WALIOIBA MILIONI 500/- KWA ATM WAKUTWA NA KADI BANDIA 231...


Polisi mkoani Mwanza, inawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuiba fedha kwa kutumia kadi za ATM, kwenye akaunti za wateja katika benki mbalimbali hapa nchini.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kuiba takribani Sh milioni 500 kuanzia Oktoba mwaka 2012, hadi walipokamatwa.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Christopher Fuime, Februari 10 mwaka huu, saa sita usiku, mtuhumiwa mmoja alikamatwa akiiba fedha za wateja katika benki ya NMB tawi la PPF Plaza.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Salim Nassoro mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, Maniki Kimani na Leonard Masunga ambao ni ndugu na wakazi wa Nyegezi jijini Mwanza.
Alisema baada ya kukamatwa usiku huo, siku iliyofuata mtuhumiwa huyo, aliwapeleka askari Polisi walipo wenzake na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine wawili pamoja na vifaa mbalimbali vya kutengenezea kadi feki, wanazotumia kuibia wateja wa benki.
Alisema walipopekuliwa, walikutwa na kadi takribani 231 za benki mbalimbali, zikiwemo kadi 194 za wateja wa benki ya NMB, kadi 36 za wateja wa Diamond Trust Bank (DTB), kadi moja ya KCB na kadi 18 zisizo na nembo.
Pia watuhumiwa hao walikutwa na kompyuta ndogo za mkononi (laptops) tatu, printa, vifaa vya kutengeneza kadi feki, kamera ya kuchukua picha kwa siri na rangi makopo matatu wanazotumia kupulizia kwenye kamera zilizoko katika ATM, ili sura zao zisionekane.
Pia watuhumiwa hao walikutwa na madaftari matatu aina ya ‘counter book’, ambayo yalikuwa yameorodheshwa namba za siri za wateja mbalimbali, ambao taarifa zao zilikuwa zimenaswa kwa kutumia vifaa maalumu walivyokuwa wanavibandika kwa siri, katika mashine za ATM.
Kamanda Fuime alisema kwa kutumia zana hizo, watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti hususani usiku, wamekuwa wakienda katika mashine za ATM na kuchukua fedha kutoka kwenye akaunti mbalimbali.
Fedha hizo wamekuwa ‘wakizichota’ kwa kutumia kadi walizozitengeneza wao wenyewe na   taarifa za wateja zilizokusanywa na vifaa maalumu. 
Fuime alisema watuhumiwa walikutwa pia na vifaa vingine vya kielektroniki, ambavyo havikutambuliwa kwa urahisi, hadi pale vitakapopelekwa makao makuu ya uchunguzi wa wizi kwa njia ya mtandao na kemikali ambazo zitapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya utambuzi. 
Alisema walipohojiwa watuhumiwa hao, walikiri kuhusika na wizi wa fedha katika mashine za ATM na wanafanya wizi huo kwa kushirikiana na wazungu watatu, raia wa Bulgaria ambao ndio mafundi wa kutengeneza zana wanazotumia kuiba. 
Kaimu Kamanda huyo alisema Polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

No comments: