Mahakama ya Mwanzo mjini Sumbawanga, imemtia hatiani aliyekuwa Sista wa Shirika la Kitawa la Kanisa Katoliki, Jimbo la Sumbawanga, Yasinta Sindani, kwa kufumaniwa na mume wa mtu.
Kutokana na kutiwa hatiani, Yasinta aliamriwa kumlipa fidia ya kimila ya Sh 700,000, malalamikaji, Asteria Mgabo.
Katika kesi hiyo ya msingi ya madai, Asteria alikuwa akimtaka mshitakiwa alipe Sh milioni 3 ya fidia, baada ya kumfumania na mumewe wa ndoa, Martin Msangawale (39), ambaye pia ni mkazi wa mjini hapa.
Mshitakiwa huyo ambaye ni mtumishi katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa, kwa sasa anaishi nje ya nyumba ya utawa, eneo la Kantalamba mjini hapa.
Inadaiwa mshitakiwa ambaye alikuwa mtawa wa Shirika la Masista wa Maria Mtakatifu Malkia wa Afrika (MMMA), ameachana na maisha ya kitawa miaka miwili iliyopita kwa hiyari yake mwenyewe.
Katika hati ya awali ya madai, mshitakiwa alikuwa akidaiwa kufumaniwa na Asteria akiwa na mumewe Msangawale katika nyumba ya kulala wageni ya Chipa iliyoko eneo la Katandala mjini Sumbawanga, usiku wa Desemba 24 mwaka jana, siku ya Mkesha wa Sikukuu ya Krismasi.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Jaffar Mkinga, alisema ushahidi uliotolewa na mlalamikaji, ulikuwa mzito wenye kuondoa shaka zote kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo, tofauti na utetezi uliotolewa na mdai kwamba ushahidi ulikuwa dhaifu.
Katika utetezi wake, mshitakiwa aliiambia mahakama hiyo kuwa kwanza alikuwa hajui kuwa Martin alikuwa mume wa mtu. Alidai kuwa pia mwanamume huyo, alimweleza kuwa hana mke na alimwomba wafunge ndoa.
Lakini Hakimu Mkinga alipinga na utetezi huo kwa sababu siku hiyo ya Mkesha wa Krismas, mwaka jana saa saba na robo usiku, mlalamikaji akiongoza na Mwenyekiti wa Mtaa na mashahidi wengine watatu, walimfumania mshitakiwa akiwa na Martin.
Alisema mdai na mashahidi hao, walimfumania mshitakiwa na Martin wakitoka katika moja ya vyumba vya kulaa katika nyumba yakulala wageni ya Chipa, iliyopo katika eneo la Katandala mjini hapa.
Kwa mujibu wa Hakimu Mkinga, baada ya kufumaniwa mshitakiwa na Martin walipokubali kusaini karatasi ya ya fumanizi ya ugoni, iliyoaandaliwa na Mwenyekiti huyo wa mtaa.
“Hivyo kama mshitakiwa ulikuwa haufahamu kuwa Martin alikuwa hana mke, ilikuwaje ukakubali kusaini karatasi hiyo ya fumanizi iliyoandaliwa na Mwenyekiti huyo?” Alihoji.
Hata hivyo alisema kutokana na Sheria ya Ndoa na Mirathi ya 1971, faini ya fumanizi la ugoni si adhabu, inapaswa itolewe kulingana na mila na desturi za eneo la tukio.
Kutokana na sheria hiyo, Hakimu Mkinga alimuamuru mshitakiwa kulipa mara moja faini ya fumanizi la ugoni ya Sh 700,000 kwa mlalamikaji.
“Mlalamikaji alimtaka mshitakiwa alipe Sh milioni 3 kwa ajili ya fumanizi la ugoni, kiasi hicho si tu ni kikubwa, lakini pia ni adhabu.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa na Mirathi ya 1971, faini ya fumanizi la ugoni, haipaswi kuwa adhabu kwani inatatozwa kulinga na mila na desturi za mahali husika.
“Wafipa faini ya ugoni ni ng’ombe wawili ambao thamani yake ni Sh 600,000, mshitakiwa unaamriwa na Mahakama umlipe mara moja mlalamikaji Sh 700,000 ikiwa ni faini ya fumanizi la ugoni,“ alisema Hakimu Mkinga.
Akizungumza nje ya chumba cha Mahakama mara baada ya kusomwa kwa hukumu, Asteria alikiri kuwa hukumu iliyotolewa, ameridhika nayo. Aidha alisema amedhamiria kufungua shauri lingine mahakamani hapo, kudai talaka.
“Baada ya hukumu hii, kesho nitaanza mchakato wa kufungua shauri mahakamani hapa kudai talaka kwani siko tayari tena kuendela kuishi na Martin,“ alisisitiza.
Wakati hayo yakijiri ndani Mahakama hiyo, Martin alivyokuwa akijiandaa kuingia ndani, ghafla alizuiwa na kuwekwa chini ya ulinzi Mahakamani hapo.
Mwanasheria wa Manispaa ya Sumbawanga, Tulalemwa Mwenda alithibitisha kukamatwa kwa Martin, akituhumiwa kujifanya Ofisa Ardhi wa Manispaa hiyo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
“Tumekuwa tukimtafuta kwa muda mrefu, sasa leo tumepata. Amekuwa akijifanya Ofisa wa Manipaa, mara mhasibu na sasa anajifanya Ofisa Ardhi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,“ alidai Mwenda.
Kwa mujibu wa madai ya Mwenda, Martin awali alikuwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji, lakini baadaye alifukuzwa kazi na kwa muda mrefu amekuwa akitapeli wakazi wa manispaa hiyo, akijifanya kuwa Ofisa Ardhi Mwandamizi.
No comments:
Post a Comment