MTOTO WA ASKOFU LAIZER AMWOMBEA MSAMAHA BABA YAKE...

Marehemu Askofu Thomas Laizer.
Mtoto wa marehemu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laizer, Ezra Laizer amewasihi waumini wa Kanisa hilo kumsamehe baba yao kwa mabaya aliyoyafanya kama yapo na kuendeleza mazuri aliyotenda katika uhai wake.
Hayo aliyasema jana nyumbani kwao Nduruma, Arumeru,  akiwa na familia ya Askofu pamoja na ndugu na jamaa.
Alisema ingawa kifo ni kifo lakini kuondokewa na mzazi inauma sana, “lakini kikubwa baba yetu  alikuwa kiongozi wa watu wengi, hivyo kama binadamu alitenda mambo mengi mazuri, lakini jambo moja baya lisichukuliwe na kuwa ndilo hilo tu alilotenda".
Pia aliongeza kuwa Mungu akipanga kitu amepanga hakuna anayeweza kupangua mipango yake.
“Kuondokewa  na baba yetu ni pigo kubwa kwetu na familia kwa jumla, tunaomba kama kuna mabaya aliyotenda watu wasamehe, sababu huyu naye alikuwa binadamu na si mkamilifu na wayaendeleze mazuri mengi aliyotenda, ambayo mwenyewe alitamani sana yafikishwe mwisho wake,” alisema.
Mke wa marehemu, Maria Laizer alisema mumewe alianza kuhisi mwili una shida siku nyingi baada ya kutokewa na tezi upande wa kushoto.
Alisema alihangaika sana kuchunguzwa katika kila hospitali, lakini aliambiwa haina shida na hana tatizo lingine, alikaa ikapita miaka 10 na ilipofika mwaka 2010 akazidiwa na kupelekwa hospitali ya Selian ya Dayosisi hiyo na kugundulika kuwa tezi ina tatizo ambalo alishauriwa apelekwe Nairobi.
“Tulipokwenda Nairobi, tukaelezwa tatizo ni  kubwa tunatakiwa kwenda India na fedha iliyokuwa inahitajika kubwa, hivyo tuliomba michango na watu wenye mapenzi mema walitupa, kisha Septemba mwaka jana tulikwenda India kwa matibabu,” alisema.
Baada ya uchunguzi India, iligundulika kuwa tezi hiyo imesababisha saratani na kufanya tumbo kujaa maji na kushindwa kuhema, lakini aliendelea na matibabu siku hadi siku, hadi alipolazwa Selian hadi mauti yalipomfika jana jioni.
“Lakini juzi alidhoofu sana, alishindwa  hata kuhema, nashukuru viongozi wa Serikali, wanasiasa na wa dini walifika kutufariji, pia nashukuru watu mbalimbali waliokuwa wakisali kwa ajili ya baba,’’ alisema.
Kwa mujibu wa mjane huyo, enzi za uhai wake walijaliwa kupata  watoto watano na mmoja kufariki dunia na kubaki wanne, ambapo mtoto wa kike ni mmoja na wa kiume watatu pamoja na mjukuu.
Wakati huo huo, kifo cha Askofu Laizer kimemliza Rais Jakaya Kikwete. Kwa mujibu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, baada ya kupokea taarifa za kifo hicho juzi, Rais katika kuonesha huzuni yake, alituma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa KKKT, Askofu Mkuu Dk Alex Malasusa kuombeleza kifo hicho.
Katika salamu zake, Rais Kikwete alimwambia Askofu Mkuu Malasusa: “Nimepokea kwa mshituko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Askofu Laizer ambaye nimejulishwa kuwa ameaga dunia muda mfupi uliopita, jioni ya leo (juzi), katika hospitali ya rufaa ya Selian, Arusha.”
“Askofu Laizer ametutoka lakini tutaendelea kumkumbuka kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi wa kiroho wa Watanzania na ambaye wakati huo alitafuta namna bora zaidi ya kutumikia waumini wake.
“Daima atakumbukwa kama kiongozi ambaye alitumia vipaji vyake vyote kutumikia waumini wake na wote waliokuwa chini yake,” alisema Rais.
Ameongeza kuwa: “Kutokana na msiba huu mkubwa, nakutumia wewe Baba Askofu Mkuu Malasusa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu, kukupa pole ya msiba huu na kupitia kwako kuwapa pole nyingi maaskofu na viongozi wenzako katika KKKT pamoja na waumini wote wa Kanisa, kwa kuondokewa na kiongozi mwenzao na muumini mwenzao.”
Aidha, Rais Kikwete alituma salamu kwa familia na wana-ndugu wa marehemu Laizer.  “Naungana nao katika kuomboleza. Naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na baba, babu na mhimili wa familia.
“Nawaombea subira ili waweze kuvuka kipindi hiki kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aiweke pema peponi roho ya marehemu Laizer.”

No comments: