LOWASSA ANG'OLEWA UDHAMINI UMOJA WA VIJANA CCM...

Edward Lowassa.
Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ameenguliwa katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Mali za Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Baada ya kuenguliwa huko, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo.
Akitangaza uteuzi huo jana, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema uteuzi huo umezingatia mabadiliko yanayotokea ndani ya chama na wameamua kuingiza nguvu nyingi ya vijana.
Lowassa pamoja na wajumbe wengine wa Baraza hilo wamekuwa katika nafasi hizo kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo.
Wajumbe wengine walioachwa ni pamoja na Nadhir Karamagi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji Dk Mary Nagu, Yusuph Ahmad Yusuph na Said Aboud.
Hata hivyo, mtu aliye karibu na Lowassa ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema Waziri Mkuu huyo  wa zamani amemaliza muda wake wa uongozi katika Baraza hilo na si kwamba ameenguliwa. Alisema alishika uongozi huo kwa vipindi vitatu mfululizo.
Shigela alitaja wajumbe wapya kuwa ni Machano Othman Saidi ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.
Wengine ni William Lukuvi (ambaye alikuwamo katika Baraza lililopita), Profesa Anna Tibaijuka, Janeth Mbene, Hamad Masauni na Mohamed Aboud.
Wajumbe wa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Baraza  hilo kutoka Tanzania Bara ni Daud Njali, Ruben Sixtus, Seki Kasuga, Amini Mkalipa na Mariam Chaurembo.
Kutoka Zanzibar ni Shaka Shaka, Bakari Vuai, Nadra Mohamed, Viwe Hamisi na Ally Nassoro.
Akizungumzia taarifa, kwamba UVCCM ina mpasuko na kuwapo taarifa za kufukuzana, Shigela alisema umoja huo hauna mpasuko na hakuna mjumbe aliyefukuzwa.
Alisema vikao viliendeshwa kwa utaratibu mzuri na kama kuna watu waliamua kutangaza kuwapo mpasuko ndani ya umoja huo, zilikuwa ni hisia binafsi.
Kuhusu madai kwamba wajumbe walijadili hotuba ya Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamisi na kwamba hawakufurahishwa nayo, Shigela alisema mwanzoni hakukuwa na ajenda za kujadili hotuba ya Mwenyekiti. 
“Hotuba ya Mwenyekiti haikujadiliwa, wajumbe wa Baraza tulikuwa na ajenda zetu na hotuba ya Mwenyekiti ilikuwa kwa ajili ya ufunguzi wa Baraza. Kama kuna wajumbe wanaona hotuba ya Mwenyekiti imewadhalilisha, huwezi kuzuia watu kutathimini, waliamua kutoa hisia zao,” alisema
Alisema huwezi kubishana na hisia za mtu mmoja mmoja na kwa maana hiyo huwezi kuzuia watu kuzungumza na kusisitiza kutokuwapo mtafaruku na wananchi waelewe UVCCM ni imara na haina mgogoro wowote.
Shigela alisema hakukuwa na mtu aliyefukuzwa kwenye mkutano huo na hata wajumbe wawili walioteuliwa kuingia kwenye Baraza hilo, Rashid Msarika na Paul Makonda hawakufukuzwa, bali hawakuthibitishwa.
Alifafanua, kwamba kwa utaratibu wa UVCCM, baada ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza, majina yao hupelekwa barazani kuthibitishwa, lakini walionekana kuwa hawakuwa tayari kwa ajili hiyo.
Alisema kutokana na hali hiyo, yatapendekezwa majina mengine mawili kwani wameonesha hawako tayari kufanya kazi na UVCCM.
“Wajumbe hao wawili walikuwa hawajathibitishwa, kwa hiyo huwezi kusema wameenguliwa au wamefukuzwa,” alisema Shigela.
Shigela alisema Baraza Kuu ndilo linalothibitisha uteuzi wa wajumbe wa Baraza, lakini wajumbe hao walisema kuwa hawako tayari kwa hilo.
Akitoa maazimio ya UVCCM, Shigela alisema Baraza Kuu lilitoa maazimio kadhaa likiwamo la mikoa na wilaya zote Tanzania Bara, kuwa na maeneo ya kilimo ili kuunga mkono Sera ya Kilimo Kwanza.
Alisema umoja huo una jukumu la kutathimini hali ya kisiasa na kupendekeza njia za kukabiliana na hali hiyo na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha hali ya kisiasa inakuwa ya amani na utulivu, ili kuwezesha utekelezaji wenye mafanikio ya Ilani ya CCM.
Maazimio mengine ni kuongezwa kwa mitaala, likiwamo somo la ujarisiamali katika vyuo vikuu, ili wanafunzi wanapomaliza shule, wawe na elimu itakayowawezesha
kujiajiri.
Pia viongozi wa UVCCM mikoa na wilaya, wameagizwa kusimamia mikopo ya vijana na wanawake katika halmashauri zao, ili wapate kama inavyoelekezwa na Serikali.
Shigela alisema Baraza hilo limeelekeza mikoa ianze jitihada za kujitegemea kwa kuanzisha miradi mipya na pia Serikali iweke utaratibu mzuri kwa wajasiriamali wadogo  kama vile boda boda na wamachinga,  kuendesha shughuli zao bila kubughudhiwa na vyombo vya Dola.
Alisema Baraza hilo limeelekeza jitihada za  kujitegemea kiuchumi zipewe msukumo zaidi na kamati ya utekelezaji iendelee kusimamia miradi ya zamani na mipya.
Katika miradi hiyo, alisema Baraza Kuu limedhamiria uendelezaji wa kiwanja kilichopo jengo la Makao Makuu, Makontena ya Darajani Zanzibar na Kiwanja cha Igoma na Nyamagana, Mwanza.

No comments: