PADRI EVARIST MUSHI KUZIKWA KESHO ZANZIBAR...

KUSHOTO: Gari alilokuwa akiendesha Padri Mushi siku ya tukio. KULIA: Marehemu Padri Evarist Mushi.
Padri Evarist Mushi (55), aliyeuawa juzi kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Zanzibar, anatazamiwa kuzikwa Kitope katika eneo lililotengwa la makaburi ya mapadri.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Zanzibar, Augostino Shao, alisema maandalizi ya maziko yanaendelea vizuri.
“Tunatarajia kuupumzisha mwili wa marehemu Mushi katika makaburi ya Kitope ambako kuna sehemu maalumu ya kuzikwa mapadri,” alisema.
Marehemu Mushi atakuwa padri wa tatu kuzikwa eneo hilo mkoani Kaskazini Unguja, ambako alisema kwa sasa ni mapema kujua viongozi watakaohudhuria maziko.
Akielezea kifo cha Padri Mushi, alisema kimeacha pengo  katika Kanisa hilo, alikokuwa akijishughulisha na masuala ya kukuza maendeleo ya elimu.
“Unajua marehemu alikuwa msomi aliyebobea katika elimu na mambo ya mitaala ya wanafunzi...hapa kanisani tulimweka katika kitengo cha maendeleo na kukuza elimu kwa watumishi,” alisema.
Akielezea jinsi alivyopokea taarifa ya kifo cha Padri Mushi, ambaye alikuwa msaidizi wake mkuu, Askofu Shao alisema alipokea wakati akiendesha ibada ya kawaida ya Jumapili katika Kanisa la Minara Miwili.
“Nilikuwa naongoza ibada, lakini wenzangu tayari walikuwa wamepata taarifa ya kifo cha Padri Mushi. Nilikuwa naye asubuhi saa 12 tukaagana,  naye akaenda kuongoza misa Mtoni katika Kanisa la Beit-el-Ras,” alisema.
Askofu Shao alivitaka vyombo vya ulinzi, kufanya kazi za kusaka wahalifu kwani jamii tayari imeanza kupoteza imani. 
Padri  Mushi aliuawa  kwa risasi tatu alizopigwa kichwani na watu wasiojulikana juzi saa moja asubuhi, akienda kanisani kuongoza ibada.
Akiwa katika gari lake aina ya Toyota Hilux Surf, Padri Mushi alipigwa risasi kichwani kupitia dirisha la mlango wa kulia.
Mauaji hayo yalifanyika wakati akikata kona kuingia kanisani, ambako watu hao walikuwa wakimsubiri wakiwa na usafiri wa Vespa na baada ya kumpiga risasi walikimbia.
Kutokana na hali hiyo, gari la Padri Mushi lilipoteza mwelekeo na  kupamia ukuta wa nyumba iliyo meta chache kutoka Kanisa la Mtakatifu Theresia, ambako alikuwa akienda.

No comments: