WALIMU KUCHUNGUZWA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE...

Dk Shukuru Kawambwa.
Wakati Waziri Mkuu akiwa ametangaza kuunda tume ya kuchunguza matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne, imeelezwa kwamba kutafanyika uchunguzi kila shule, kwa kuangalia walimu wa masomo, ambayo wanafunzi wamefaulu na wamefeli.
Taarifa hiyo ilitolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha sita ya Shule ya Sekondari ya Ali Hassan Mwinyi Elite, Dar es Salaam yaliyofanyika juzi.
 “Tunataka kuangalia shule moja baada ya nyingine kwa kuangalia walimu wa masomo hayo ambayo wanafunzi wao wamefeli na wale waliofaulu katika somo husika, pia tunataka kuangalia ni kwa nini masomo ya Sayansi wamefaulu kuliko Civics  na Historia,” alisema Dk Kawambwa.
Alisema pamoja na walimu na wazazi kuwa na nafasi katika kuepuka matokeo mabaya, serikali imeona ni vyema itafute mzizi wa tatizo kwa kufuatilia upande wa walimu.
Alitoa mfano, “nilikutana na kiongozi wa Malaysia aliniambia kuwa tatizo lililotukuta, hata wao liliwakuta.”
Kwa mujibu wa Kawambwa, kiongozi huyo alimwambia Serikali ya nchi hiyo ilichokifanya, ilikuwa ni kuwafanyisha mtihani walimu wote.
Alisema serikali hiyo ilifikia muafaka na chama cha walimu, wakaona waliofeli watengewe darasa lao.
Ingawa Dk Kawambwa hakufafanua zaidi kama pia Serikali inataka ifuate mkondo wa Malaysia wa kuwafanyisha walimu mtihani, alisisitiza kwamba jambo la msingi ni kuangalia kiini cha tatizo.
Alisema, “kwa mfano tukiangalia somo la Jiografia, kila shule tutamwangalia mwalimu wake ambaye wanafunzi wake wamefeli na wale ambao wanafunzi wake wamefaulu.”
“Pamoja na wanasiasa wa bei nafuu kutaka nijiuzulu, hawajui nje ya uwaziri nina maisha mengine, naweza kurudi kulima mihogo… Jambo la msingi ni kuangalia kiini cha tatizo hili,” alisema.
Alisisitiza kiwango cha ufaulu na kuongezeka kwa waliofeli, kimekuwepo kwa kipindi cha miaka mitatu tangu mwaka 2010 katika shule za serikali, binafsi na  seminari.
Alitoa mfano wa kushuka kwa ufaulu kwa shule binafsi, kwamba mwaka 2010 waliopata daraja la kwanza ni  watahiniwa 4,276, sawa wa asimilia 4.8 na kwamba mwaka uliofuata, idadi ilishuka na kufika 1,614 sawa na asilimia 2.8.
Aidha matokeo mwaka 2012, yanaonesha ufaulu umeshuka tena, ambapo waliopata daraja la kwanza ni 1,032 sawa na asilimia 1.6.
Kwa upande wa shule za seminari, alisema mwaka 2010 wanafunzi 695 sawa na asilimia 14.3 walipata daraja la kwanza. Hata hivyo, idadi ilishuka mwaka uliofuata hadi 428 sawa na asilimia 7.9. Mwaka 2012 imeendelea kushuka hadi watahiniwa 197 sawa na asilimia 3.3.
Wakati tume iliyoundwa na Waziri Mkuu haijafahamika wajumbe wake, vile vile hazijawekwa hadidu rejea zitakazozingatiwa katika kazi yake itakayoanza wakati wowote kuanzia sasa. 
Tume hiyo inajumuisha wadau kutoka Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco), taasisi za dini zinazotoa huduma ya elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Asasi Zisizo za Serikali (Azise) zinazoshughulikia elimu.   
Wajumbe wengine watatoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa).
Akizungumza na mwandishi jana, Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema chama chake hakiko tayari kuwa sehemu ya tume hiyo, kwa kile wanachoamini kwamba matatizo yanayoikabili sekta ya elimu, yanajulikana.
“Hatuko tayari kuwa sehemu ya hiyo tume, tunasubiri watupe barua ili tuwajibu kuwa matatizo yaliyofanya wanafunzi kufeli, wanayajua,” alisema.
Mukoba aliongeza kuwa, “Serikali isipoteze muda na rasilimali ambazo inaweza kuzitumia maeneo mengine kwa sababu matatizo ya sekta ya elimu wanayajua. Tumeshawahi kufanya vikao na Waziri Mkuu, Rais na hata waziri wa elimu. Hii ni sawa na kumtafuta paka mweusi kwenye chumba cha giza.”
Mwenyekiti wa  Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye hivi karibuni alikuwa miongoni mwa waliotaka Rais aunde tume kuchunguza mfumo wa elimu, alisema tume iliyoundwa kuchunguza matokeo ni sawa na  tone katika bahari.

No comments: