WAMWAGA MAJI YOTE NYUMBANI KWA MKUU WA MKOA...

Mwantumu Mahiza.
Nyumba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani imeponea chupuchupu kuchomwa moto na wananchi waliokuwa na hasira kutokana na kukatika maji wiki mbili mfululizo.
Aidha, mkoani Dar es Salaam jana kulikuwa na maandamano ya wanawake na watoto wa eneo la Kimara ambao ilielezwa walikuwa wakitaka kwenda nyumbani kwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kuelezwa hatma ya upatikanaji maji ili waondokane na gharama kubwa kuyanunua. 
Mkuu wa  Mkoa  wa Pwani, Mwantumu  Mahiza alisema wiki iliyopita kwamba umati wa watu uliingia kwa nguvu nyumbani kwake na kumimina maji yote aliyokuwa amehifadhi.
“Wiki iliyopita nusura nyumba yangu ichomwe moto… kwani maji yalikatika hapa kwa wiki mbili na wananchi kuamua kuvamia kwangu na kujimiminia maji yote niliyokuwa nimehifadhi kwa ajili ya matumizi yangu,” alisema.
Alitoa taarifa hiyo kwa Waziri wa Maji, Profesa Maghembe aliyekuwa mkoani humo kwa ajili ya kukagua ujenzi wa  mradi  wa maji wa awamu ya pili  wa  Chalinze.
Aliendelea: “Mheshimiwa Waziri mimi pale nyumbani nina walinzi wawili, wananchi waliamua kutumia nguvu na kujimiminia maji…sasa fikiria kama wasingekuta maji yaliyohifadhiwa nyumbani kwangu naamini kabisa nyumba yangu wangeiteketeza kwa moto.”
Akizungumza akiwa Vigwaza, Mwantumu alisema kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kumezua mgogoro mkoani mwake.
Alisema wananchi  walichukua uamuzi wa kuvamia nyumba yake wakiamini kuwa  hali hiyo ingesababisha Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasco) kufungua maji. 
Aliongeza kuwa maji ni uhai na hayana kabila, dini wala na upendeleo kwani kila mmoja anayahitaji ili aishi.
Aidha, alishutumu wahandisi wa mradi huo. “Wahandisi tambueni  kuwa hamtendi haki…ninyi  ndio mlioingia mkataba na Wizara, sasa mnasubiri nani awaletee hizo risiti za madai ya malipo ndio mwendelee na ujenzi?  Alihoji Mwantumu.
Aliwaambia kama hawawezi kufuatilia wamtume na yeye atakwenda ili maji yaweze kupatikana kwa haraka.
Waziri Maghembe alikiri mradi huo wa maji kwenda taratibu  na akataka makandarasi wanaoendelea na ujenzi kubadilika, la sivyo watajieleza kama hawataki kuendelea na kazi.
Alisema Mkandarasi Mega Builders ambaye ni mmoja wa wakandarasi wa mradi huo ametimuliwa,  kutokana na kushindwa kuendelea na kazi huku akidai Rais Jakaya Kikwete ni rafiki yake.
Alisema pia yupo mkandarasi wa kituo cha mradi mwenye asili ya China, ambaye kila akifuatwa kwa ajili ya marekebisho hujifanya haelewi Kiingereza wala Kiswahili isipokuwa Kichina.
“Lakini pindi akisifiwa kama kazi kafanya vizuri huelewa anachoambiwa, jambo ambalo linarudisha nyuma kukamilika kwa mradi,” alisema Maghembe.
Alitaka  makandarasi kukabidhi mradi huo ifikapo Mei 30. “Kuanzia leo tubadilike twende haraka… nataka nikabidhiwe mradi Mei 30 ili wananchi wa mkoa huu waweze kunufaika na maji kama ambavyo tumekuwa tukiwaahidi,” alisema Profesa Maghembe katika majumuisho.
Alisema kuanzia mwaka huu wa fedha Serikali itakuwa inalipa ankara  za taasisi za umma zinazodaiwa maji, kutokana na kuonekana kuwa na madeni makubwa.
Kwa mujibu wa Waziri, kuna deni la zaidi ya Sh milioni 123.6 ambalo linatokana na taasisi hizo ambazo zimeunganishiwa maji.
Profesa Maghembe alisema Wizara ya Fedha itaanza kulipa  ankara zote zinazozikabili taasisi za umma kuanzia mwaka huu wa fedha na kinachotakiwa ni kuorodhesha bili zote zinazostahili.
Wakazi wa kata ya Kimara, Dar es Salaam waliandamana pembeni mwa barabara kuu ya Morogoro wakiwa na ndoo na madumu matupu ya maji wakilalamikia shida ya maji  na kushutumu bei kubwa ya maji  kutoka kwa wafanyabiashara.
Maandamano hayo yalihusisha wanawake na watoto waliokuwa wakiimba, inadaiwa yalikuwa yakielekea nyumbani kwa Waziri wa Maji, Profesa Maghembe.  “Tunataka maji yashuke bei... tunateseka hivi hadi lini? Ndoo ya maji Sh 600, tunateseka,” walisikika wakiimba.
Ililazimu magari kusimama kwa dakika kadhaa kupisha maandamano hayo yaliyokuwa yakitoka Kimara Stop Over kwenda Kimara Mwisho.
“Wananchi wamedhamiria kuja kulala kwangu, lakini kwa kuwa sitakuwa na uwezo wa kuwahifadhi wote, itabidi tutafute nyumbani kwa Profesa Maghembe ili waende kueleza shida zao huko,” alisema Diwani wa Kimara, Pascal Manota.

No comments: