CHUO CHAFUNGWA KWA KULEA WATOTO WASIOJULIKANA...

Stella Manyanya.
Kuibuka kwa biashara ya binadamu kunakoendelea kuimarika duniani, kumemtia shaka Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya na kuonya taasisi zinazochukua watoto na kuwalea bila taarifa zao kufahamika.
Manyanya alitoa onyo hilo juzi kutokana na taarifa ya kuwapo kituo cha elimu na malezi ya Kiislamu cha Nourul Hudaa Islamic Center Muzdalifa (MICO) kilichoko mjini  hapa licha ya kuwa hakipo kisheria,  lakini hata orodha ya watoto wanaolelewa hapo  haifahamiki.
Pia viongozi wanaoendesha kituo hicho hawafahamiki huku daftari linaloonesha watoto hao wanakotoka au taarifa za wazazi wao halipo.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa  alilazimika kutengua uamuzi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Sumbawanga iliyoamuru kufungwa kituo cha  MICO baada ya  kushindwa kukidhi vigezo muhimu ikiwa ni pamoja na kutosajiliwa.
Manyanya alifikia uamuzi  huo  jana jioni baada  ya  watoto 190 na walimu wao   wawili,  Hamisi Matope na Ustaadh Idrisa Majundo kutoka kituo hicho kilichopo  eneo la Nelson Mandela mjini hapa, kuandamana hadi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ili waonane naye.
Akimweleza Mkuu wa Mkoa katika kikao cha dharura kilichofanyika katika  jengo  la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Salum Chima, mmoja wa walimu wa kituo hicho Matope alidai walilazimika kuwapeleka watoto hao ili Mkuu wa Mkoa  awape  malazi, kwa kuwa kituo  chao kimeamriwa  kufungwa  na  Manispaa  ya Sumbawanga.
“Tumeamriwa kufunga kituo  chetu na  watoto  warudishwe kwao  hadi kitakapokidhi  hadhi ya kuwa chuo, sasa tumewaleta  watoto  hawa kwa Mkuu wa Mkoa, ili awape malazi  hadi watakapoweza kurejeshwa kwao, kwa kuwa sasa  hawana pa kulala,“ alisema Matope.
Watoto hao kwa mujibu  wa Majundo baadhi yao ni yatima kutoka sehemu mbalimbali za  Mkoa wa Rukwa na mikoa  ya jirani ya Mbeya, Katavi na Kigoma, ambapo baadhi yao wanasoma shule za msingi na sekondari mjini hapa.
Wengi  wao hawakuwa tayari kuzungumza na  mwandishi wa habari  hizi  kwa kile walichodai kuwa wamekatazwa na walimu wao kusema lolote kuhusu malezi yao.
Hata hivyo,  mtoto aliyejitambulisha kwa jina la Maka Salumu (15) wa Kigoma,  alionesha ujasiri na kudai kuwa waliandamana ili kumshinikiza Mkuu wa Mkoa  awape malazi  na chakula, hadi  watakaporejea kwao kwani kituo chao  kimefungwa kwa amri ya Manispaa.
“Mtoto mdogo miongoni mwetu ana umri wa miaka saba, miye nililetwa kituoni na  bibi  yangu  nikitoka Kigoma, sasa kimefungwa hatuna pa kulala, hivyo tumekuja  hapa  ikiwezekana tulale hapa hapa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, hadi  tutakaporejeshwa  kwetu,“ alisema Salumu.
Katibu Tawala wa Mkoa, Chima alifafanua sababu za kufungwa kwa kituo hicho.
Alisema watoto katika kituo hicho walikuwa wakikabiliwa na kadhia mbalimbali zikiwamo za kulala chini sakafuni huku sakafu hiyo ikiwa na imelowa maji hata kwa waliokuwa  wagonjwa, kushinda na njaa.
Licha ya kuwa kituo hicho hakijasajiliwa lakini watoto hao walikuwa hawana sehemu ya kupikia, huku majengo ya kituo hicho yakiwa chakavu na yasiyofaa kabisa kwa matumizi  ya binadamu, kwani  hata vyumba vya kulala watoto hao sakafu zina mashimo.
“Miye binafsi nilishafika kituoni hapo, pamoja na matatizo hayo pia hakijasajiliwa, hivyo hakipo kisheria na hata utunzaji kumbukumbu zake si mzuri kwani hakina hata daftari la orodha ya watoto hao sambamba na kuwa hata idadi yao haijulikani pia  viongozi wanaongoza kituo  hicho hawafahamiki kabisa,“ alisema Chima.
Ndipo Manyanya licha ya kuwashukuru kufanya maandamano ya  amani, pia aliagiza  wapewe miezi miwili zaidi ili waboreshe  upungufu uliojitokeza.
Pia alimwagiza Chima afanye ukaguzi wa mara kwa mara katika  kituo  hicho, ili kuhakikisha kama upungufu uliojitokeza umerekebishwa na kuboreshwa  pia wapewe wataalamu watakaowasaidia kuhakikisha  kinasajiliwa kisheria.
“Lazima idadi na majina na wanakotoka ifahamike, si sahihi kulea watoto ambao  hawafahamiki wazazi  wao  wako  wapi  lazima na watoto  wenyewe  wafahamishe  walipo  wazazi wao,“ alisisitiza.

No comments: