ZANZIBAR YAWATOA HOFU WATALII KUHUSU MAUAJI...

Baadhi ya majengo ya kitalii katika mji wa Zanzibar.
Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imewahakikishia  watalii usalama kwa kuweka ulinzi katika vyanzo vikuu vya utalii.
Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk alisema pamoja na matukio ya hivi karibuni ya mauaji, visiwa hivyo viko salama.
Alitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari kutokana na matukio ya hivi karibuni ya mauaji ya Padri wa Kanisa Katoliki la Minara Miwili, lililopo Mji Mkongwe Zanzibar, Evarist Mushi (56).
Kuuawa kwa padri huyo kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akienda kuendesha misa ya Jumapili, kuliibua hisia kali kupitia vyombo vya nchini na vya kimataifa.
Akifafanua katika taarifa yake, Mbarouk alisema serikali imekutana na wawekezaji na wamiliki wa hoteli za kitalii na kuahidi kuweka ulinzi katika maeneo hayo.
 “Hali ya utalii na usalama wa wageni wanaozuru Zanzibar ni salama...tumekutana na wawekezaji na wamiliki wa hoteli za kitalii kwa kuwaahidi kuwapatia ulinzi kadri inavyowezekana,” alisema.
Alisema ulinzi umeimarishwa katika maeneo ya vyanzo vikuu vya utalii, ikiwemo Kanisa la Anglikana la Mkunazi,  ambalo zamani lilikuwa soko kuu la watumwa waliokuwa wakitoka sehemu mbali mbali za Afrika ya Mashariki na kuuzwa hapo.
Mkuu wa Idara ya Mapokezi ya Watalii katika Kanisa hilo, John Mwakanjuki alisema wamekuwa wakipokea askari polisi wanaokuja kwa zamu kuanzia asubuhi, jioni hadi usiku kulinda eneo hilo.
“Tunashukuru sana hapa ulinzi umeimarishwa kutoka jeshi la polisi na hii imetusaidia sana katika usalama wa kanisa na watalii wanaozuru hapa,” alisema Mwakanjuki.
Kanisa la Mkunazi ambalo ni la kihistoria,  lilijengwa mwaka 1893. Ni moja ya makanisa ya mwanzo katika Afrika ya Mashariki. Kiwanja cha ujenzi wa kanisa hilo, kilitolewa na mtawala wa wakati huo, Sultani wa Oman.
Takwimu zinasema kanisa hilo kwa mwaka hupokea zaidi ya watalii 60,000 wanaozuru  hapo na kujipatia historia ya kale na kutembelea mapango ya chini kwa chini, yaliyokuwa yakitumiwa kusafirisha watumwa kutoka baharini.
Aidha doria ya polisi imeonekana ikifanyika Kaskazini mwa kisiwa cha Zanzibar, ambako kuna hoteli nyingi za kitalii, ikiwemo Kiwengwa, Pwani Mchangani na Nungwi.
Mmoja ya wasambazaji wa vyakula ikiwemo samaki katika hoteli za kitalii saba zilizopo eneo la Kiwengwa, Chura Abdalla alisema hali ya utalii bado ni imara, licha ya kujitokeza kwa matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani.
Chura anayetoa huduma katika hoteli kubwa za kitalii zilizopo Kiwengwa, ikiwemo ya Mapenzi na Sea Cliff , alisema mwaka jana hali ya utalii iliyumba, kutokana na kujitokeza kwa matukio ya fujo yaliyosababishwa na wafuasi wa kundi la Uamsho.
“Vurugu na fujo za uamsho za mwaka jana zilizorotesha maendeleo ya sekta ya utalii ambapo baadhi ya mahoteli yaliahirisha kupokea watalii kutoka nje ya nchi,” alisema Chura.
Awali akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Habari, Mbarouk alisema kwa sasa Kamisheni ya Utalii Zanzibar ipo katika mikakati ya kuimarisha masoko ya utalii katika nchi za Asia, ikiwemo China, Japan na Korea zenye idadi kubwa ya watu.
Mwaka jana, Zanzibar inatajwa kwamba ilipokea watalii 175,000. Imewekwa mikakati ifikapo mwaka 2020 wapokee watalii 500,000.
 Sekta ya Utalii Zanzibar ni tegemeo katika kuchangia pato la taifa kwa asilimia 27 huku ikitoa ajira kwa zaidi ya wananchi 25,000 katika maeneo mbalimbali. 
Zanzibar hutegemea kupokea watalii wengi kutoka Italia, Uingereza, Hispania pamoja na nchi za Scandinavia.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia Kanisa la Living Water Centre  lililoko Kawe,  Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliwaeleza waumini  jana kwamba pamoja na vurugu za kidini zilizotokea, Tanzania ni nchi ya amani na mfano kwa Afrika.
Dk Mwakyembe alitaka Wakristo na Waislamu kuendelea kuhubiri amani. Aliwaonya vijana kutokubali kutumiwa kuigawa nchi. Aliwataka waendelee kumuenzi Baba wa Taifa, Julius Nyerere kwa vitendo kwa kuimarisha amani.
Kwa upande wake, kiongozi wa kanisa hilo, Mtume na Nabii Cosmas Ndegi alitaka viongozi  wa dini wakemee na kusimamia kwa vitendo kauli wanazotoa.  Alisema, “tumekuwa wazungumzaji mno, haitoshi tusimamie kwa vitendo na tusimamie serikali na siyo kukaa kimya.”

No comments: