MLINZI WA MTUME MWINGIRA WA EFATHA AUAWA...

Josephat Mwingira.

Mlinzi wa shamba la mifugo la Shirika la Efatha Ministry linaloongozwa na Joseph Mwingira, ameuawa na wengine wawili kujeruhiwa baada ya wananchi kuwavamia wilayani Sumbawanga. 
Wakazi zaidi ya 200 wa Kijiji  cha Sikaunga wilayani Sumbawanga mkoani  Rukwa  walivamia shamba hilo la Malonje, wakawashambulia walinzi 10  na kumuua mmoja na wengine wawili walijeruhiwa vibaya. 
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Peter Ngusa  ambaye pia  ni Ofisa  Upelelezi  wa Mkoa  amethibitisha kuwepo tukio hilo jana. 
Kwa mujibu wa Ngusa  mwili wa mlinzi huyo  umehifadhiwa  katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa  Rukwa mjini  Sumbawanga  kusubiri uchunguzi  wa kitabibu  ambapo  majeruhi  wawili  wamelazwa  katika hospitali hiyo  kwa matibabu  huku  hali  zao  zikielezwa kuwa  tete.
Jina la marehemu halikuweza kufahamika mara moja . Mmoja wa majeruhi ni  Briton Ngimili. Kaimu Kamanda alisema hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na  kisa hicho. Polisi inasaka wahusika wa vurugu hizo. 
Akisimulia mkasa  huo Ngusa alisema uvamizi  huo  unatokana na kuwepo   mgogoro  wa ardhi  wa muda mrefu  kati ya mwekezaji, Efatha Ministry na wanakijiji wa Sikaunga. 
“Tulipata  taarifa  za vurugu hizo jana  na tulipofika huko  tulikuta tayari  walinzi  wawili  wa shamba  hilo wakiwa  wamejeruhiwa na kuhifadhiwa  ndani ya ofisi  kijijini  hapo  hivyo walikimbizwa haraka  katika Hospitali  ya Mkoa mjini hapa ambako wamelazwa kwa matibabu,” alisema.
Alisema baada  ya msako  wa muda mrefu  ndipo  polisi waligundua mwili wa mlinzi  anayedaiwa  kuuawa kikatili  na  wanakijiji  hao. 
Mlinzi wa shamba hilo, Ngilimi  aliyelazwa kwa matibabu alidai kuwa  kabla ya kutokea vurugu  hizo   kundi dogo la  wakazi  wa kijini hapo  walivamia  eneo la  shamba  hilo.
Alisema walipohojiwa na  walinzi wa shamba  hilo, wanakijiji hao walianza kuwasiliana kwa simu  na  wenzao huku wakipuliza  filimbi. Kundi  kubwa la  watu wakitokea kijijini walivamia shamba na walinzi kwa silaha. 
Meneja  wa Shamba hilo , Peter Kibona  alidai  kikundi  cha  watu hao  wanaokadiriwa kufikia  200  kutoka Kijiji hicho cha Sikaunga  wakiwa na  silaha  mbalimbali za jadi  zikiwemo marungu , mapanga na fimbo  waliwashambulia  walinzi  hao 10 waliojaribu  kuwatoa  wanakijiji  kwa kuingia shambani bila kuwa na vitambulisho.
Kibona  alisema walinzi  hao  walipewa maagizo ya kuwatishia wakazi  hao   kwa kupiga risasi  juu  ndipo  walipoanza kushambuliwa  kwa  silaha hizo za  jadi na kusababisha  kifo  cha mmoja wao .
“ Tuliwakataza kabisa walinzi wetu wasiwafyatulie risasi  wanakijiji  hao waliovamia shambani bali wafyatue  hewani  na ndivyo walivyofanya,” alisema. 
Shamba hilo la Efatha linadaiwa kuwa na ukubwa wa hekta 10,000. Mgogoro baina ya wanakijiji na mwekezaji ni wa muda mrefu. 

No comments: