WANANDOA WATUMIA MAJI YA TANKI LENYE MWILI WA MTU HOTELINI...

KUSHOTO: Michael na Sabina. KULIA: Mafundi wakichunguza matanki hayo.
Wanandoa wa Uingereza walioko mapumzikoni mjini Los Angeles wameeleza jinsi walivyokunywa, kuoga na kupiga mswaki meno yao kwa kutumia maji kutoka katika tanki lililoko katika paa la hoteli - ambamo mwili wa mwanamke ulikuwa umezama kwa wiki tatu.
Ni hadi pale mwili ulioharibika wa mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye miaka 21, Elisa Lam ulipogunduliwa wiki hii ndipo walipobaini kwanini maji ya hoteli hiyo yalikuwa na ladha ya 'ajabu'.
Sabina Baugh, mwenye miaka 27, alikaa siku nane na mumewe Michael, ambaye pia ana miaka 27, kwenye Hoteli ya Cecil iliyoko Los Angeles.
Eneo hilo lina matukio mengi ya uhalifu katika jiji, hivyo kuliko kutoka usiku na kwenda kusaka chupa ya maji ya kunywa, walikunywa kutoka kwenye bomba.
Juzi Sabina, mwalimu wa piano, alisema: "Maji hayo yalikuwa na ladha ya ajabu na inayokera. Hatukuwahi kamwe kufikiria kitu kama hicho. Tulifikiri ilikuwa ndivyo yalivyo."
Michael, mpiga gitaa na mwalimu wa muziki, aliongeza: "Pale tulipobaini, tulijihisi kuumwa tumbo, hali mbaya mno. Hatuko sawa kisaikolojia. Ni kitu cha elimu nafsia. Kama unakifikiria, sio kizuri."
Wanandoa hao pia walisema maji katika hoteli hiyo inayotoza Pauni 52 kwa usiku mmoja, na kupewa hadhi ya nyota mbili katika mtandao wa TripAdvisor, yalikuwa  yakichuruzika kutoka kwenye bomba. Wageni wengine waliripoti mafuriko.
Wanandoa hao wanaotokea Plymouth, sasa wanakaa katika sehemu nyingine ya mji na mamlaka hizo zinachunguza maji hayo katika eneo hilo kwa uchafu.
Polisi walithibitisha juzi kwamba mwili huo ulikuwa wa Elisa Lam, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha British Columbia nchini Canada, ambaye alikuwa akisafiri kwenda Santa Cruz kaskazini mwa California ndipo alipotoweka mwanzoni mwa mwezi na kuipa wasiwasi familia yake.
Polisi hawafahamu jinsi gani Elisa alivyokufa au jinsi alivyoishia kwenye tanki katika paa la hoteli, ambayo inalindwa na milango madhubuti na kengele za dharura.
Hoteli hiyo ilijengwa mwaka 1920 lakini ilikarabatiwa miaka kadhaa iliyopita wakati fulani ilikuwa makazi mara kwa mara ya muuaji Richard Ramirez - aliyejipa jina la utani the Night Stalker - na Jack Unterweger aliyehusika na vifo vya makahaba tisa barani Ulaya na Marekani.
Polisi wamesema kumekuwa na ripoti za kuendelea kwa uhalifu katika hoteli hiyo.
Mwili wake uligunduliwa kwenye moja ya matanki makubwa ya maji baada ya wafanyakazi wa matengenezo walipopanda juu kuchunguza taarifa za kuwapo kwa presha ndogo ya maji, msemaji wa polisi wa Los Angeles alisema.
Bernard Diaz, mwenye miaka 89, ambaye ameishi hapo kwa miaka 32, alilieleza gazeti la Los Angeles Times kwamba alisikia kelele 'kubwa' katika ghorofa yake juu usiku ambao Elisa alitoweka.
Alisema ghorofa hilo lilikumbwa na matatizo ya mafuriko ya maji usiku huo.

No comments: