ASKOFU THOMAS LAIZER KUZIKWA LEO ARUSHA...

Marehemu Askofu Thomas Laizer.

Rais Kikwete leo anatarajiwa kushiriki katika maziko ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Thomas Laizer. 
Askofu Laizer anatarajiwa kuzikwa leo katika Kanisa Kuu la Usharika wa Mjini Kati, uliopo katikati ya Jiji la Arusha. 
Waumini wa Kanisa hilo na wananchi wa Arusha tangu jana walianza kuuga mwili wa Askofu Laizer katika Kanisa Kuu la KKKT la Usharika wa Mjini Kati uliopo Barabara ya Goliondoi, sehemu ambayo imetengwa kwa ajili ya maziko. 
Askofu Laizer alifariki Alhamisi ya wiki iliyopita, katika Hospital ya Rufaa ya Seliani, inayomilikiwa na Kanisa hilo alikokuwa amelazwa kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu, akisumbuliwa na saratani.  
Miongoni mwa wageni wanaotarajiwa katika maziko hayo mbali na Rais Kikwete ni Mwinyi na Mkapa. Wengine ni waaliokuwa mawaziri  wakuu, Fredrick Sumaye na Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli mkoani Arusha.
Barabara za Goliondo, India na nyinginezo zilizoko karibu na kanisa hilo, huenda zikafungwa ikiwa ni njia mojawapo ya kuondoa msongamano wa magari kabla na wakati wa mazishi.  
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Dk Alex Malasusa, aliwasili Jijini Arusha tangu Jumamosi ya wiki iliyopita na Msaidizi wa Askofu, Solomoni Massangwa, alikaimishwa rasmi Uaskofu wa Dayosisi hiyo Jumapili iliyopita.

No comments: