PENGO AKATAZA WAKRISTO KULIPIZA KISASI...

Askofu wa Zanzibar akitoa heshima zake za mwisho kwa mwili wa Padri Evarist Mushi, jana.
Askofu Mkuu, Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ametaka Watanzania kujenga tabia ya kuvumiliana katika masuala yanayotofautiana, zikiwamo imani za kidini.
Aidha, ametaka wafuasi na waumini wa dini ya Kikristo kuishi na wenzao vizuri bila kulipiza kisasi kama yalivyo maandiko matakatifu kwenye Biblia. 
Alisema hayo jana katika maziko ya Padri wa Kanisa la Minara Miwili, Evarist Mushi aliyeuawa Jumapili kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana, wakati akienda kanisani kuendesha misa katika Kanisa la Mtakatifu Terezia Mtoni nje kidogo ya mji wa Unguja.
Mamia ya wananchi, viongozi wa dini na vyama vya siasa wakiongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein  walihudhuria misa ya maziko ya Padri Mushi katika Kanisa la Minara Miwili.
Akiongoza misa ya kumwombea marehemu katika kanisa hilo lililoko Mji Mkongwe, Pengo alisema: “Katika kujenga Taifa lenye umoja na mshikamano, tunahitaji kuwa na uvumilivu katika imani za kidini na kuheshimiana”.
Alisema hiyo ndiyo misingi muhimu ya kuishi vizuri ambayo iliasisiwa na viongozi wa Taifa hili baada ya uhuru wa Tanganyika na Zanzibar.  Akiongoza sala ya mwisho katika eneo la kaburi kwa niaba ya viongozi wengine wa dini, Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Anthony Banzi alisisitiza uvumilivu akiwataka Wakristo kuishi na wenzao wenye itikadi tofauti ya dini bila matatizo.
“Adui mpende lakini maisha ya binadamu yana thamani kubwa, kwa hivyo tuepuke ukatili,” alisema.
Jeneza lenye mwili wa marehemu Mushi lilibebwa na maaskofu na kusogezwa karibu na eneo la kaburi katika kijiji cha Kitope mkoa wa Kaskazini Unguja eneo maalumu wanalozikwa mapadri.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein alifika katika Kanisa la Minara Miwili kuaga na kusaini kitabu cha waombolezaji.
Alishiriki maziko hayo kwa kuweka udongo na shada la maua kwenye kaburi, akifuatiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Akitoa salamu za SMZ, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema Serikali imesikitishwa na mauaji hayo.
Alisisitiza kwamba Serikali itafanya uchunguzi wa kina hadi wahusika watiwe mbaroni.
“Tunawaomba waumini wa kikristo na ndugu na jamaa wa marehemu kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba...Serikali inafanya uchunguzi wa tukio hilo,” alisema.
Mwakilishi wa Ubalozi wa Vatican nchini, Balozi Askofu  Fransisco Padilla katika salamu zake, alisema amepokea taarifa za kifo cha Padri Mushi kwa mshituko mkubwa na hakuamini.
“Nilipokea taarifa za kifo cha Mushi kwa mshituko mkubwa bila kuamini...kifo kimeumbwa, lakini kinauma sana katika mazingira kinapotokea,” alisema Padilla.
Mwakilishi wa familia ya marehemu,  Francis Mushi ambaye alifuatana na ndugu wa karibu,  alisema kila nafsi itaonja mauti, lakini akataka binadamu waache kufanya ukatili.
Alimtaja ndugu yao kuwa, ndiye aliyekuwa msaada mkubwa katika kuendeleza maisha yao licha ya kwamba walikuwa wakiishi mbalimbali.
Maziko ya Padri Mushi yalihudhuriwa pia na viongozi wa vyama vya siasa akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia pamoja na mabalozi mbalimbali.
Ulinzi uliimarishwa katika maeneo ya Mji Mkongwe hasa eneo la Kanisa Kuu la Katoliki Shangani na  vichochoro jirani na eneo hilo sawa na ilivyokuwa katika eneo la makaburi ya Kitope. 
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga limeomba Idara ya Usalama wa Taifa kwa kushirikiana na vyombo vingine, wafanye uchunguzi wa kina kubaini wanaoendeleza hujuma dhidi ya viongozi wa dini na mali za madhehebu hayo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Theresia Msuya katika kikao maalumu cha Baraza hilo, alieleza hofu ya kuwapo mtandao wa watu wenye lengo la kuchochea vurugu za kidini nchini, kwa maslahi yao jambo ambalo litaathiri umoja wa kitaifa uliopo.
Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi alitaka viongozi wa dini zote nchini kutafuta njia mpya za ushirikiano zitakazosaidia kudhibiti sababu zinazovuruga amani nchini.
Alitoa mwito huo Dar es Salaam katika  mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Mashekhe na Wanazuoni wa Kiislamu kwa lengo la kuzungumzia utulivu na amani ya Taifa.
Mwinyi ambaye pia ni mlezi wa Taasisi hiyo, alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa kuzuia mambo mabaya katika jamii.
Bingwa wa kimataifa wa  masuala ya amani, Dk Abdalla Omar Naseef aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alisema ni vyema waumini wa dini zote wakaheshimiana na  kudumisha amani iliyopo kwa kuwa ndiyo misingi iliyowekwa na Mwenyezi Mungu kwa kila mwanadamu.
Wakati huo huo, Rais wa Wapo Mission International, Askofu Sylvester Gamanywa alisema kila mmoja ana haki ya kuabudu na kwamba tofauti zinazojitokeza sasa hazina msingi wowote na zimelenga kuchafuana na kubaguana kwa misingi ya kidini.
Alisema mkutano huo unaonesha ni namna gani viongozi wa dini wanaweza kukaa pamoja na kujadili tatizo linalojitokeza. Alitaka wanaoeneza chuki kwa misingi ya dini kuacha tabia hiyo.

No comments: