TANESCO YAENDESHA KINYEMELA MGAWO WA UMEME USIKU...

Pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) , kutangaza kuwa hakuna mgawo wa umeme, lakini wakati wa mahitaji makubwa ya umeme hasa usiku, limekuwa likilazimika kuendesha mgawo mdogo.
Akizungumza jana Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alisema kuwa pamoja na kuzalisha umeme kwa kutegemea mitambo ya dharura, hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea yatakayofanya kuwapo kwa mgawo wa umeme.
“Hakuna jambo lolote jipya lililotokea, bado hali ya maji ni kama ilivyokuwa mwaka jana, bado tuko kwenye hali ya dharura, lakini umeme umeendelea kupatikana na ndivyo hali itakavyoendelea kuwa. Uwezo wa kuzalisha umeme upo, kinachotakiwa ni fedha ya kununulia mafuta,” alisema.
Hata hivyo, alikiri kuwa mahitaji ya umeme kwa nchi nzima ni wastani wa megawati 750 kwa siku na kuwa nyakati za matumizi makubwa, ambazo ni kuanzia saa 12 jioni mpaka saa tano usiku, hufikia megawati 850.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mramba jana, wakati uwezo wa kuzalisha umeme wa maji ni kati ya megawati 120 hadi 130, umeme unaozalishwa na gesi kutoka Songosongo ni megawati 330 na umeme wa   mafuta ni megawati 365.
Kutokana na takwimu hizo, inaonesha kuwa katika hali ya kawaida Tanesco huwa na uwezo wa kuzalisha megawati 825 na hivyo wakati wa usiku, kuanzia saa 12 jioni mpaka saa 5 usiku, hukabiliwa na upungufu wa megawati 25 kwa kuwa mahitaji hufikia megawati 850.
Mbali na kutokiri kuwa kuna wakati Tanesco inakabiliwa na upungufu wa umeme, lakini Mramba alikiri kuwa   kuzalisha umeme kwa njia ya mafuta ni ghali ambako kiasi cha megawati 365 zinazozalishwa kwa siku, hugharimu Sh bilioni 5.4 kwa siku, huku mapato ya shirika yakiwa ni Sh bilioni 2.34 kwa siku.
Aidha, Mramba aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ruzuku inayotumika kununua mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura, ambapo kwa takribani miezi saba tangu Juni mwaka jana, hadi Februari mwaka huu, imetoa kiasi cha Sh  bilioni 231.2.
“Mapato yetu hayawezi kabisa kuendesha mitambo hiyo inayosaidia upatikanaji wa umeme, niishukuru sana Serikali kwa kutusaidia kwa kutoa ruzuku ya kununulia mafuta na ndio maana umeme upo,” alisema.

Comments

Popular Posts