JENGO LA ATCL KUPIGWA MNADA KWA DENI LA DOLA 700,000...

Jengo la ATCL lililoko kando ya Barabara ya Ohio.
Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, imeamuru jengo la Shirika la Ndege nchini (ATCL) lifanyiwe tathmini kujua thamani yake kabla ya kutoa amri ya kuliuza ili kufidia deni la dola 716,259.52 za Marekani ambazo ni sawa na zaidi  na Sh bilioni moja inazodaiwa na kampuni ya Leisure Tours and Holidays Limited.
Hatua hiyo inatokana na kampuni hiyo kuiomba Mahakama kuamuru jengo hilo lililopo barabara ya Ohio, Dar es Salaam liuzwe ili kufidia deni hilo ambalo lililotokana na kutoa huduma ya usafiri kwa wateja wa shirika hilo tangu mwaka 2008.
Katika amri hiyo iliyotolewa Februari 11, Jaji Robert Makaramba aliagiza taarifa ya tathmini ya jengo iwasilishwe mahakamani leo na kesi imepangwa kuendelea Februari 25, kwa uamuzi.
Kwa mujibu wa hati ya madai katika kesi hiyo, deni hilo lilitokana na  kampuni hiyo kutoa  huduma za usafiri kwa ATCL tangu mwaka 2008 bila kuwasilisha malipo kama walivyokubaliana.
Ilidaiwa kuwa Januari 16, 2008, ATCL ilikuwa ikidaiwa dola 313,759 na kuahidi kulipa deni hilo kwa awamu tatu kuanzia Februari hadi Aprili, 2008,lakini kampuni hiyo ilibaini upungufu kadhaa na kufanya marekebisho ya deni na kuwa dola 321,016.
Machi 31, 2008, deni liifikia dola 367,097 kulingana na hati za malipo ya Januari 17 na Machi 31, 2008  pamoja na riba ya asilimia mbili.
Ilipofika Machi 31, 2008, ATCL haikulipa deni hilo na hadi Mei 30, 2008, deni liliongezeka hadi dola 418,305, ATCL ikapendekeza kuanzia Juni 6, 2008  ilipe dola 30,000 na baadaye dola 5,000 kila mwezi.
Kwa mujibu wa hati hiyo, kampuni hiyo ilikubali mapendekezo hayo, lakini ikaomba ilipwe riba ya asilimia 1.5 ya deni kila siku na hadi Februari 3, 2009, deni likawa limefikia dola 596,382.
Kutokana na kutolipwa deni, kampuni hiyo ilifungua kesi mahakamani ili kudai haki zake na kukubaliana kuwa ATCL italipa deni hilo.
Novemba 20 mwaka jana, Mahakama iliitaka ATCL kupeleka mahakamani mchanganuo wa jinsi itakavyolipa deni hilo, hata hivyo ilishindwa kutimiza amri hiyo na kampuni hiyo kuwasilisha maombi ya kukamatwa na kuliuza jengo lao.
ATCL kwa kipindi kirefu imekuwa ikisuasuakutokana na kukosa ndege za kutosha kufanya biashara ya huduma za kusafirisha abiria ndani na nje ya nchi huku kampuni zingine za binafsi katika tasnia hiyo zikishamiri na kuiacha kama mtoto mkiwa.

No comments: