ZANZIBAR SI SHWARI! IMAMU AUAWA KWA MAPANGA...

Msikiti wa Mwakaje, Zanzibar.
Imamu wa Msikiti wa Mwakaje, Ali Khamis Ali (60)  amepigwa mapanga hadi kufa na watu wanaodhaniwa kuwa wezi alipokwenda shambani mwake kukagua mazao yake Kitope mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada Abdalla alithibitisha kutokea mauaji hayo na kusema juzi mchana alikwenda shambani kwake na kukuta watu wakiiba nazi katika shamba hilo ambapo walimvamia na kumpiga mapanga.
“Ni kweli marehemu alivamiwa na watu wanaoaminika kuwa wezi shambani ambako kumekuwa na wizi wa mazao uliokithiri,” alisema.
Marehemu alizikwa jana na waumini wa dini ya kiislamu katika Msikiti wa Mwakaje, ambapo Jeshi la Polisi lilisema limeanza msako dhidi wahusika waliofanya uhalifu huo.
Mapema Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema Jeshi lake limetangaza dau nono la Sh milioni 10 kwa watu watakaotoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watu waliomuua Padri Evarist Mushi wiki iliyopita.
“Jeshi la Polisi linatangaza dau la Sh milioni 10 kwa watu watakaotoa taarifa na hatimaye kukamatwa kwa wahalifu waliomuua Padri Mushi,” alisema Mussa.
Akifafanua, alisema hadi sasa Polisi imekamata watu kadhaa wakifanyiwa mahojiano kuhusu taarifa za kifo cha Padri Mushi.
“Tumekamata watu kadhaa tukiwafanyia mahojiano zaidi kuhusu tukio la mauaji ya Padri Mushi lakini hatujamfikisha mtu yeyote mahakamani hadi sasa,” alisema Mussa.
Haya ni mashambulizi ya nne kutokea tangu mwaka jana dhidi ya viongozi wa dini, ambapo katika tukio la kwanza, Shehe Fadhil Suleiman Soraga alimwagiwa tindikali akiwa mazoezini karibu na nyumbani kwake Magomeni saa za asubuhi.
Shambulizi lingine ni dhidi ya Padri Ambrose Mkenda ambaye alipigwa mapanga shingoni nyumbani kwake Tomondo, Unguja.

No comments: