA KUONGOZA MAANDAMANO YA MAJI DAR MACHI 16...

Baadhi ya kinamama wa Dar es Salaam wakipanga foleni kusubiria maji.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amewasilisha notisi kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela kwa ajili ya kuitisha mkusanyiko wa wananchi na kuongoza maandamano kwenda Wizara ya Maji.
Lengo la maandamano hayo ni kupeleka kilio chao tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam kwa wizara hiyo, inayoongozwa na Profesa Jumanne Maghembe na Naibu wake, Dk Binillith Mahenge.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mnyika alisema amepanga  kuitisha mkusanyiko huo,  utakaokwenda pamoja na maandamano Machi 16 mwaka huu.
Maandamano hayo yataanza saa 5.00 asubuhi katika eneo la Bakhresa, Manzese kwenda makao makuu ya Wizara ya Maji yaliyopo eneo la Ubungo.
Alisema  hatua hiyo imekuja, kutokana na kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Dar es Salaam juu ya tatizo la maji kutopatiwa majibu hadi hivi sasa, hivyo kuwaacha wananchi wakihangaika, huku akifananisha kitendo hicho sawa na ufisadi katika Wizara ya Maji.
Mnyika alisema Kifungu cha 43 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi  Sura ya 322,  kinampa mamlaka ya kuwasilisha notisi hiyo ya kutoa taarifa ya kuitisha mkusanyiko na maandamano hayo bila kuwepo na ukiukwaji wowote wa taratibu.
Alisema ameshatekeleza wajibu wake kuhusu kusudio lake hilo. Alisema kwamba kilichobaki ni siku ya kufanyika kwa maandamano hayo, aliyoyaita kuwa ya amani.

No comments: